Raia wa Kenya aliyedai ni Mtanzania, afukuzwa nchini

Tanga. Kuna usemi unaosema ukiwa muongo uwe na kumbukumbu, hiki ndicho kilichomuumbua raia wa Kenya, Mbaraka Mbaraka aliyekuwa anapinga kufukuzwa akidai ni Mtanzania, akasahau kuna mahali alikiri ni raia wa Kenya.

Mamlaka za Tanzania zimesisitiza kuwa kitambulisho cha Taifa cha Tanzania kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), pasi ya Kusafiria ya Tanzania na cheti cha kuzaliwa alivyokuwa navyo, vilipatikana kinyume cha sheria.

Agosti 31,2022, Mbaraka alifurushwa nchini na Jeshi la Uhamiaji na kurejeshwa kwa nguvu Kenya kupitia PI namba 0077001, lakini akarejea nchini na kufungua maombi ya mapitio ya Mahakama (Judicial review), kupinga uamuzi wa Serikali.

Hata hivyo, ni Mbaraka huyohuyo ambaye alisahau kuwa aliwahi kufungua maombi ya talaka namba 20 ya 2022 dhidi ya Khadija Fidali, ambapo alikiri mahakamani kuwa yeye ni raia wa Kenya na ndoa yao ilifungwa nchini Kenya.

Akitoa uamuzi wake juu ya maombi hayo ya mapitio ya 2024, Jaji Katarina Mteule wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Tanga, alisema inaonekana Mbaraka ana hati ya kusafiria ya Kenya iliyotolewa huko Mombasa.

“Kupatikana kwa nyaraka hizi hususan mwenendo wa kesi ya talaka ikionyesha yeye ni raia wa Kenya na uwepo wa hati ya kusafiria katika nchi ambayo hairuhusu uraia pacha, mtoa maamuzi angefikia uamuzi sawa na wa uhamiaji,”alisema Jaji.

Jaji aliongeza kusema kuwa:-“Mamlaka yoyote yenye kufikiri sawasawa lazima ingehoji uadilifu wa mwombaji kwa kuwa na nyaraka kutoka nchi zote mbili na kumtangaza kama mhamiaji haramu. Uamuzi wa kumfukuza ulikuwa na mantiki.

Kulingana na Jaji alisema kwa uchambuzi huo, suala la kama kukamatwa kwa muombaji, kurejeshwa kwao na kutamkwa ni mhamiaji haramu kulikuwa kinyume cha sheria na taratibu zilikiukwa, Mahakama inaona taratibu zote zilifuatwa.

Kwa msingi huo, Jaji Mteule ameyatupilia mbali maombi hayo ambayo yalikuwa ni dhidi ya Kamishina Jenerali wa Uhamiaji, Kamishna wa Mipaka, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Tanga na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama wajibu maombi.

Alichokuwa akiiomba Mahakama

Raia huyo wa Kenya, alikuwa anaiomba Mahakama itamke kuwa uamuzi wa mjibu maombi wa kwanza hadi wa tatu kama chombo cha utawala na uamuzi wa Novemba 24,2022 wa kumfukuza kutoka nchi yake ulikiuka sheria na taratibu.

Pia alikuwa anaiomba Mahakama itamke kuwa hakupewa fursa ya kusikilizwa hivyo uamuzi huo utamkwe ni batili na Mahakama itamke kuwa Mbaraka Mbaraka ni raia wa Tanzania na aruhusiwe kuingia na kuishi nchini Tanzania.

Kupitia maombi hayo alikuwa anaiomba Mahakama ifute PI namba 0077001 ya Agosti 31, 2022 na arudishiwe uraia wake na imuamuru kufutwa kwa amri ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji iliyomtaka kuwa yeye sio raia wa Tanzania.

Pia alikuwa anaomba wajibu maombi wamrejeshee uraia wake na aruhusiwe kuingia na kuishi Tanzania na pia wajibu maombi hao kumrejeshee  hati zake za uraia na ya kusafiria vilivyotaifishwa kinyume cha sheria.

Wakili Eric Akaro aliyemtetea Mbaraka alidai mteja wake ni mwathirika wa vitendo visivyo vya upendeleo,  visivyo vya haki vya Idara ya Uhamiaji na kwamba mteja wake ana pasi ya kusafiria namba TAE107593 ya Agosti 31,2022.

