Sababu Waislam kuchinja Sikukuu ya Eid Udh-hiya

Ibada ya kuchinja (Udh-hiya) ni miongoni mwa alama kuu za Uislamu, ambapo Muislamu anakumbushwa kumwamini Allah Mtukufu kwa kumtakasia ibada, kumshukuru kwa neema Zake, na kufuata utiifu wa Baba yetu Ibrahim (Amani iwe juu yake) kwa Mola wake.

Ibada hii ina baraka nyingi na kheri, hivyo ni Sunna iliyosisitizwa kwa Muislamu kuipa umuhimu na kuiheshimu.

Udh-hiya ni mnyama anayefugwa mfano wa ngamia, ng’ombe au kondoo anayechinjwa kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allah Mtukufu.

Huchijwa kwa nia ya ibada kuanzia baada ya Swala ya Idi ya kuchinja (Id Al-Adh’ha) hadi mwisho wa siku za Tashriq (siku ya tarehe 13 Dhul-Hijja –Mfungo tatu. Allah Mtukufu ansema:

“Basi sali na uchinje kwa ajili ya Mola wako Mlezi (2: 108)” Ibada ya kuchinja ni Sunna iliyothabiti kwa mujibu wa kauli ya wanazuoni wengi.

Baadhi ya wanazuoni wamesema kuwa ni wajibu. Kawaida na asili Sunna hii inafaa kuchinjwa na mtu aliye hai kwa ajili yake mwenyewe na watu wa nyumba yake (wategemezi wake). Anaweza kushirikisha thawabu zake kwa yeyote anayetaka, awe hai au amekufa.

Ikiwa mtu aliyekufa aliacha wasia kuwa achinjiwe, au aliweka sehemu ya mali yake kuwa wakfu kwa ajili hiyo, basi ni lazima kutekeleza hilo.

Wanazuoni wamekubaliana kuwa kuchinja na kugawa nyama ni bora kuliko kutoa pesa yenye thamani ya mnyama kama sadaka.

Hii ni kwa sababu Mtume (rehema na amani ziwe juu yake) alichinja, na hakuwa akifanya ila lililo bora.

 Huu ni mtazamo wa Imamu Abu Hanifa, Shafi na Ahmad. Kondoo mmoja anatosha kwa mtu mmoja na familia yake, kama ilivyo katika Hadithi ya Abu Ayub:

 “Katika zama za Mtume wa Allah, mtu alikuwa akichinja kondoo kwa ajili yake na watu wa nyumba yake, nao walikula na kuwapa wengine.” (Tirmidhiy).

Wanyama wanaotakiwa kuchinja ni ngamia, ng’ombe, na kondoo. Wanazuoni wengine wamesema:

Kilicho bora zaidi ni ngamia, kisha ng’ombe, kisha kondoo. Ngamia mmoja au ng’ombe mmoja wanatosha kwa watu saba kushirikiana.

“Mtume wa Allah alituamuru tushirikiane katika kuchinja ngamia na ng’ombe, watu saba kwa mnyama mmoja.”

Umri sahihi wa wanyama wa Udh’hiya, kwa upnde wa kondoo awe amefikisha miezi sita, mbuzi mwaka mmoja, ng’ombe miaka miwili, ngamia miaka mitano.

Kadhalika mnyama huyo asiwe na kasoro, kama vile upofu, ulemavu, ugonjwa wa wazi au kukondeana.

 Kuna kasoro ndogo zisizoathari mnyama wa Udh’hiya kama vile, kukatwa sikio au kuvunjika pembe n.k.

Kadhalika iwapo ameshateuliwa kwa ajili ya Udh’hiya, hairuhusiwi kumuuza au kumzawadia mtu, isipokuwa kumbadilisha na kupata bora zaidi.

Sharti nyingine ni kuchinja katika wakati wake uliowekwa, ambao huanza baada ya Swala ya Id. Na wala si mara tu baada ya kuchomoza kwa jua.

Muda wake unaendelea hadi jua linapozama siku ya tarehe 13 ya Dhul-Hijja (Mfungotatu).

Sehemu ya kwanza ale yeye na familia yake, Sehemu ya pili awape zawadi jamaa na majirani, Sehemu ya tatu atoe kama sadaka kwa masikini.

Wanazuoni wamekubaliana kuwa si halali kuuza sehemu yoyote ya sadaka hiyo kama vile nyama, mafuta au ngozi.

 Hapasi kumpa mchinjaji chochote katika hayo kama malipo.

Hata hivyo, inajuzu kumpa kama zawadi tu. Ni bora mtu kuchinja kwa mkono wake mwenyewe:

 Kama hawezi, basi inapendeza awepo wakati wa kuchinjwa.

Muislamu anayekusudia kuchinja ni Sunna kwake kujiepusha katika siku Kumi za mwanzo za mwezi wa Dhul-Hijjah (mfungotatu) kukata nywele zake na kucha tu, au kuondoa sehemu yoyote ya ngozi yake kuanzia mwandamo wa mwezi Dhul-Hijjah (mfungtatu) hadi atakapochinja.

 Mtume wa Allah amesema:

“Mnapouona mwezi wa Dhul-Hijja na mmoja wenu anataka kutoa sadaka ya kuchinja, basi asikate nywele zake wala kucha zake mpaka achinje.”

 Katika riwaya nyingine amesema

 “Asiguse nywele zake wala ngozi yake chochote.” (Muslim). Hikma yake huyu anayechinja anashabihiana na hujaji kwa baadhi ya ibada za Hijja, kama vile kujikurubisha kwa Allah kwa kuchinja mnyama.

Hivyo, alipewa baadhi ya hukumu (sharia) zake. Lakini hakatazwi kutumia manukato, kufanya tendo la ndoa na mkewe, kuvaa mavazi yaliyoshonwa na mengineyo kama hayo. Katazo ni kwa kukata nywele, kucha na ngozi tu.

Related Posts