Geita. Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amesema chama hicho kipo tayari kufia uwanja wa mapambano kikilenga kupigania haki za wananchi kuliko kushinda kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii na ‘Club house’ kupiga porojo.
Kauli hiyo ni muendelezo wa kurushiana vijembe na mahasimu wao wa sasa wa kisiasa, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliohamishia kampeni yao ya ‘No reforms no election’ kwenye mitandao hiyo na kugeuka shubiri na kero kwa baadhi ya watumiaji.
Kwa sasa mtu akichapisha maudhuhi yoyote yale katika majukwaa hayo, iwe kumpongeza mwanaye, Send -Off au maneno mengine yasiyokuwa na unasaba na masuala ya kisiasa, anajitokeza mmoja na kuandika ‘No reforms no Election.’
Tangu Chaumma kizindue kampeni yake ya C4C Juni3, 2025 viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, kimekuwa kikirusha vijembe kujibu hoja zote zinazotolewa na mahasimu wao hao ikiwemo ile wanayotuhumiwa kuwa ni wasaliti na wanapenda vyeo baada ya makada wengi kuhama Chadema na kujiunga na Chaumma.
Mtindo huo wa kuchongeana kwenye mikimutano ya hadhara unalenga kuwashawishi wananchi kuunga mkono misimamo yao ikiwemo ule wa Chaumma wa kushiriki uchaguzi Mkuu 2025 na ule Chadema wa No reforms no Election.

Akizungumza kwenye mkutano uliofanyika leo Jumapili Juni 8 eneo Katoro, mkoani Geita ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya hadhara ya C4C, Mwalimu amesema mabadiliko na haki za Watanzania zitapatikana kwa kuingia kwenye mapambano bila kujali aina ya mazingira yaliyopo.
“Chaumma tunasema, tupo tayari kufa kwenye mapambano kupigania haki za wananchi kuliko kushinda kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii na Club House kupiga porojo kama wanavyofanya wenzetu,” amesema Mwalimu.
Amesema chama hicho kinaamini mabadiliko ya kweli ya haki na mateso ya wananchi yatakoma kwa nguvu ya umma kupitia sanduku la kura badala ya kusubiria vipande vya makaratasi vinavyojadiliwa na baadhi ya watu.
“Chaumma tumegoma kususia uchaguzi, CCM si wakuwasusia uchaguzi, Chadema wanazungumzia kususia bila kuwaambia wananchi madhara yake, niwaambie tusijaribu kuwasusia CCM, tunaweza kupitia hali duni tena kwa miaka mitano ijayo, tusikubali, msidanganyike,” amesema Mwalimu.
Katibu mkuu huyo akijenga hoja hiyo kimkakati, amemtolea mfano aliyekuwa mwanasiasa nguli huko Zanzibar, marehemu Maalim Self akidai aligomea uchaguzi 2015 akiamini usingeweza kufanyika, lakini kilichotokea alistaajabu.
“Maalimu aliamini uchaguzi hautafanyika, CCM iliingia kwenye uchaguzi ikaenda kujitangaza kwenye kata zote na majimbo yote kuanzia Pemba na Unguja kote walishinda bila kupingwa,” amesema Mwalimu.
Amesema baada ya matokeo hayo,
Maliam alihangaika kwa miaka mitano mingine bila chama chake cha CUF kuwa na diwani wala mbunge.
Akaamua kwenda kushtaki kimataifa lakini walimgomea wakimueleza hawawezi kuingilia mambo ya ndani ya nchi.
“Pemba ambako hakukuwa na mwanachama wa CCM, lakini kwa sababu walisusia uchaguzi 2015 Pemba kuna wanachama wengi wa CCM,” amesema.
Amesema si hivyo hata Baraza la Wawakilishi kule Zanzibar, CCM walipitisha sheria mwaka 2018 ya kufanya uchaguzi siku mbili ambayo hadi sasa inaendelea kuwatesa.
“Haya yanayotokea si hadhithi, tatizo Chadema hawawaambii madhara ya kususia uchaguzi kwamba hayo yanaweza kutokea iwapo CCM tutawaacha washiriki uchaguzi bila kupingwa, wanaweza hata kupitisha katiba ambayo hatuitaki,” amesema Mwalimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchumi wa Chaumma, Catherine Ruge amesema Chadema kimegeuka kuwa chama cha wapiga dili kina taka kususia uchaguzi badala ya kuwapigania wananchi.
“Tutapambana na tutafia kwenye mapambano, tunaomba mtuunge mkono tutaweka wagombea wa udiwani, ubunge na urais, muwapigie kura tukafanye mabadiliko ya kweli bungeni tubadilishe mifumo ya nchi hii,” amesema Ruge.
Amesema Chadema hawana mbinu ya kuzuia uchaguzi huku akisema wananchi wenye akili timamu hawawezi kwenda kulala barabarani kuzuia uchaguzi ili wagongwe na magari.
Hata hivyo, madai hayo yamejibiwa na Msemaji wa Chadema, Brenda Rupia aliyekanusha hoja hiyo akisema Chadema hakiwezi kuwa chama cha kupiga dili isipokuwa Chaumma.
“Chadema hatuwezi kuwa wapiga dili. Kwanza hatujasema tutasusia uchaguzi isipokuwa tumesema tutazuia uchaguzi usifanyike na mbinu ya kuzuia hatuwezi kuisema kwa sasa wasubiri muda ukifika wataona,” amesema Rupia.
Katika maelezo yake akijibu kuhusu hoja ya wapiga dili, Rupia amedai Chaumma wao ni wapiga dili wanafanya mambo makubwa ambayo hayaakisi uchumi wao na hawasemi fedha wanazipata wapi.
“Ruge tunamjua tulikuwa naye Chadema na wenzake wote, Chaumma hakikuwa na uwezo huo wa ghafla wanafanya mambo bila kuwaeleza Watanzania chanzo cha fedha hizo ni wapi,” amesema Rupia.
Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Chaumma- Bara, Devotha Minja amesema wamejipanga kwenda kukaba “Huwezi kuchukua kombe bila kupeleka timu uwanjani. Tunachotakiwa ni kwenda kupambana kupiga chini CCM na kuweka Chaumma.”
Amesema wanaenda kupigania haki zao kwenye vituo vya kipigia kura kwani hawatakubali mgombea wao kuenguliwa na iwapo atashundwa kutangazwa baada ya kushinda.