Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amelipongeza Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa wazo la kujenga kituo kwa ajili ya watoto wenye uhitaji maalumu huku akieleza kuwa, huo ndiyo utumishi wa dini.
Amesema KKKT imeendelea kuonesha kwa vitendo namna inavyoshirikiana na Serikali kusaidia jamii hasa katika elimu na afya huku ikifanya kazi kubwa katika ujenzi wa maadili ya jamii.
Rais Samia amesema hayo leo Alhamisi Juni 5, 2025 wakati wa harambee iliyoandaliwa na kanisa hilo kwa ajili ya kuchangisha fedha zitakazotumika kujenga kituo hicho eneo la Kitopeni, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
“Ninatambua, mbali ya kuhubiri injili, KKKT imekuwa na dhima kubwa ya kutoa huduma za kijamii ikiwamo elimu na afya. Huu ni mwendelezo wa kile kinachofanywa na kanisa hili.

“Huu ndio utumishi wa dini, kazi hii mnayoifanya inapeleka ujumbe kwa wale waliojionesha kuwa ni watumishi wa dini lakini kumbe ni watumishi wa shetani au mambo mengine. Utumishi wa dini ni kujenga jamii yenye maadili,” amesema Rais Samia.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amekiri suala la watoto wenye ulemavu wa akili ni tatizo kubwa, hivyo ipo haja ya kuchukuliwa kwa uzito wake kulisaidia kundi hilo linalozidi kuongezeka.
“Nakubaliana na Baba Askofu kwamba tatizo bado ni kubwa ingawa tatizo hili halichagui dini licha ya kuwa kituo kinajengwa na kanisa. Hili ni tatizo kubwa ambalo tunatakiwa kusimama wote kwa pamoja na kulifanyia kazi.
“Bahati mbaya, miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wenye matatizo ya akili hasa utindio wa ubongo. Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiria katika watoto 100 wanaozaliwa, mmoja ana tatizo la usonji,” amesema Rais Samia.
“Takwimu hizi zinatukumbusha kuhusu ukubwa wa tatizo hili na kuweka afua za kukabiliana nalo, hivyo Serikali tutashirikiana na kanisa katika ujenzi na uendeshaji wa kituo hiki. Tunataka kituo hiki kiwe cha mfano kuwezesha watoto hawa kupata elimu na usaidizi.”
Katika harambee hiyo, Rais Samia na ofisi yake imechangia jumla ya Sh250 milioni huku akiahidi Serikali itaendelea kushirikiana na kanisa kuhakikisha lengo la kuwa na kituo hicho linatimia.

“Ninapoalikwa kwenye mambo makubwa ya kanisa, kiwango changu cha kuchangia nimejiwekea ni Sh100 milioni lakini leo kwa maajabu makubwa washauri wangu sita ndani ya ofisi yangu, nao wanakuja na Sh100 milioni. Nikivaa kofia ya bibi, nitawachangia wajukuu zangu Sh50 milioni, hivyo jumla kutoka ofisi ya mama itakuwa Sh250 milioni,” amesema.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameipongeza KKKT kwa kudumisha amani na umoja katika Taifa na kuwasihi waendelee kushirikiana na Serikali katika kujenga jamii yenye maadili mema.
“Niwaombe tuendelee kuihubiri na kuiomba amani kwa ajili ya nchi yetu, hasa katika kipindi hiki ambacho tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu,” amesema.
Awali, Mkuu wa KKKT na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa amesema wazo la kujenga kituo hicho ni matokeo ya utafiti uliofanywa katika mataifa mbalimbali ukilenga kuangalia namna ya kuwasaidia watoto wenye ulemavu wa akili.

“Tulifanya utafiti katika nchi mbalimbali ikiwamo Ujerumani, Finland na China kuangalia ni kwa namna gani watoto wenye ulemavu wa akili wanashiriki kwenye shughuli za ujenzi wa Taifa.
“Dayosisi imechukua hatua thabiti kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi, sisi tulio hai tunyooshe mikono yetu. Hadi sasa tumepata eneo ambalo tunatakiwa kumalizia taratibu za umiliki, tayari tumeanza michoro ya usanifu wa majengo na imekamilika,” amesema.
Amesema mafanikio ya mradi huu yanahitaji ushirikiano kati ya kanisa, Serikali na sekta binafsi, hivyo kanisa limedhamiria kulijafanya jambo hilo kuwa endelevu kuondoa uwezekano wa watoto wenye ulemavu wa akili kuzurura mitaani.
Askofu Malasusa amesema tatizo la watoto wanaozaliwa na ulemavu wa akili limezidi kuongezeka, hivyo hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa kuhakikisha watoto hao wanaishi vyema katika jamii ikiwa ni pamoja na kupata elimu.
Akizungumza kwenye harambee hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameitaka Serikali kuwa na utaratibu wa kuzifuatilia taasisi za dini ili zisitoe mahubiri yanayoweza kupotosha Taifa.
Amesema hiyo itasaidia kuziondolea usajili taasisi zenye mahubiri na mafunzo yanayoweza kuwa sumu kwa Taifa.
Kauli ya Chalamila imekuja siku chache baada ya Serikali kulifutia usajili Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima kwa kile kilichoelezwa, mahubiri yake yana uelekeo wa kisiasa unaolenga kuichonganisha Serikali na wananchi, ikiwa ni siku moja tangu kiongozi huyo wa kiroho atangaze msimamo wake wa kuendelea kukemea vitendo vya utekaji na watu kupotea.

Kwa mujibu wa Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa kanisa hilo limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.
Chalamila akitolea mfano wa kanisa alilolitembelea hivi karibuni ambalo kiongozi wake alitoa mahubiri ya uongo amesema, “nafikiri tuwe tunafanya vetting (uchunguzi) mara kwa mara kwenye hizi taasisi za dini ili kuhakikisha Taifa halipati sumu kupitia mahubiri yanayotolewa.”
Chalamila pia amezungumzia watu wanaopotosha umma na kumuhusisha Rais Samia Suluhu na familia yake na umiliki wa mali nyingi akieleza kuwa habari hizo ni za upotoshaji.
“Nikupe pole Rais kwa unachopitia, watu wachache wameamua kukusema wewe na familia yako kwamba mnajilimbikizia mali. Haya maneno wakati mwingine wanaoyasema hata hawaelewi.
“Siku moja nikiwa nafanya mazoezi nilikutana na mtu akaniambia kituo cha mafuta kilichopo katika eneo hilo ni cha mtoto wa Rais na akasisitiza huwa anakuja pale, bahati nzuri huyo mtoto wa Rais akapita nikamuuliza unamjua yule akasema hamjui nikamwambia huyo sasa ndio mtoto wa Rais.”
Chalamila amesema suala la kuhusisha familia ya kiongozi aliyeko madarakani na ulimbikizaji mali lilitokea pia kwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete lakini uvumi huo ulimalizika baada ya kutoka madarakani.