Hii ndio sababu ya Mahujaji kukusanyika Arafa

Dar es Salaam. Ibada ya Hijja imeanza na leo Mahujaji kutwa nzima wanakusanyika  katika viwanja vya Arafa nje kidogo ya Mji Mtukufu wa Makka nchini Saudi Arabia.

Ni viwanja ambavyo miaka zaidi ya miaka 1,400 iliyopita, kiongozi wa Waislamu, Mtume Muhammad (Rehma na amani zimshukie) alitoa kile kiitwacho Hotuba ya Kuaga, iliyokuwa ya mwisho kwake na iliyoutangaza rasmi Uislamu kuwa dini ya ulimwengu mzima.

Kwa mahujaji, kufika kwenye eneo hilo ni sehemu muhimu ya ibada hiyo na takribani kilele cha imani, kwani kunawakumbusha siku ya makutano ya wanaadamu wote mbele ya Muumba wao, yaani Siku ya Kiama.

Mahujaji wapo viwanja hivyo katika eneo la Mlima Arafa kwa ibada na dua kuanzia alfajiri  hadi jioni, na baada ya machweo ya watakwenda kwenye viwanja ya Muzdalifah kukusanya vijiwe vitakavyotumika kwenye sehemu ya ibada inayoitwa kumrushia mawe ibilisi.

Umuhimu wa Arafa unatajwa kuwa ndilo eneo ambalo mahujaji wanamlilia Mola wao kwa madhambi waliyofanya wakiomba msamaha sambamba na maombi mbalimbali yakiwamom yanayohusu imani na hata masuala ya kimaisha. Zaidi ya mahujaji milioni 1.5 wamekusanyika katika viwanja hivyo mwaka huu.

Kwa mujibu wa mafunzo ya Mtume Muhammad (Rehma na amani zimhuskie), Siku ya Arafa ni siku tukufu, kwani ni siku ambayo Mwenyezi Mungu mwenyewe hujikaribisha zaidi kwa waumini na kuwasemehe madhambi yao.

Safari ya kuelekea Arafa ilianza jana Jumatano, kwa wengi wa mahujaji kutembea kwa miguu wakiwa wamebeba mizigo yao, huku hali ya hewa ikikadiriwa kufikia nyuzijoto 40.

Hata hivyo, katika kuelekea ibada hiyo leo Juni 5, 2025 Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuber ameandaa dua maalum ya kuiombea nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu.

“Kwa mwaka huu jambo kubwa tumelielekeza kuwa Mahujaji wote wa Tanzania na kwa taasisi zote kwamba kazi kubwa ya kuifanya mwaka huu ni lile jambo lililo mbele yetu sisi katika nchi yetu, nalo ni jambo la uchaguzi mkuu liweze kupita salama na amani, “amesema Mufti Zuber akinukuliwa na mtandao wa Bab Deo Miladu.

Pia amesema wanaliombea Taifa amani, utulivu, upendo, na mshikamano, ili Mwenyezi Mungu aepushe na hali yoyote ya vurugu katika nchi.

“Nchi yetu iendelee kuwa na msingi wa amani, ishara ya upendo, na hali ya utulivu. Hiyo ndiyo kazi yetu kuhakikisha kila eneo linafikiwa na ujumbe wa matumaini na mshikamano. Kazi yetu ni kufanya dua na ibada maalumu kwa pamoja, ili kuiombea nchi yetu iendelee kuishi kwa amani na kuiombea siku ya kesho iwe salama zaidi,” amesema Mufti.

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amesema hali ni njema, kwani Arafa ya leo ni kushinda kwenye mahema makubwa yenye viyoyozi si ile ya mwaka 2007 ya kukusanyika chini ya mlima Arafa.

“Kubwa ni dua kwa nchi yetu na watu wake hasa tunapoelekea uchaguzi mkuu na uwepo wa ishara ya changamoto za kisiasa na kijaami,” amesema Sheikh Mataka.

Sheikh Mataka ameushukuru Ufalme wa Saudia kwa maboresho na miundombinu inayorahisisha ibada Hijja na kuondoa changamoto zilizokuwa zinasababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo vitokanavyo na a misongamano isiyo ya lazima, jua kali na joto lisilohimilika.

Kwa upande wake, mwanaharakati Fatma Karume (Shangazi) ametoa wito kwa Waislam wenye uwezo kwenda Makka kuhiji

“Nawaasa waislamu wenzangu wote wenye uwezo wakipata nafasi wawe wanakuja kufanya ibada,”amesema Fatma.

Mwaka huu, Saudi Arabia imetumia mabilioni ya dola kwenye hatua za kudhibiti usalama wa mahujaji, lakini kiwango kikubwa cha mahujaji kinaonekana kuzifanya hatua hizo kuwa na athari ndogo kwenye usalama wao. Mojawapo ya changamoto kubwa kabisa kwenye hija za miaka ya karibuni imekuwa ni kiwango kikubwa cha joto.

Katika kutambua hilo Wizara ya Ulinzi ya Saudia Arabia wametumia ndege maalumu ili kukabiliana na dharura ya matibabu wakati wa msimu wa hija kwa msimu huu.

Wizara pia imetoa magari ya kisasa ya kubebea wagonjwa kwa ajili ya kuhamasisha wagonjwa wa dharura kutoka maeneo ya ibada  kwenda hospitali ndani na nje ya Mji Mtukufu wa Makka.

Related Posts