Kuna kisa cha mzee wa Kifilipino aliyeolewa akidhani ameoa. Ni jamaa wa miaka kama 60 na ushei. Huyu bwana, baada ya kutua Canada, alinyakwa na mama mmoja mtu mzima aliyekwishatalikiwa.
Ni mama tajiri aliyestaafu biashara ya uuzaji wa vinywaji. Kwa vile ni jirani yetu, na tunaishi kwenye mji mdogo ambapo kila mmoja anamjua mkazi wake, tumetokea kumjua si kwa sababu tuna uhusiano naye. La hasha! Tumemjua kutokana na namna anavyotenzwa kama mtumwa wa mapenzi.
Kila asubuhi, iwe kiangazi chenye joto kali au kipupwe chenye baridi kiasi cha shughuli za umma kama biashara na shule kufungwa, utamuona akitweta akimtembeza mbwa wa mkewe.
Hakuna siku tulimuona mke akimtembeza mbwa zaidi ya kumuona naye akiwa amekaa kiti cha mbele mama aamuapo kutoka naye au kumpeleke saluni ya mbwa kupigishwa mswaki, kuoshwa na mengineyo au veterinari kuchunguzwa afya au kutibiwa.
Pia, kuna watu wanaopiga pesa nzuri kwa kufungua kambi za kutunzia mbwa. Hawa, wateja wao wakuu ni wafuga mbwa wanaofanya kazi zinazowanyima muda wa kukaa na mbwa wao.
Hivyo, kama wazazi wapelekevyo watoto wao chekechea au vituo vya kutunzia watoto, nao hupeleka mbwa wao kwenye maeneo haya kushinda huko hadi wanaowafuga warejeapo kutoka kazini.
Kwa tabia za walio wengi wanaopenda kufuga wanyama pendwa au pets kwa kimombo, wapo wanaokula hata kulala nao.
Utashangaa kukuta watu kama hawa wakiwabagua binadamu wenzao wasio Wazungu, lakini wakawapenda na kuwachukulia kama binadamu mifugo yao. Tunajua utashangaa.
Je, inakuwaje kwa mtu ambaye mila na desturi zake zinakinzana au kutofautiana na utamaduni huu? Ni mawili.
Mosi, mhusika ama akatae na kuamua kuachana au akubali kufanya anachotakiwa kufanya kwa sababu ndiyo njia yake ya kuishi.
Pili, mhusika akubali yaishe ateseke ili aweze kuishi. Haya ni machache tunayoyaona nje. Nani anajua mengi mengineyo ya ndani? Je, kwa mujibu wa mila na desturi za Kiafrika, unaweza kusema hii ni ndoa? Na kama ni ndoa, je ni ya amani na furaha?
Kutokana na mfumo dume wengi tunamotoka na tulimokulia, huwapa wanaume mamlaka makubwa na kuwanyima wanawake.
Je, katika mfumo huu tutakaouita mfumo jike, mume wa namna hii ameoa au ameolewa? Je, inakuwaje kwenye ndoa ya wawili wanaotoka jamii tofauti kutochanganya mila zao kwa usawa?
Japo si rahisi kueleza ni kwanini wapo baadhi ya wenzetu walioingia na kukubali au kulazimika kuukubali mfumo na ndoa hizi, hatujui kilichowasibu na kuwasukuma kuingia katika utumwa huu.
Juzi juzi tulishuhudia rais mbaguzi wa Marekani Donald Trump akiwafurusha wageni walioingia na kuishi Marekani kinyume cha sheria.
Hivi wengi ni wale walioingia kwenye nchi hizi kinyume cha sheria? Ni wale waliopenda kupitia kiasi? Hakuna jibu rahisi.
Kilicho wazi ni kwamba haya mambo yapo na yanafanywa na wale waliotuaminisha kuwa ni wastaarabu na wenye kupigania haki na usawa wa binadamu!
Japo hatujawahi kumhoji mhusika au tuseme mwathirika katika kisa hiki, ukimuona kwa macho, ni mtu asiye na furaha wala madaraka. Wakati mwingine, mbwa wake ana amani na furaha kuliko jamaa huyu ambaye siku zote ni mkimya anayejitahidi kuepuka kuzoeana na watu wengine kutokana na yanayomsibu.
Kwa upande wa pili, baba wa Kiafrika anapooa mama wa Kizungu na kumpeleka Afrika, kwanza, huonekana ana bahati kumuoa mtu bora kama Mzungu.
Pili, kwa ukarimu wa Kiafrika, mama husika huenziwa tofauti na wanaume hata wanawake wanavyofanyiwa huku.
Pamoja na hayo yote hapo juu, tofauti, Wanawake wengi wa Kifilipino, kama walivyo Waswahili, wanapenda kuolewa na wanaume wa Kizungu. Tulipohamia mji huu, hapakuwa na Mfilipino hata mmoja. Hata hivyo, alihamia mama mmoja Mfilipino ambaye ni nesi. Hakupita akaolewa na mzee wa Kizungu.
Ndani ya miaka miwili, idadi ya Wafilipino iliumka kutoka mmoja hadi zaidi ya 20. Katika kuchunguza, tuligundua kuwa, kama tulivyobainisha, kutokana na ugumu wa maisha huko kwao, Wafilipino wengi wameolewa na Wazungu ingawa si wengi waliooa Wazungu.
Tuna rafiki yetu wa Kizungu tuliyemtumia kupata mengi. Kwanza, binti yake wa pekee aliyemzaa na mama wa Kifilipino aliyemzidi umri alikuwa anasoma na mmoja wa wanetu pia kujifunza naye kareti.
Huyu baba, alituambia kuwa shangazi yake alikuwa akifanya kazi na nesi wa Kifilipino. Hivyo, siku moja wakiwa kwenye harusi ya ndugu yake, alikuja na mwanamke aliyemuunganisha naye ambaye sasa ni mkewe.
Tulimuuliza, inakuwaje wanaume wengi wa Kizungu hapa walichangamkia kuoa wanawake wa Kifilipino? Alijibu kuwa wanawapenda kwa sababu hawana makuu kama wanawake wa Kizungu.