Mashtaka ya uhujumu uchumi, uhalifu wa kupangwa kufunguliwa bila idhini ya DPP

Dodoma. Bunge limepitisha marekebisho ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa na sasa mashtaka yanayohusiana na makosa chini ya sheria hiyo yatafunguliwa bila kuhitaji idhini ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Hatua hiyo inalenga kuharakisha mchakato wa uendeshaji wa mashauri na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.

Marekebisho hayo yamewasilishwa bungeni kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2025, unaohusisha mabadiliko katika jumla ya sheria tisa tofauti.

Sheria nyingine zilizofanyiwa marekebisho ni  katika muswada huo ni Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani.

Nyingine ni ya Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sheria ya Bandari, Sheria ya Leseni za Usafirishaji na Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini.

Sheria nyingine  ni Sheria ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Sheria ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu.

Akifafanua kuhusu marekebisho ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa nje ya ukumbi wa Bunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Joseph Mhagama amesema kilichobadilika baada ya marekebisho hayo ni ufunguaji wa mashtaka hayo kutolazimisha kuwepo kwa idhini ya mkurugenzi wa mashtaka.

“Kabla ya hapo, sheria ilitaka idhini ya ya Mkurugenzi wa Mashtaka ili kufungua kesi, lakini sasa hivi kutokana na kuboreshwa kwa ofisi ya mwendesha mashtaka kuna mawakili wa Serikali kila mahali wanaoweza kusimamia hilo,” amesema.

Dk Mhagama amesema hatua hiyo inalenga kuondoa ucheleweshaji wa kesi na kupunguza idadi ya watuhumiwa wanaolazimika kukaa mahabusu kwa muda mrefu wakisubiri kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka, hasa kwa makosa ambayo kisheria hayana dhamana.

Aidha, amesema marekebisho hayo hayajaondoa mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuamua kuondoa kesi mahakamani, kwani bado anabaki kuwa msimamizi mkuu wa waendesha mashtaka nchini.

Awali, akiwasilisha muswada huo leo Juni 5, 2025, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amesema unapendekeza kufanyika marekebisho katika Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa ili kuboresha uendeshaji wa mashauri yanayoangukia chini ya sheria hiyo.

Amesema kuwa, kifungu cha 26 cha sheria hiyo kinapendekezwa kufutwa, lengo la marekebisho hayo ni kuruhusu mashtaka yanayoangukia chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi kufunguliwa bila kuhitaji ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka.

 “Takwa la ridhaa ya mkurugenzi wa mashtaka kabla ya kufungua shtaka chini ya sheria hii liliwekwa miaka ya nyuma, sehemu kubwa ya mashtaka yalikuwa yanaendeshwa na askari polisi kwa kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka haikuwa imeenea katika mikoa na wilaya zote nchini,” amesema.

Amesema hivyo, awali kulikuwa na umuhimu wa kupata ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka ili kudhibiti ufunguaji holela wa mashtaka.

“Katika mazingira ya sasa ambapo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imefungua ofisi zake hadi ngazi ya wilaya na kesi zote za jinai zinaendeshwa na mawakili wa Serikali wanaowajibika moja kwa moja kwa mkurugenzi wa mashtaka,”amesema.

Amesema, masharti ya kupata ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka yanakosa mantiki ya kuendelea kuwepo na yanaweza kuchangia ucheleweshaji wa haki jinai.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Seif Gulamali amesema maoni ya kamati ni kuwa, marekebisho hayo yamejikita katika misingi ya Haki Jinai yanayoakisi Falsafa ya 4R za Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kwa kuwa, mashauri yote yanayohitaji ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchi nzima ni lazima yafike kwa mkurugenzi wa mashtaka mwenyewe, kamati inakubaliana na mapendekezo ya marekebisho yanayoondoa sharti hilo kwa kuwa yataondoa mlundikano wa mahabusu gerezani,”amesema.

Mbunge wa Muleba Kusini (CCM) Oscar Kikoyo amesema anaungana na marekebisho yaliyoletwa na Serikali ya kuondoa takwa la kutaka idhini ya Mkurugenzi wa Mashtaka kabla ya kesi kufunguliwa.

“Kuruhusu kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi bila idhini ya Mkurugenzi wa Mashtaka itasaidia kupunguza mlundikano wa kesi katika Mahakama za wilaya na watu wakapata haki haraka sana,”amesema.

Hata hivyo, ameomba kuboreshwa ofisi za wilaya na zisizokaa vizuri kwa kupatiwa vitendea kazi vya kutosha.

Related Posts