Twange ang’aka, atoa maagizo kwa mkandarasi wa umeme jua

Shinyanga. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange amemuagiza mkandarasi wa mradi wa umeme jua kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba, huku akisisitiza kuwa Serikali nayo itatimiza wajibu wake kama mwajiri wa mradi huo anavyopaswa kuwajibika.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumapili Juni 8, 2025, alipokuwa akikagua mradi wa umeme jua unaotekelezwa katika Kijiji cha Ngunga, Kata ya Talaga, Wilaya ya Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, kufuatia mkandarasi kushindwa kukamilisha kazi ndani ya muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba.

“Tunamtaka mkandarasi kutekeleza wajibu wake, na sisi kama Serikali tutatekeleza wajibu wetu kwa sababu tumemuajiri. Sisi hatudai bali tunamdai,” amesema Twange.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Mkandarasi wa mradi huo, Daniel Xu kutoka kampuni ya Sinohydro, ametaja sababu ya kuchelewa kwamba ni mvua nyingi zilizonyesha mwaka jana.

Mkandarasi huyo amesema ziliathiri utekelezaji wa mradi kutokana na maji kujaa katika eneo la ujenzi, hata hivyo, ameahidi kutekeleza maagizo ya Serikali na kukamilisha mradi huo ndani ya muda wa nyongeza waliopatiwa.

“Mvua kubwa mwaka jana ilisababisha kuchelewa kwa kazi, lakini tumejipanga kuhakikisha tunakamilisha mradi kwa muda tulioongezewa,” amesema Xu.

Naye Meneja wa mradi huo, Emmanuel Anderson amesema mradi ulianza Desemba 2023 na ulitarajiwa kukamilika Februari 2025.

Hata hivyo, kutokana na changamoto zilizo nje ya uwezo wa mkandarasi, ikiwamo upungufu wa vifaa vya kupasua miamba na kusimika paneli za sola, Serikali imeongeza muda wa utekelezaji sasa unapaswa kukamilika Oktoba 2025.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Kwa sasa, utekelezaji wa mradi huo wa awamu ya kwanza umefikia asilimia 63. Kiwango cha usanifu ni asilimia 92.7, manunuzi yamekamilika kwa asilimia 78.3, na ujenzi upo kwenye asilimia 54.9,” amesema Anderson.

Ameongeza kuwa; “Mradi huu wa awamu ya kwanza unagharimu Sh118 bilioni na unahusisha usimikaji wa paneli za sola zenye uwezo wa kuzalisha megawati 50 katika eneo lenye ukubwa wa hekta 64,” amesema.

Related Posts