Juni 05 kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Mazingira Duniani tukio muhimu lililoasisiwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1972 kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira. Uhifadhi wa mazingira umekuwa ni fursa na ni vema kuangazia namna mtu mmoja mmoja anaweza kushiriki kwa vitendo na kunufaika.
Katika muktadha wa Tanzania, siku hii inabeba uzito wa pekee kwani changamoto kama uchafuzi wa mazingira, matumizi holela ya plastiki, uharibifu wa vyanzo vya maji na mabadiliko ya tabianchi zimeanza kuwa sehemu ya maisha ya kila siku.
Katika hali ya kawaida, huenda mtu mmoja asione namna mazingira yanavyoweza kuhusiana na hali yake ya kiuchumi. Lakini kwa mtazamo wa kina, mazingira yanatoa fursa nyingi zisizo na kikomo za kupunguza gharama za maisha na hata kuongeza kipato kwa ubunifu na matumizi sahihi ya rasilimali zinazopatikana kirahisi.
Katika nyakati hizi ambapo gharama za maisha zimepanda kwa kasi, mtu anaweza kuanza kwa kutumia maji ya mvua kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani. Kwa kuweka mifumo rahisi ya kuvuna na kuhifadhi maji hayo, familia inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama ya bili ya maji, hasa katika msimu wa mvua.
Kadhalika, kwa kutumia mwangaza wa jua kupitia taa na majiko ya sola, gharama za umeme au mafuta ya taa hupungua sana. Ni wazi kuwa teknolojia rafiki kwa mazingira imeanza kuwa rafiki pia wa mifuko ya watu binafsi, hasa kwa kuwa inahitaji matunzo kidogo na ni ya muda mrefu.
Hata taka zinazozalishwa majumbani ambazo mara nyingi huonekana kama mzigo zinaweza kuwa chanzo cha kipato. Biashara ya kuchambua na kuuza taka kama plastiki, karatasi, chupa na chuma imeendelea kukua kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam. Vijana wengi wameunda vikundi vya kuchakata taka na kuuza bidhaa zilizotengenezwa kwa kutumia malighafi hizo, hivyo kujipatia ajira na kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa wakati mmoja.
Fursa nyingine inayojitokeza kwa urahisi ni kilimo cha mjini. Hii ni njia nyepesi ya kuzalisha chakula kwa kutumia nafasi ndogo kwa kutumia ndoo ama vyungu. Mboga kama mchicha, matembele, hoho na sukuma wiki huweza kupandwa kwa kutumia mbolea ya asili kutoka jikoni. Uzalishaji huu ukifanywa na watu wengi na kwa wingi kuna fursa ya kuingia mikataba midogo na migahawa ya karibu kuwasilisha mboga kila wiki.
Kwa wale wanaoishi karibu na maeneo ya asili au mandhari nzuri ya kuvutia, kama fukwe, maporomoko ya maji au milima, wanaweza kufikiria biashara ndogo za kiutalii wa mazingira. Kutoa huduma za kuongoza watalii, kuuza bidhaa za asili kama vikapu, vinyago au vyakula vya kitamaduni, au hata kuweka sehemu ya kulala wageni katika nyumba zao ni njia mojawapo ya kuingiza kipato pasipo kuharibu mazingira.
Uwekezaji wa kijani pia umeanza kupata nafasi pana kwa mtu binafsi. Benki na taasisi za kifedha zimeanza kutoa bidhaa mahsusi kwa miradi ya mazingira kama vile ufugaji wa nyuki, kilimo cha miti, na matumizi ya teknolojia safi.
Taasisi za kibenki na hata bima, zimeanzisha mikopo ya riba nafuu kwa wajasiriamali wa mazingira, pia uwekezaji katika hati fungani zenye mrengo wa kufanya biashara bila kuharibu mazingira. Mikopo hii na bima hizi ni fursa ya kiuchumi ambayo mtu anaweza kuzitumia bila kuwa na sharti kubwa la dhamana ama kulipia gharama kubwa za bima kama ilivyokuwa awali.
Kwa kuzingatia haya yote, Siku ya Mazingira Duniani mwaka 2025 ni yakujitafakari sio tu kwa ajili ya sayari, bali kwa ajili ya maisha bora na ya gharama nafuu. Mazingira yanapohifadhiwa, uchumi wa mtu binafsi nao huimarika na hivyo maisha kuwa endelevu kwa wote.