Dar es Salaam. Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayeshughulikia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Sauda Msemo amesema kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia za fedha, Serikali inahakikisha matumizi yake yanakuza uchumi na kuiweka nchi katika hali salama.
Amesema tayari Serikali imezindua mfumo wa kufanyia majaribio teknolojia za kifedha kabla ya kuingizwa sokoni, ambao pia utashughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kifedha, mfumo huo umepewa jina la “Sema na Benki Kuu”.
Mfumo huo unalenga kulinda haki za wateja, kuongeza uwazi na kuimarisha usimamizi katika sekta ya fedha.
Sauda amesema hayo Juni 6, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla iliyoandaliwa na Jukwaa la Impact Business Breakfast (IBB), lililowakutanisha wadau mbalimbali kujadili mageuzi ya ujumuishaji wa kifedha na nguvu ya akili mnemba (artificial intelligence).
“Tunachopaswa kuzingatia wakati tunakuza teknolojia, hasa tunapoleta sokoni bidhaa mbalimbali za kifedha, ni kuhakikisha zinaiacha nchi salama na zinaendelea kukuza uchumi wetu. Hatuwezi kuwa salama tukisema tunakuza teknolojia bila kuzingatia vigezo muhimu vya uendelevu wa teknolojia hiyo,” amesema.
Aidha, Sauda amesema ni muhimu sekta binafsi kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha bunifu zinazoingizwa sokoni zinazingatia maslahi ya uchumi wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vihatarishi na Utekelezaji kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Anethe Magogo amesema hafla hiyo inasaidia kuanzisha njia ya ujumuishaji wa akili mnemba katika masuala ya kifedha.
“Akili mnemba inamhusu kila mtu. Tumeona vijana wakitoa mawazo yao kuhusu namna ya kuifanya sekta ya fedha iwe endelevu kupitia matumizi ya akili mnemba,” amesema.
Naye, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Kampuni ya Impact Advisory, Angel Mbogoro amesema jukwaa hilo alilianzisha mahususi baada ya kubaini ombwe katika ushirikiano wa kitaaluma hapa nchini.
“Tuna ombwe kubwa la kushirikishana maarifa, watu hawasemi walivyofanikiwa, hakuna ushirikiano. Mtu anapofanikiwa, yule aliye chini yake haendelezwi.
Kwa mfano, meneja akifariki, kampuni huajiri mtu kutoka nje badala ya kuinua aliyekuwa chini yake, kwa sababu hakuwahi kuandaliwa,” amesema.
Kwa upande mwingine, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yass, Angelica Pesha amesema ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika masuala ya teknolojia hutoa suluhisho madhubuti, huongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na hujenga uchumi imara unaowanufaisha wananchi wote.
“Teknolojia za kifedha zinapaswa kuzungumza lugha ya watu,ziwe rahisi kufikiwa, jumuishi, na ziendane na mahitaji halisi ya jamii zisizohudumiwa ipasavyo,” amesema.