Wanasiasa wahimiza utii wa sheria, haki na wajibu wakiadhimisha Eid

Dar/Mikoani. Katika kuadhimisha sikukuu ya Eid El-Adh’haa viongozi wa kisiasa wamehimiza kukuza umoja wa kitaifa, kuelimisha kuhusu majukumu ya kidini kwa mujibu wa sheria, wakiweka mkazo juu ya utawala wa sheria, haki, mshikamano na maendeleo ya jamii.

Kwa nyakati tofauti viongozi hao wamesema hayo baada ya swala ya Eid El-Adh’haa iliyofanyika leo Juni 7, 2025 maeneo kadhaa nchini.

Eid El- Adh’ haa ni sikukuu inayoadhimishwa baada ya Waislamu kukamilisha ibada ya Hijja ambayo ni nguzo ya mwisho katika nguzo tano za Uislamu na hufanyika katika miji ya Makka na Madina nchini Saudi Arabia.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wanaofanya shughuli mbalimbali ziwe za kikundi, binafsi au za umma kuzingatia sheria, ikiwemo katika uitekelezaji wa haki ya kuabudu.

“Tunapokuja kuabudu, lazima tuzingatie sheria ya uhuru wa kuabudu. Katiba ya Tanzania ibara 19(3) imeweka bayana ufafanuzi wa kuabudu ilimradi hakuna uvunjifu wa amani na sheria za nchi.

“Kuabudu si watu tu kukutana na kufanya wanavyotaka, bali iko sheria iliyoruhusu hata msikiti kuwa hapa au kanisa kuwa pale, ndiyo iliyoruhusu kiongozi wa dini awepo ili kuzungumzia masuala ya dini,” amesema.

Majaliwa akihutubia Baraza la Eid El- Adh’ haa lililofanyika katika Msikiti wa Mohammed VI uliopo makao ya makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Kinondoni, Dar es Salaam, amesema masuala yote ya dini yanalindwa na sheria hata uwepo wa masheikh na maimamu, ni kwa sababu sheria imewaruhusu kufanya hivyo.

“Tunapopata nafasi ya kuja hapa kama leo hii, tunatarajia viongozi mtatumia muda mwingi uliotengwa kwa ajili ya ibada kuzungumzia dini na si vinginevyo, kwa sababu uwepo wa jengo hilo na ujio waumini ni kuja kusikia neno la Mungu na kuendelezwa kiimani itakayoleta amani na utulivu.

“Tunafanya haya kwa sababu tunazo sheria, unapoivunja sheria na kufanya vinginevyo sheria inachukua mkondo wake. Lazima tukumbushane na kufanya mambo kwa sababu kuna uhuru, hata hivyo uhuru una mipaka. Haki lazima iende na kutimiza wajibu,” amesema.

Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati ambao Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa Juni 2, 2025 alitangaza kulifuta Kanisa la Ufufuo na Uzima lenye makao yake makuu Ubungo, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa barua, iliyotolewa Jumatatu Juni 2, 2025 Kihampa alieleza kanisa hilo limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337: “Kwa kutoa mahubiri yenye muelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.”

Nafasi ya viongozi wa dini

Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema Serikali inawaamini viongozi wa dini wa madhehebu yote kwa sababu wamekuwa chachu ya kuimarisha amani na mshikamano katika Taifa kupitia mahubiri wanayoyatoa.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha uhusiano mzuri kati yake na viongozi wa dini zote, wa madhehebu mbalimbali nchini, ili kila mmoja ashiriki kuhakikisha Taifa linakuwa na amani ya kutosha.

“Ninaamini viongozi wa dini mtaendeleza jukumu hilo la kuwasihi Watanzania kuwaona kila mmoja ana mchango wa kulifanya Taifa la Tanzania kuwa tulivu na kuimarisha mshikamano miongoni mwetu,” amesema.

Amesema dini ina misingi yake na imejengwa kwa namna ya kuwafanya waumini wake kuwa na staha, ustaharabu, uvumilivu, hivyo viongozi wa dini pia wana nafasi kubwa ya kuhamasisha waumini kushiriki shughuli za maendeleo.

“Dini imeifanya Tanzania kuendelea kuwa nchi ya amani wakati wote na viongozi wa dini mnayo nafasi ya kukemea mambo yote yanayosababisha mmomonyoko wa maadili ndani ya Taifa hili. Imani hii imejengwa kwa miaka mingi na Taifa tuna masilahi nayo,” amesema.

Majaliwa amesema waumini wanapojengwa kiimani basi iwe ya kujenga Taifa si kuwajengea watu imani inayokwenda kulibomoa Taifa ambayo itasababisha jamii kuharibika.

Amesisitiza kuwa dini haina nafasi ya kubomoa jamii bali ipo kwa ajili ya kujenga jamii inayoizunguka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera akizungumza baada ya swala jijini Mbeya amewataka wananchi kudumisha amani na mshikamano, akionya kuhusu mgawanyiko kikabila na kidini, akieleza kuwa muasisi wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere alishaweka mifumo bora.

Amesema katika kusherekea sikukuu zaidi ya ng’ombe 35 watachinjwa na kugawanywa kwa wananchi, akiahidi kuchangia Sh5 milioni kwa ajili ya shule ya sekondari ya Kiislamu inayotarajiwa kujengwa.

“Tusiombeane mabaya bali tupendane, tushikamane na kushirikiana, tusigawanyike kikabila wala kidini na leo ng’ombe zaidi ya 35 watachinjwa na kugawanywa kwa wananchi,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ametoa wito kwa watumishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi( INEC), wakatende haki katika kusimamia uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

Amesema hayo baada ya kushiriki swala ya Eid katika Masjid Noor, uliopo Bariadi mkoani Simiyu, alikoongoza harambee kuchangisha fedha za ujenzi wa msikiti huo.

Mwalimu amesema wanaposherekea sikukuu hiyo viongozi wasihubiri amani bila haki, hasa kwa kuwataka wasimamizi wa uchaguzi wakatende haki.

“Tunapohimiza amani tuhubiri na haki vyote viende sambamba na hata watendaji watakaoenda kusimamia uchaguzi mkuu wakatende haki ili tukimaliza wote tuwe wamoja,” amesema.

Amewataka waumini wa Kiislamu na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kushiriki haki hiyo ya msingi ya kuchagua, kuchaguliwa na kupiga kura kama Katiba ya Tanzania inayoeleza.

“Mkashiriki uchaguzi. Msirudi nyuma, nendeni mkagombee udiwani, ubunge na urais, tukapeane mawazo kuhakikisha tunashinda na kupata viongozi watakaokuja kuondoa kiu ya matatizo yanayowakabili Watanzania,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia kurasa za mitandao yake ya kijamii ameandika:

“Ninawatakia Waislamu na Watanzania wote kheri ya sikukuu ya Eid al-Adha. Tafakari na mafundisho ya sikukuu hii yanatuasa kuishi katika utii kwa Mola wetu, katika ukweli na kumtegemea Mwenyezi Mungu, huku tukiwajali wenye uhitaji na wote ambao Mola amewaweka katika njia ya kuhudumiwa nasi kwa namna mbalimbali.

“Sikukuu hii iendelee kutudumisha sote na Taifa letu katika amani, upendo na umoja. Mwenyezi Mungu Mtukufu aendelee kuzipokea na kuzikubali dua zetu katika yote mema kwa nchi yetu.”

Imeandikwa na Bakari Kiango (Dar), Saddam Sadick (Mbeya) na Tuzo Mapunda (Bariadi).

Related Posts