Vijiji vitatu vyajikomboa kero ya maji

Simiyu. Wananchi wa Kata ya Mwamashimba wilayani Maswa mkoani Simiyu, wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji baada ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (Mauwasa) kuwajengea tangi lenye ujazo wa lita 200,000 na vituo 16 vya kuchotea maji.

Wananchi hao walikuwa wakitembea umbali wa kilomita 10 kutafuta maji, huku wakichangia huduma hiyo na wanyamapori kwenye visima vidogo vilivyoko kwenye mito inayozunguka vijiji vya kata hiyo.

Mhandisi Nandi Mathias aliyepo mbele akitoa maelezo mara ya kukamilika kwa kituo cha kuchotea maji katika kijiji cha Likungulayasubi wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga

Wakizungumza na Mwananchi leo Juni 7, 2025 baada ya kukamilika kwa mradi huo, Mkazi wa Kijiji cha Buyubi, Yustina Deus amesema awali walikuwa wanatoka alfajiri kwenda kutafuta maji umbali wa kilomita 10 hadi kufika kwenye visima ambavyo maji yake si salama.

“Tuliamka alfajiri saa 10:00 kufuata maji kwenye visima tulivyochimba kwenye mito. Maji hayo hayakuwa salama  kiafya, lakini sasa tunapata maji karibu kabisa na nyumbani,” amesema.

Veronika Moga, mkazi wa Kijiji cha Buyubi, amesema kukamilika kwa mradi huo kumeondoa hatari ya kutumia maji kutoka kwenye visima vilivyotumiwa pia na wanyamapori wakiwamo fisi.

Buyaga Chai, mkazi wa Kijiji cha Likungulyasubi amesema ndoa nyingi zilikuwa na ugomvi wa mara kwa mara kwani wanawake walikuwa wakitoka alfajiri kuchota maji maji na wakichelewa kurudi inatafsiriwa wamekwenda kufanya mambo ya kihuni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Mhandisi Nandi Mathias akimtwisha ndoo mmoja wa wakazi wa kijiji cha Buyubi ikiwa ni sehemu ya kuzindua vituo vya kuchotea maji katika Kata ya Mwamashimba wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga

“Sasa wake zetu hawalazimiki tena kuamka alfajiri kusaka maji porini, tumeondokana na hali hiyo na kwa sasa ndoa zetu zilizo nyingi zitaimarika kutokana na kusogezewa huduma ya maji kwenye kijiji chetu,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Nandi Mathias amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi 18 iliyotekelezwa na mamlaka hiyo na unawahudumia wananchi katika vijiji vya Buyubi, Dodoma na Likungulyasubi.

“Mradi huu umeweka vituo 16 vya kuchotea maji na mabirika mawili kwa ajili ya mifugo kunywea maji, huku chanzo chake kikuu kikiwa Bwawa la New Sola lililopo Kijiji cha Zanzui wilayani Maswa,” amesema.

Amesema wamepokea kutoka kwa Serikali zaidi ya Sh29 bilioni ndani ya kipindi cha miaka minne kwa ajili ya miradi ya maji.

Amesema mbali na miradi ya ndani ya wilaya, mamlaka hiyo inasimamia utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria, unaoanzia katika Mji wa Malampaka wilayani humo hadi Mji wa Malya wilayani Kwimba, mkoani Mwanza.

Moja ya kituo cha kuchotea maji katika kijiji cha Buyubi kilichojengwa na  Mauwasa. Picha na Samwel Mwanga

Nandi amesema lengo kuu la miradi hiyo ni kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi, hususan katika vijiji ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikitegemea maji kutoka vyanzo visivyo salama kama vile mito na mabwawa ya asili.

Miradi hiyo amesema ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha huduma za msingi zinawafikia wananchi vijijini, hasa maeneo yaliyokuwa yakikumbwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu.

Related Posts