Karatu. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema ilani mpya ya uchaguzi ya mwaka 2025/30 iliyozinduliwa hivi karibuni, imebeba masuala muhimu yanayogusa maisha ya Watanzania.
Aidha, amesema mwaka huu, chama hicho kimejipanga kushinda kwa kishindo kwa kuhakikisha inapeleka wagombea wazuri ili wachaguliwe.
Makalla ameyasema hayo leo Alhamisi Juni 5, 2025 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mazingira Bora, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Amesema ilani hiyo imetokana na tathmini ya ilani iliyopita kwa kufanya tafiti na kushirikisha wananchi na wadau mbalimbali, ili kubaini vipaumbele na mahitaji muhimu ya Watanzania.
“Ilani hii inazungumzia kukuza ajira, kukuza uchumi na kuwawezesha Watanzania kimaisha na ustawi wao, itashughulikia changamoto zote zinazokabili Watanzania na muda utakapofika tutainadi.
“Tunawaahidi, ilani inakwenda kushughulika na maisha ya Watanzania na muda utakapofika tutakuja kuinadi na hakuna chama chenye ilani nzuri zaidi ya CCM,” ameongeza Makalla.
Kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu, amewataka Watanzania wakatae viongozi au wagombea wanaowagawa kwa udini au uchochezi.
“Wakataeni viongozi, wagombea watakaotugawa kwa udini, uchochezi, watakaohatarisha amani ya nchi yetu, nataka niwakumbushe wanaKaratu, hatuna Karatu wala Tanzania nyingine, tuendelee kudumisha amani, tubishane kwa hoja, itikadi lakini Tanzania ibaki salama. Tuwakate viongozi wanaopandikiza chuki ya kutugawa Watanzania,” amesema.