Serikali yagoma kubadilisha matumizi mashamba ya mpira

Unguja. Licha ya Serikali kukikiri kwamba hakuna tija inayopatikana kwa sasa kutokana na mashamba ya mpira, lakini imegoma kubadilisha matumizi ya mashamba hayo.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameishauri kubadilisha matumizi ya mashamba hayo kuwa ya miwa na karafuu kutokana na kutokuwa na tija katika uchumi wa Zanzibar kwa sasa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, kuna mashamba sita ya zao la mpira, Pemba matano na Unguja moja. Mashamba hayo ni sanaa, maziwani, makangale na kangani ambayo yapo Pemba na shamba la Kichwele lililopo Unguja.

Wakati wa mkutano wa Baraza la wawakilishi leo Juni 6, 2025 mwakilishi wa kuteuliwa na Rais, Juma Ali Khatib (Ada Tadea) amehoji kwanini serikali isibadilishe matumizi ya mashamba hayo kwa yale ambayo yapo Pemba yakatumika kwa ajili ya kilimo cha karafuu na kwa lile ambalo lipo Unguja likatumika kwa ajili ya miwa.

“Haya mashamba yanaonekana hayana tija kwasasa, yasibadilishwe matumizi, tunalia sana na ajira, kuna kiwanda cha miwa Mahonda hakina miwa ya kutosha, wakati kuna mashamba haya ambayo hayana tija, sasa ifike wakati yatumiwe kwa miwa na kule Pemba yawe ya karafuu jambo ambalo litaongeza ajira na kutatua changamoto ya sukari,” amesema Khatib.

Katika swali lake la msingi, Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir alitaka kufahamu kwa sasa zao hilo linachangia kiwango gani katika pato la taifa na sababu za mashamba hayo kutosimamiwa na kuendelezwa.

Naye mwakilishi wa Tumbe, Saleh Said Saleh amesema lipo wimbi kubwa la ukataji wa miti ya zao hilo kiasi kwamba kama serikali imebinafsisha na kutaka kujua sababu ya kukatwa waziwazi hata bila ya watu kuchukuliwa hatua.

Hata hivyo, akijibu hoja za wawakilishi hao, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis licha ya kukiri zao hilo kutokuwa na tija yoyote kwa serikali, bado hawajafikiria kubadilisha matumizi yake.

Amesema wapo baadhi ya wawekezaji ambao wanaonyesha nia ya kutaka kuwekeza na kuyaendeleza mashamba hayo.

“Kwasasa zao la mpira halina mchango wa moja kwa moja kwa pato la taifa kwa vile mashamba ya zao hili yamekuwa hayasimamiwi ipasavyo huku Serikali ikitafuta mwekezaji ya kuyafufua kwa vile yamekuwa na umri mrefu unaokwaza uzalishaji wake kiuchumi,” amesema.

Licha ya kukiri mashamba hayo ambayo yapo chini ya serikali kuwa na faida nyingi za kiuchumi na kuwa alama ya Zanzibar, lakini amesema yamekuwa na uvamizi mkubwa na kutoendelezwa, hata hivyo hakuweka wazi sababu ya kutoendelezwa.

Waziri Shamata amesema serikali kwasasa haifikirii kuyabadilisha matumizi yake bali itawatafuta wawekezaji kuyaendeleza na kwamba wale wanaoyavamia hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, amesema kwasasa mashamba hayo yamehamishwa kutoka Wizara hiyo na kupelekwa Wizara ya Kazi Uchumi na Uwekezaji chini ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa) lakini wizara ya kilimo inaendelea kushirikiana nao kwa sababu zao hilo ni miti