Mradi wa Sh270 bilioni kupunguza bei ya gesi kwa asilimia 40

Tanga. Sekta ya nishati ya Tanzania inatarajiwa kupitia mageuzi makubwa kufuatia uwekezaji wa dola 100 milioni (Sh270 bilioni) kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kimataifa cha gesi ya kupikia jijini Tanga (LPG).

Kituo hicho ambacho ni ushirikiano kati ya kampuni ya Asas Limited na kampuni ya Uingereza ya Petredec, kitajengwa Chongoleani mkoani Tanga.

Baada ya kuanza kufanya kazi, kinatarajiwa kupunguza bei ya gesi ya kupikia hadi asilimia 40, hivyo kufanya nishati hiyo safi kuwa nafuu zaidi nchini na kupanua upatikanaji wake kwa nchi jirani na zisizo na bandari, ikiwemo Zambia.

Mradi huo ulizinduliwa Jumatano katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi iliyoongozwa na Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2027.

Ukijengwa kwenye eneo la hekta 26 katika Ghuba ya Tanga, awamu ya kwanza ya kituo hicho itakuwa na matanki sita ya kuhifadhia gesi yenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 40,000, maeneo nane ya kuegesha malori, pamoja na bomba la chini ya bahari, lenye urefu wa kilomita 2.8.

“Mradi huu unachangia maono yetu ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanapata nishati safi ifikapo mwaka 2034,” alisema Dk Biteko, akitambua juhudi za Serikali katika kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji.

Alisema matumizi ya LPG yameongezeka kutoka tani 300,000 mwaka 2022/23 hadi tani 400,000 mwaka 2023/24 kutokana na kampeni ya kitaifa ya nishati safi.

Amewasihi wawekezaji kuwapa kipaumbele wakandarasi wa ndani wakati wa ujenzi ili kuchochea ajira na ukuaji wa uchumi.

“Endapo kazi ndogo ambazo Watanzania wanaweza kufanya watapewa wageni, uchumi wetu hauwezi kukua,” amesema. “Mradi huu ni kama ule wa umeme wa Chalinze – Dodoma; ni lazima tuulinde.”

Aidha, Dk Biteko ametoa wito kwa sekta ya LPG kuhakikisha inawafikia watu wa vijijini.

“Tulete teknolojia ndogondogo zenye masharti nafuu ya malipo kama vile mifumo ya ‘Lipa Kadri Unavyotumia’. Siyo kila mtu anaweza kununua mtungi mzima kwa mara moja,” alisema

Mwakilishi wa Asas Group, Ahmed Salim Abri amesema kituo hicho kitapunguza gharama za ununuzi wa gesi kwa jumla na hivyo kufanya bei ya gesi iwe nafuu zaidi.

“Tutamiliki pia meli ya kusafirisha gesi ili kupunguza gharama za uendeshaji,” ameongeza huku akieleza kuwa kituo hicho kinauzidi kwa ukubwa mradi wa Petredec ulioko Afrika Kusini na kitasaidia kupunguza utegemezi wa Afrika Mashariki kwa gesi kutoka Russia na masoko mengine ya mbali.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Buriani ameusifia mradi huo akisema utakuwa kichocheo cha maendeleo ya ndani.

“Mradi huu utaifanya Tanga ijulikane duniani. Unatarajiwa kuleta ajira zaidi ya 1,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, na hivyo kuongeza kipato cha mkoa,” alisema.

Mkurugenzi wa Petredec kwa Afrika, Michael Demond amesema miundombinu ya kiwango kikubwa ni muhimu kwa upatikanaji wa gesi ya kupikia kwa bei nafuu na ya uhakika.

“Tunajivunia kushiriki katika mradi huu wa mageuzi. Kituo cha Tanga kitaiweka Tanzania kuwa kitovu cha nishati safi kwa Afrika Mashariki,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Mafuta na Gesi Tanzania, Abdulsamad Abdulrahim amesema kampuni za ndani ziko tayari kushiriki.

“Hii ni fursa ya kuonyesha uwezo wa Watanzania katika masuala ya usafirishaji, usalama, masoko na huduma za kiufundi. Hatupo pembeni—tupo kwenye uwanja na tuko tayari kutekeleza,” alibainisha.

Related Posts