Wafanyabiashara walia kufungwa mtandao wa X

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitangaza kuufungia mtandao wa X (twitter zamani) hapa nchini wafanyabiashara na wahamasishaji (infulencers) wameanza kuonja joto la jiwe.

Hiyo ni baada ya biashara zilizokuwa zikifanyika katika mtandao huo kuanza kudorora huku baadhi ya kampuni zikisitisha mikataba waliyokuwa wameingia na watumiaji mbalimbali wa mtandao huo ikiwemo zile zilizohusu kampeni mbalimbali.

Hivi karibuni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa kuweka wazi kuwa iwapo mwananchi anashindwa kupata mtandao fulani ajue kuwa Serikali imefanya namna kumlinda Mtanzania.

“Kama umeona kuna baadhi ya mtandao siyo lazima uwe X wowote hata YouTube kuna kitu unatafuta hukipati ujue ni kazi inayofanywa na Serikali kuhakikisha inamlinda mlaji na kuhakikisha watu wote wanaoendesha huduma kwenye anga la Taifa letu wanafuata sheria,” amesema.

Silaa katika mahojiano yake na Kituo cha runinga cha Wasafi, alisema Kifungu cha 16 cha Kanuni ya Maudhui ya Mtandao ya mwaka 2000, kinaeleza aina ya maudhui yanayopaswa kuchapishwa katika mtandao husika.

Amesema kanuni hizo zinalenga kumlinda mtumiaji Mtanzania na ikifanywa kinyume Serikali inafanya namna kuhakikisha mtumiaji analindwa.

“Baada ya X kununuliwa na baadaye Mei 2024 mtandao huo ulibadili sera yao ya faragha inayokwenda kinyume na kanuni hiyo ya Tanzania. Ukienda X unaweza kukuta picha za ngono, mambo ambayo yanakwenda kinyume na sheria, tamaduni, mila na desturi zetu,” amesema.

Ukata kwa wafanyabiashara

Licha ya kutokuwa tayari kutaja majina yao lakini walilaani kitendo hicho huku wakieleza kuwa kinawarudisha nyuma kiuchumi kwani mtandao huo ulikuwa sehemu ya mapato wanayoyategemea kila mwezi.

Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wafanyabiashara katika mtandao huo wanaolia na ugumu wa biashara kutokana na kupungua kwa idadi ya wateja wanaoweza kuifikia X sasa kupungua.

“Unajua wanaopata X sasa hivi ni wale wanaotumia VPN, wengi hawajui kuhusu hili, hivyo ule mwingiliano umepungia kwa kiasi kikubwa, hii inafanya watu wengi kushindwa kupata taarifa pale kunapokuwa na bidhaa mpya,” amesema.

Jambo hilo hufanya hata mzigo ambao amefungua kutumia muda mrefu tofauti na awali wakati mtandao huo haujawekewa zuio lolote.

Mbali na kuwa mfanyabiashara pia hutumiwa na kampuni mbalimbali kama mhamasishaji (influencer) lakini sasa baadhi ya kampuni zimesitisha mikataba hadi pale watakapoambiwa baadaye na zilizokuwa mbioni nazo zimeomba kusitisha.

“Kwa sababu hawafikii ile idadi ya watu waliokuwa wamelenga kuifikia, hizi zote ni fedha zimepotea, mfano hizi kampuni nilizokuwa nazo zilikuwa zikilipa hadi Sh1 milioni kwa mwezi unaweza kuona ni kiasi gani tumepoteza fedha,” amesema dada huyo.

Mfanyabiashara mwingine amesema kiwango cha wateja kimepungua kwa sababu waliobakia katika mtandao huo ni walewale hata ikiwa wao ndiyo wateja basi hawatanunua kila siku.

“Unajua watu wanapokuwa wengi ndiyo wigo wa biashara unakuwa mpana zaidi, watu wakiwa wachache hata mzunguko unakuwa ni mdogo, badala ya kufunga mtandao kulikuwa na namna ya kuzuia maudhui wanayoyalalamikia kwani si mamlaka zipo,” alihoji.

Amesema kukimbilia kufunga mtandao wote hakuwezi kuwa njia ya kutatua tatizo na badala yake inafanya vijana wengi ambao walikuwa na uwezo wa kupata fedha kupitia mtandao huo kukaa bila chanzo chochote cha kipato.

“Unajua huku kuna watu wanaingiza fedha nyingi sana kwa kufanya kazi na kampuni mbalimbali kama influencer. Mimi naweza kuwa siingizi hela nyingi lakini kuna wanaoingiza hela nyingi lakini leo kampuni zimesitisha mikataba, kipato chao kinapungua,” amesema.

Mhamasishaji mwingine amesema jambo hilo limemfanya kupoteza mkataba ambao ungeweza kumuingia Sh9 milioni fedha ambayo anaeleza kuwa ingesaidia kumudu mahitaji yake na kumfanya apige hatua kimaisha.

“Unaweza kudhani ni utani lakini ndiyo uhalisia, tukiwa katika hatua za mwisho kukamilisha hili dili nikaona X imefungwa, kaa kwenye viatu vyangu, nusu ya pesa nilitakiwa kulipwa wakati naanza kazi halafu asilimia inayobaki ningelipwa kidogo hadi muda utakapokwisha, nimeshapiga na hesabu zangu matokeo yake nimeishia kuiona fedha hiyo kwenye makaratasi,” amesema.

Ameitaka Serikali kuongeza nguvu katika kudhibiti maudhui ambayo haitaki yafike kwa jamii badala ya kufunga mtandao wote na kuathiri vijana wengine ambao wanajitafutia kipato huko.

Wakati wafanyabiashara wakilia njaa, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani uamuzi wa Serikali wa kuzuia upatikanaji wa mtandao wa kijamii wa X.

LHRC imeitaka Serikali Kurejesha mtandao wa X sambamba na upatikanaji wa mtandao wa Clubhouse, Telegram na majukwaa mengine ya kidijitali yaliyofungiwa.

“Pia, Serikali ihakikishe kunakuwa na uwazi katika mchakato wa udhibiti wa kidijitali na kuwashirikisha wadau katika kuandaa sera za usimamizi wa maudhui zinazoenzi haki za binadamu,” imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa kwa umma.

Pia LHRC imetoa wito kwa wananchi, asasi za kiraia, na jamii ya kimataifa kusimama pamoja kwa nguvu moja kutetea na kulinda uhuru wa kidijitali nchini Tanzania.

Related Posts