Muhas yaja na mradi usambazaji wa bidhaa za afya

Dodoma. Jumla ya Sh2.5 bilioni kutumika kwa ajili ya kujenga uwezo katika mnyororo wa usambazaji wa bidhaa za afya utakaofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).

Lengo la mradi huo ni kutatua changamoto zinazotokana na majanga duniani zinazofanana ugonjwa wa Uviko-19 ambapo baadhi ya nchi zilifungia watu (lockdown).

Mradi huo wa miaka mitatu, utahusisha, pia, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Wizara ya Afya na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, unaojulikana kwa jina la Senselet, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Muhas, Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema mradi huo utafanyika nchini kwa muda wa miaka mitatu.

Amesema utekelezaji wa mradi huo unatokana na urafiki kati ya chuo hicho na Chuo Kikuu cha Addis Ababa nchini Ethiopia baada ya kupata wafadhili kutoka Ulaya.

“Tutatoa mafunzo kwa wataalamu wa mnyororo wa thamani lakini vilevile tutaanzisha mtaala wa masomo ya uzamili (masters). Tupate wataalamu wa waliosomea masters ya supply chain (mnyororo wa usambazaji) na jinsi ya kusimamia, kusambaza bidhaa za afya,” amesema.

Profesa Kamuhabwa amesema katika mradi huo kutakuwa, pia, na mafunzo ya muda mfupi yatakayotengenezwa kwa ajili ya kujengea uwezo watu wa mbalimbali wakiwemo wafanyakazi walioko makazini.

Amesema mradi huo pia utahusika na kufanya tafiti mbalimbali zinazolenga katika kuleta majibu ya changamoto ambazo zilitokea huko nyuma kama vile Uviko-19.

“Sasa tumepata mafunzo (Uviko-19). Tunataka sasa tuweke mikakati. Tufundishe watu, tuweke mitaala kuhakikisha kwamba tunavyopata janga kama hilo, tayari tumejiandaa jinsi ya kukabiliana nayo,” amesema.

Naye Mratibu wa mradi huo, Profesa Eliangiringa Kaale amesema kupitia program hiyo kama chuo wataongeza idadi ya wanafunzi.

Amesema ili kuendana na idadi kubwa ya wanafunzi ambayo imeongezeka itabidi uwezo wao kama chuo kwa maana walimu wa kufundisha waongezeke.

Profesa Kaale amesema kutakuwa ufadhili wa masomo wa shahada ya udaktari (Phd) kwa ajili ya walimu kwenye nyanja ya mnyororo wa bidhaa za afya.

Pia, amesema mradi huo unasehemu ya kujenga uwezo kwa taasisi zinazotoa huduma na kuimarisha miundombinu ya mnyororo wa usambazaji wa bidhaa za afya ikiwemo majokofu yanayotumia umeme wa jua kwa ajili ya kuhifadhia bidhaa za afya.

Meneja Mkuu wa Mpango na Usafirishaji wa Taasisi ya Kuhne, Wolf Noske amesema ushirikiano huo unalenga katika kuongeza uwezo katika usimamizi wa vifaa na mnyororo wa ugavi katika vyuo vikuu vya ndani hapa Tanzania.

“Ninayo furaha kusema kwamba sasa tumefanikiwa kusonga mbele na tunatekeleza miradi kadhaa nchini katika mikoa mbalimbali,” amesema.

Mkurugenzi wa mradi, Jane Rasmussen amesema lengo kuu ni kuhakikisha kuwa nchi za Afrika zinajifunza kutoka kwa kila mmoja kuhusu jinsi ya kushughulikia changamato ya mnyororo wa ugavi katika utaratibu unaofaa.

“Kwa sababu hiyo, tulitaka kuchangia kwa kutoa ujuzi wa usimamizi wa mnyororo wa ugavi lakini pia kuhakikisha kuwa mnajifunza kutoka kwa kila mmoja na kupata suluhisho bora zaidi,”amesema.

Related Posts