Hawa ndio maadui wa afya ya ngozi yako

Dar es Salaam. Hakuna mtu asiyependa kuwa na ngozi yenye afya. Kutokana na hilo watu wengi  wamekuwa wakitumia vitu mbalimbali kama vipodozi asili au vile vya viwandani, ambavyo wanadai vinasaidia kuwa na ngozi nzuri.

Yote hayo wanayafanya ili kuwasaidia  kupata mvuto  katika ngozi zao.Wengine huenda mbali hata kufikia uamuzi  wa kufanya upasuaji rekebishi  ili tu waweze kuwa na mwonekano wa kuvutia.

Hata hivyo,  wataalam mbalimbali wa ngozi wanabainisha mambo ya kuyaepuka ili kuendelea kuwa na ngozi yenye mvuto.

 Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuepuka mionzi ya jua, usafi, lishe duni, kutokunywa maji ya kutosha pamoja na msongo wa mawazo. 

Kwa mujibu wa tovuti ya afya ya WebMb, mionzi ya jua hasa wakati wa mchana (kati ya saa nne  asubuhi hadi 10 jioni) ni hatari kwa afya ya ngozi. 

 Mionzi hiyo inaelezwa kuwa inaweza kusababisha kuungua kwa ngozi, kuzeeka mapema, na kuongeza hatari ya kupata saratani ya ngozi. 

“Ni muhimu kutumia krimu za kuzuia jua (sunscreen) kila siku, hata wakati wa mawingu”inaeleza tovuti hiyo katika chapisho lake la namna mwanga wa jua unavyoweza kuathiri ngozi.

 Kutumia vipodozi bila kupata ushauri wa wataalmu

Pia imegusia tabia ya kutumia vipodozi hasa vyenye kemikali bila ushauri wa mtaalamu wa ngozi.

Inaeleza kuwa tabia hiyo inamuweka mtu katika hatari ya kuharibu ngozi yake na hata kupata saratani,  kwani anaweza kutumia vipodozi hivyo isivyo sahihi.

 Pia baadhi ya vipodozi hivyo vinaweza kuwa na kemikali hatarishi au havijathibitishwa na mamlaka zinazopima ubora wa bidhaa.

 Uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupindukia

 Kwa mujibu wa tovuti ya Nation Institute of health, uvutaji wa sigara kupita kiasi huharibu mzunguko wa damu kwenye ngozi sambamba na  kolajeni, protini inayohifadhi uimara wa ngozi. 

 Pia unywaji wa pombe kupindukia kwa upande mwingine huondoa unyevu na virutubisho muhimu katika ngozi, hivyo kuifanya ichoke na kuzeeka mapema.

Akizungumza na Mwananchi,  mtaalamu wa masuala ya chakula na lishe na Meneja mradi wa Afya ya Mama na Mtoto kutoka Shirika la Word Vision, Dk Daud Gambo anaeleza kuwa ukosefu wa virutubisho muhimu kama vitamini A, C, E, na zinki,  unaweza kudhoofisha ngozi, kuifanya isikabiliane vizuri na maambukizi au uharibifu. 

Anasisitiza kuwa ulaji wa lishe bora huifanya ngozi kuwa na afya, kung’aa na kuwa na unyevu wa kutosha.

Anasema ulaji wa matunda hasa yale yenye wingi wa vitamin C kama vile machungwa, limao, pensheni, nanasi, parachichi na mengineyo yenye asili hiyo,  kwani pamoja na kazi yake ya kuusaidia mwili kupambana dhidi ya mashambulizi na sumu za vyakula,  pia  husaidia katika kuondoa uvimbe na mikunjo ya ngozi hivyo kuilinda ngozi yako isizeeke mapema.

 Kwa mujibu wa wa tovuti ya ‘Times of India’ vyakula vingine ambavyo vinashauriwa kwa ustawi wa ngozi yako ni pamoja na mayai, maziwa, samaki, manjano na  zabibu.

 Daktari wa ngozi kutoka hospitali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Tumpale Luhanga,  anasema kutooga mara kwa mara, kutumia taulo chafu, au kushindwa kuondoa vipodozi kabla ya kulala,  husababisha kuziba kwa vinyweleo, kuchafuka kwa ngozi, na kuongezeka kwa bakteria wanaoweza kusababisha upele au chunusi.

 Anasema mtu anapofanya usafi wa ngozi ya uso pamoja na mwili mzima inasaidia kuondoa uchafu uliopo juu ya ngozi.

 “Ni muhimu kujitahidi kuoga mwili mzima angalau mara mbili kwa siku yaani asubuhi na jioni kwa kutumia maji ya uvuguvugu na sabuni”

 Mambo mengine aliyosisitiza ambayo yanasaidia kuwa na ngozi yenye afya ni pamoja na kunywa maji ya kutosha, kulala kwa muda usiopungua saa nane kwa siku na  kuepuka vyakula vyenye sukari nyingi.

Related Posts