Kulingana na wakili huyo, alipinga nyaraka mbalimbali ambazo wajibu maombi wanadai kumkuta nazo mteja wake kwani hapakuwepo hati ya upekuzi.

Katika kiapo chake, Mbaraka alidai yeye ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa na ana cheti cha kuzaliwa na Kitambulisho cha Taifa kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Tanzania (Nida) na amekuwa akiishi na kujipatia kipato jijini Tanga.

Jijini Tanga amekuwa akiishi na mke na kufanikiwa kupata watoto wawili wote ni watanzania, akimiliki mali kadha wa kadha ikiwamo viwanja nchini Tanzania.

Analalamika alifukuzwa nchini Agosti 31,2022 kinyume cha sheria, huku wajibu maombi wa kwanza hadi watatu wakimnyang’anya pasi yake, na kupewa hati ya dharura namba AB0427896 na kurudishwa Kenya kupitia mpaka wa Horohoro.

Haya ndio majibu ya Serikali

Katika kiapo kinzani, wajibu maombi kupitia kiapo cha Ofisa Uhamiaji  Mkoa wa Tanga, Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji (SACI), Phaustine Ngunge, walipinga madai ya Mbaraka lakini wakakiri tu kuwa alifukuzwa nchini.

SACI Ngunge katika kiapo hicho, alieleza kuwa muombaji ni raia wa Kenya kwa kuzaliwa, na kwamba alizaliwa Mombasa huku wazazi wake wote wawili wakiwa ni Wakenya, ambapo aliambatanisha vielelezo kadhaa kuthibitisha hilo.

Vithibitisho hivyo ni Kitambulisho cha Taifa la Kenya na. 13733448, kitambulisho cha mwanafunzi kilichotolewa Mombasa, Kenya, na namba binafsi ya utambulisho A0002733533Q na cheti cha Utambulisho cha Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA).

Mbali na vielelezo hivyo, SACI Ngunge aliambatanisha pia Hati ya kusafiria ya Kenya namba A434067, A044481 na KE 039945 ambavyo uhamiaji iliieleza Mahakama kuwa alikuwa akitumia nyaraka hizo kuingia na kutoka Tanzania.

Wajibu maombi kupitia kiapo hicho, walimtuhumu muombaji huyo kuingia Tanzania kinyume cha sheria na kwa kutumia utambulisho wa uongo, alifanikiwa kujipatia kitambulisho cha Taifa cha Tanzania kutoka Nida kwa njia ya kughushi.

Kulingana na kiapo hicho kinzani, wajibu wanadai muombaji aliwahi kukiri kuwa yeye ni raia wa Kenya kupitia shauri lake la talaka namba 20 la 2022 ambalo kukiri kwake kulisababisha shauri hilo kufutwa kwa kuwa wadaawa ni raia wa Kenya.

Wajibu maombi walisisitiza kuwa taratibu zote zilifuatwa katika kutoa PI namba 0077001 ya Agosti 31,2022 kwa kuwa kulikuwa na upelelezi na muombaji alipewa fursa ya kusikilizwa ikiwa ni kanuni ya msingi ya kisheria ya haki ya kusikilizwa.

Katika uamuzi wake alioutoa Juni 2,2025 na nakala ya uamuzi huo kuwekwa katika mtandao wa Mahakama Tanzania leo Juni 4,2025, Jaji Mteule alisema katika kuthibitisha uraia, kila upande ulikuja na nyaraka kuthibitisha vinginevyo.

Jaji alisema wakili wa muombaji alijenga hoja kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu kutokana na wajibu maombi kutomfikisha kortini mteja wake baada ya kumkamata na kwamba Mahakama ndio ilipaswa kutoa amri hiyo.

 “Hapakuwa na maelezo kutoka kwa mwombaji inayoonyesha kuwa wajibu maombi walitenda wajibu wao nje ya ule wa kisheria. Kamishna wa Uhamiaji anayo mamlaka kumtamka mtu kuwa ni mhamiaji haramu,”alisema Jaji.

Akinukuu kanuni ya 17 ya Uhamiaji, Jaji alisema kutokana na msingi huo, madai kuwa kulikuwa na ukiukwaji kutamka mwombaji ni mhamiaji haramu hayana msingi na kwamba hakufikishwa kortini kwa sababu ya kifungu cha 27 sura 54.

