Dodoma. Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na taasisi ya African Program for Cyber Security Technology kutoka Marekani, kimeanzisha mafunzo ya kimataifa ya usalama wa mtandao kwa vijana.
Mafunzo haya ni muhimu kwa kukuza uelewa wa usalama wa mtandao, kuandaa wataalamu wa ndani na kutoa fursa za ajira na kujiajiri.
Pia, yanakuza ushirikiano wa kimataifa na kusaidia kujenga Taifa salama kiteknolojia, hatua ambayo ni muhimu katika kukabiliana na uhalifu wa kimtandao na kuimarisha mifumo ya kidijitali nchini, hasa kwenye taasisi nyeti, sekta ya umma na binafsi.

Makamu Mkuu wa Chuo kikuu Cha Dodoma (Udom) Profesa Lughano Kusiluka akimkagua mmoja wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na program ya masuala ya usalama mtandaoni.
Mafunzo hayo yanatolewa kwa vijana wa Kitanzania waliopo vyuoni pamoja na wale walio nje ya mfumo wa vyuo, lakini wenye ujuzi au mwelekeo katika masuala ya usalama wa mtandao na teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).
Jumla ya vijana 76 wamechaguliwa kuanza mafunzo hayo, huku lengo likiwa ni kufikia vijana 200, hususan wanawake, kutokana na hitaji kubwa la wataalamu wa usalama wa mtandao barani Afrika.
Inakadiriwa kuwa bara la Afrika linakabiliwa na upungufu wa zaidi ya wataalamu milioni 4, huku waliopo kwa sasa wasiozidi 10,000.
Akizungumza katika uzinduzi wa mafunzo hayo leo, Alhamisi Juni 5, 2025, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Lughano Kusiluka, amewataka washiriki kuyatumia mafunzo hayo kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa, siyo kinyume chake.
“Hatuanzishi programu kwa ajili ya vijana wanaokwenda kutumia ndivyo sivyo ni kwa ajili ya vijana ambao wanatakiwa wakaitumie vizuri, lakini ukitumia ndivyo sivyo sheria za makosa ya kimtandao ni kali kweli kweli,” amesema Profesa Kusiluka na kuongeza kuwa,
“Ila mimi kama mzazi na kama mwanataaluma nadhani ukipitia programu hii halafu ukafanya hiyo ndivyo sivyo mimi kwangu wewe ni mjinga tu na haukustahili kuingia kwenye hiyo programu.
Profesa Kusiluka, amesema mafunzo ya usalama wa mtandao yanayotolewa kwa kushirikiana na taasisi ya African Program for Cyber Security Technology kutoka Marekani ni uwekezaji wa kitaifa na si nafasi ya mtu binafsi.
Ametoa onyo kuwa vijana watakaoshindwa kuyatumia mafunzo hayo ipasavyo wataondolewa, kwani nafasi hiyo ni ya Watanzania wote.
Kwa mujibu wa Profesa Kusiluka, changamoto za usalama wa mtandao zimekuwa kubwa duniani kote, hivyo mafunzo haya yatasaidia vijana wa Tanzania kuajirika kimataifa.
Ameongeza kuwa programu hii imefungua mlango mkubwa kwa vijana kupata vyeti vya kimataifa vitakavyowatambulisha kama wataalamu wa usalama wa kimtandao, hivyo kuongeza nafasi yao ya kupata ajira ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake mmiliki mwenza wa kampuni ya African Program for Cyber Security Technology, Edward Sundberg amesema kila huduma sasa inaendeshwa kwa mtandao, hivyo kuna fursa kubwa ya ajira kwenye usalama wa kimtandao.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kusaidia kulinda taarifa za watu na taasisi dhidi ya udukuzi.

Baadhi ya wanafunzi waliopata nafasi ya kusoma program ya kimataifa ya masuala ya usalama mtandaoni
Rebbeca Kubanda, mmoja wa wanafunzi wa programu hiyo, amesema mafunzo yanawawezesha kukabiliana na changamoto kama udhalilishaji wa wanawake, watoto na vijana mtandaoni.
Ameongeza kuwa wanajifunza namna ya kulinda taarifa binafsi ili kusaidia wengine kuepuka madhara ya uvujaji wa picha na video mitandaoni.
Kwa upande wake Emmanuel Goliama, ambaye ni kiongozi wa mafundi simu mkoa wa Dodoma na mtaalamu wa Tehama, amesema usalama wa mtandao ni muhimu katika dunia ya sasa ambapo taarifa nyingi zinahifadhiwa huko.