Dk Nyambura Moremi aaga Maabara ya Taifa

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Umma (NPHL), Dk Nyambura Moremi ametangaza rasmi kung’atuka kutoka nafasi yake akiikamilisha enzi iliyobadili kabisa taswira ya uchunguzi wa magonjwa na sayansi ya maabara nchini.

Anaondoka wiki moja baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO), kuidhinisha maabara hiyo kwa ajili ya kupima usugu wa dawa kwa wagonjwa wa Ukimwi, surua na rubella, hatua iliyoongeza hadhi yake kimataifa.

Dk Moremi, mtaalamu wa microbiolojia ya kitabibu na magonjwa ya kuambukiza, ni miongoni mwa wanasayansi mahiri nchini Tanzania. Alitangaza kujiuzulu nafasi yake kupitia mitandao ya kijamii siku ya Alhamisi.

“Ninashukuru sana kwa zaidi ya miaka minne ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilinipa dhamana ya kuongoza NPHL,” aliandika.

“Kwa pamoja, kama timu, tulifikia mafanikio makubwa ambayo yaliinua hadhi ya maabara kitaifa, kikanda na kimataifa,” aliongeza.

Kipindi chake cha pili cha uongozi NPHL kilifuatia kuondolewa ghafla na kwa utata ulioibuka Mei 2020.

Wakati janga la Uviko-19, alisimamishwa kazi na aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kutokana na mvutano kuhusu uhalali wa taratibu za maabara hiyo katika kupima virusi vya hivyo.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Rais wa wakati huo, John Magufuli, kudai kuwa sampuli kutoka kwa vyanzo visivyo vya kibinadamu ikiwemo mbuzi, papai na mafuta ya injini zilionyesha matokeo chanya kwa virusi hivyo, jambo lililoashiria ama uzembe mkubwa au hujuma katika maabara hiyo ya Taifa.

Madai hayo yalisababisha kuundwa kwa kamati ya uchunguzi ya watu 10, ingawa matokeo yake hayakuwahi kuchapishwa na Tanzania ilisitisha utoaji wa taarifa za Uviko-19.

Licha ya mazingira hayo, kurejeshwa kazini tena kwa Dk Moremi na uteuzi wake upya kulionekana na wengi kama uthibitisho wa kuondolewa lawama.

Wanaojua undani wanasema ukosefu wa ushahidi wa uchunguzi uliowekwa hadharani, pamoja na kurejeshwa kwake, uliashiria kurejesha imani juu ya weledi wake na uadilifu wa kisayansi.

Katika kipindi chake cha pili, Dk Moremi aliongoza mageuzi makubwa katika NPHL.

Chini ya uongozi wake, maabara hiyo ilipata vyeti vya ubora na umahiri katika upimaji wa kitabibu kupitia ISO 15189:2022, na pia cheti cha ISO 17043:2010 kwa ajili ya upimaji wa uwezo wa kitaalamu.

Pia, iliteuliwa kuwa Kituo cha Ubora cha Kanda ya Afrika Mashariki kwa usalama na ulinzi wa kibiolojia, ambapo wataalamu zaidi ya 70 kutoka nchi tisa walipata mafunzo.

Uongozi wake pia uliifanya NPHL kuwa kituo cha Taifa kwa ajili ya ufuatiliaji wa usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (AMR) katika afya ya binadamu, na ikaingia katika mchakato wa kuwa maabara rejea ya Taifa kwa ajili ya kupima ugonjwa wa polio.

Zaidi ya hayo, maabara hiyo ilipanua uwezo wake kiteknolojia kwa kuanzisha mbinu za kisasa za kugundua saratani ya mlango wa kizazi na kuweka miundombinu ya uchambuzi wa jeni (genome sequencing) na bioinformatics ndani ya nchi.

Hii iliiwezesha Tanzania kuchunguza virusi na bakteria wanaosababisha milipuko bila kuhitaji kutuma sampuli nje ya nchi, ikitajwa kuwa ni hatua kubwa kuelekea uhuru wa kisayansi wa kitaifa.

Dk Moremi sasa anakwenda kushika wadhifa mpya wa Ofisa wa Kiufundi wa AMR katika mradi wa GIZ wa Umoja wa Afrika/Africa CDC.

Katika nafasi hiyo, atazisaidia nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kubuni, kupitia na kutekeleza mipango yao ya kitaifa ya kukabiliana na usugu wa dawa, kwa kuzingatia mwongozo wa Umoja wa Afrika.

“Hongera kwa mwanzo mpya,” aliandika katika ujumbe wake wa kuaga, akionyesha hamasa yake kwa hatua inayofuata katika taaluma yake.

Kipindi cha Dk Moremi katika NPHL hakikusaidia tu kurejesha hadhi ya maabara hiyo, bali pia kuliinua nafasi ya Tanzania katika afya ya umma kimataifa na kikanda.

Urithi wa Dk Moremi unatajwa kuwa alama pia dira ya matumaini katika kuhakikisha sayansi inapewa nafasi.

Related Posts