“Kwa mtazamo wangu, uamuzi wa kumtangaza mtu kuwa ni mhamiaji asiyeruhusiwa nchini ukishafanywa na kamishna wa uhamiaji basi ulazima wa kifungu cha 27 cha Sheria ya uraia kinakuwa tena sio lazima,”alisema Jaji.

Kuhusu hoja kuwa muombaji hakupewa fursa ya kusikilizwa, Jaji alisema amepitia nyaraka zilizoambatanishwa na kiapo kinzani na inaonyesha wajibu maombi walifanya uchunguzi kwa mamlaka waliyopewa na kifungu cha 16 sura ya 54.

“Katika uchunguzi huo, nyaraka mbalimbali zilikusanywa kama vile kitambulisho cha taifa cha Kenya namba 13733448, kitambulisho cha mwanafunzi kilichotolewa Mombasa , cheti cha KRA na hati za kusafiria zilizotolewa Kenya,”alisema Jaji.

“Wajibu maombi waliwasilisha pia maelezo ya onyo ya mleta maombi ambayo alielezea hali halisi ya uraia wake. Kwa maoni yangu, kwa kuwa alipewa nafasi ya kutoa maelezo yake ya onyo, inatosha kusema alipewa fursa ya kusikilizwa”

“Wakili Akaro alisema maelezo hayo yalipaswa kutumika katika mahakama na sio kutumiwa na Kamishna wa Uhamiaji. Lakini kama alivyojibu wakili wa Serikali, Rashid Mohamed, hoja hiyo haikupata nukuu au msimamo wowote wa kisheria”

“Sijaona msimamo wowote wa sheria unaokataza kutumika kwa maelezo hayo kuiwezesha mamlaka nyingine kutenda wajibu wake wa kisheria. Kwa msingi huo, hapakuwa na ukiukwaji wowote wa haki ya asili ya kusikilizwa ya mleta maombi”

Kuhusu nyaraka mbalimbali za Kenya, Jaji alisema amepitia nyaraka hizo pamoja na mwenendo wa kesi ya talaka ambazo zinahitimisha muombaji sio raia wa Kenya, huku Jaji akinukuu sehemu ya mwenendo wa shauri hilo la talaka.

Wakili Tumaini Bakari (kwa ajili ya mdaiwa): “Mheshimiwa , shauri linakuja kwa ajili ya kusikilizwa. Kabla ya kuendelea, tuna taarifa kwamba mdai na mdaiwa sio raia wa nchi ya Tanzania. Wote ni raia wa Kenya na ndoa imefungwa Kenya,”

Akaendelea kueleza “Hivyo mheshimiwa kwa mtazamo wa kisheria, Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza shauri hili kwani mdai na mdaiwa  ni raia wa Kenya na ndoa hii imefungwa nchini Kenya. Tunaomba shauri hili liondolewe kwa gharama”

Hakimu Mkazi akamuuliza mdai (Mbaraka) naye akajibu “Ni kweli mimi na mdaiwa ni raia wa Kenya na ndoa yetu imefungwa Kenya”, mwisho wa kunukuu.

Ni kutokana na msimamo huo, Hakimu akatoa uamuzi mdogo kuwa kwa kuwa hakuna ubishi mdai na mdaiwa ni raia wa Kenya na ndoa yao imefungiwa Kenya, basi mahakama hiyo haina mamlaka ya kuendesha shauri hivyo linaondolewa.

Jaji alisema mbali na mwenendo huo, lakini inaonekana mleta maombi anamiliki pasi ya kusafiria ya Kenya iliyotolewa na mamlaka ya utoaji pasi Mombasa.

“Kwa nyaraka hizi hususan mwenendo huo wa kesi ambao ulithibitisha mleta maombi ni raia wa Kenya na uwepo wa pasi ya kusafiria ya Kenya ambayo hairuhusu uraia pacha, mamlaka yoyote ingefikia uamuzi kama wa uhamiaji”

Ni kutokana na uchambuzi huo, Jaji alisema Mahakama inaona maombi hayo ya mapitio ya mahakama haya mashiko hivyo inayatupilia mbali, na uamuzi wa kumfurusha nchini muombaji ulikuwa sahihi na hakukiuka taratibu wala sheria.

Related Posts