Dar es Salaam. Mtanzania aliyejulikana kwa jina la Iqbal Baghdad, amefariki akiwa nchini Saudi Arabia kutekeleza ibada ya Hijja.
Hujaji huyo amefariki jana katika mji wa Madina kabla ya kuanza kwa Manasiq yaani mfululizo wa ibada za Hijja ambapo leo mahujaji wanakusanyika katika viwanja vitakatifu vya Arafa, ikiwa ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa ibada hiyo ya Hijja ambayo ni nguzo ya tano ya dini ya Uislam.
Kifo hicho kimethibitishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka aliyezungumza na Mwananchi akiwa nchini Saudi Arabia anapotekeleza ibada hiyo.
Kwa mujibu wa Sheikh Mataka hali katika viwanja vya Arafa ambavyo Mahujaji watakuwa hapo kwa kutwa nzima ya leo ni salama akisema: ‘’Hali ni njema. Arafa ya leo ni kushinda katika mahema makubwa yenye viyoyozi si ile ya mwaka 2007 ya kukusanyika chini ya Mlima Arafa. Things made simple, flexible and comfortable (mambo sasa yamerahisishwa na tunapata faraja).
Viwanja vya Arafa viko takriban kilomita 15 kutoka mji wa Makka. Wakiwa hapo mahujaji hufanya dhikri na dua mbalimbali, wakijikurubisha kwa Mola wao Mtukufu. Ni eneo ambalo pia hotuba ya Hijja hutolewa.
Endelea kufuatilia mitandaio ya Mwananchi kwa habari zaidi kuhusu Ibada ya Hija kwa mwaka 2025.