Pemba. Baraza la Manispaa la Chake Chake limefanya operesheni maalumu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kukagua usafi kwa wafanyabiashara wa vyakula kwenye viwanja vya Sikukuu na kupiga marufuku baadhi ya biashara kama ya juisi.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Juni 8, 2025, wakati wa operesheni hiyo, mkurugenzi wa baraza hilo, Shida Kombo amesema lengo ni kuhimiza usafi kwa wafanyabiashara hao.
Amesema katika kipindi hiki cha mvua kunaweza kujitokeza mlipuko wa magonjwa kama wafanyabiashara hawatokuwa makini.
Shida amesema wamebaini baadhi ya wafanyabiashara hawapo makini na hawachukui tahadhari kwa kuacha wazi vyakula wanavyoviuza, jambo linalotishia usalama wa afya ya walaji.
Amesema wameamua kuja na operesheni hiyo inayohimiza wafanyabiashara kuweka mazingira salama ya vyakula wanavyoziuza.
Amesema mfanyabiashara yeyote atakaekaidi agizo hilo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kufungiwa au kulipa faini.
“Tumefanya operesheni hii katika maeneo ya biashara na sehemu za viwanja vya Sikukuu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tukiwa na lengo la kuwataka wafanya biashara kuchukua tahadhari kwa kuweka usafi na kuzifunika biashara zao hasa katika kipindi hiki cha mvua,” amesema Shida.
Aidha, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwafungia watoto vyakula waendapo shuleni ili kuepuka kununua ovyo vyakula mitaani.
“Hali hivi sasa si nzuri, vyakula vya kununua tu mitaani vinaweza kuwaletea athari watoto wenu, hivyo katika kujiepusha na hayo, lazima wazazi muwapikie watoto vyakula majumbani waje navyo shuleni vikiwa salama,” amesema.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Haji Khatib Haji amesema Wizara ya Afya imepiga marufuku uuzaji wa baadhi ya vinywaji kama juisi kwa sababu ni rahisi kwa mtumiaji kupata maabukizi.
“Bado tunaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na wananchi kuchukua tahadhari ingawa bado wengine wamekuwa wazito kuchukua hatua,” amesema.
Operesheni hiyo ya kuhamasisha usafi kwa wafanyabiashara itaendelea kufanyika kwenye maeneo yote ya biashara na viwanja vya sikukuu kisiwani Pemba.