Dodoma. Wakati Benki ya NMB ikiendelea kuvunja rekodi ya kupata faida kwa mwaka wa tatu mfululizo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, David Nchimbi, amepongeza ushirikiano wa wanahisa kwa kuridhia kwao maazimio ambayo yamekuwa chachu ya mafanikio ya benki hiyo.
Kutokana na ufanisi huo, wanahisa wa NMB sasa watanufaika na gawio la kihistoria baada ya benki hiyo kupata faida huku Sh214.43 bilioni zikipitishwa kwa ajili ya wanahisa wake.
Mkutano mkuu wa 25 wa wanahisa wa NMB uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Juni 5, 2025, umeinidhisha gawio hilo lililotokana na mafanikio makubwa kwa mwaka 2024, ikipata faida ya Sh643 bilioni baada ya kodi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna akizungumza na waandishi wa habari amesema mafanikio hayo yametokana na ubunifu wa huduma, utawala bora, pamoja na mazingira wezeshi ya kiuchumi yaliyowekwa na Serikali.
Amesema pia mali za benki zimeongezeka kwa asilimia 13 hadi Sh13.7 trilioni, mikopo kufikia Sh8.5 trilioni (ongezeko la asilimia 10), na amana za wateja zimefikia Sh9.6 trilioni (ongezeko la asilimia 13).
Zaipuna amefafanua kuwa, mwaka 2024, Benki ya NMB imeendelea kuimarisha ufanisi wake wa kifedha kwa kuvunja rekodi ya faida kwa mwaka wa tatu mfululizo na kufanikisha ongezeko la gawio kwa wanahisa kutoka Sh181 bilioni mwaka 2023 hadi Sh214.43 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 19. Gawio kwa kila hisa limepanda kwa asilimia 26 hadi kufikia Sh428.85.
Amesema kupitia mpango wa ‘Rural Banking,’ benki hiyo imepata wateja wapya milioni 1.5 na kufikisha jumla ya akaunti milioni 6.6.
Aidha, NMB imefanikiwa kuingia kwenye klabu ya kampuni zenye thamani ya zaidi ya Dola1 bilioni za Marekani baada ya thamani ya hisa zake kufikia Sh3 trilioni, kutokana na kufunga mwaka kwa bei ya Sh6,000 kwa hisa moja.

Mwenyekiti mpya wa Bodi ya NMB, David Nchimbi aliyekuwa akishiriki AGM ya kwanza tangu uteuzi wake wa Januari, 2025 uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, alimshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumpa heshima ya kuwa mwenyekiti wa bodi, huku akiwashukuru pia wanahisa kwa kumthibitisha.
Nchimbi amesema mafanikio yao kama taasisi na gawio kubwa kwa wanahisa wao, ni kielezo cha dhamira isiyoyumba katika kuongeza thamani ya wawekezaji wao na uimara wa kanuni na taratibu za kiutawala na kwamba, bodi yake imeridhishwa na mafanikio hayo na kuipongeza menejimenti na wafanyakazi.
“Tumeridhishwa sio tu na mafanikio yetu kwa mwaka jana, bali namna pia wanahisa walivyoridhia maazimio angalau kwa asilimia 99, ambayo ni dalili njema ya namna wanavyoridhishwa na utendaji, uendeshaji na ufanisi wa benki yao.
“Tunawashukuru kwa ushirikiano, mchango na msaada wao katika kuifanya NMB kuwa benki kubwa na bora. Bodi ya wakurugenzi tumeridhishwa na kiwango cha faida tulichopata mwaka jana kilichozaa gawio hili kubwa zaidi kuwahi kutolewa na NMB, kwenda kwa wanahisa,” amesema Nchimbi.
Aidha, Nchimbi amesema hatua ya NMB kuingia kwenye klabu ya kampuni zenye thamani ya zaidi ya Dola 1 bilioni za Marekani ni heshima sio tu taasisi hiyo, bali kwa Taifa na kwamba mafanikio hayo yataongeza mvuto wa hisa kwa hisa na kutanua wigo wa kukua kwa thamani ya hisa zao na kuongeza ukubwa wa gawio.