Watatu ACT Wazalendo wajitosa kupeperusha bendera Moshi Mjini

Moshi. Makada watatu wa Chama cha ACT-Wazalendo, wamechukua fomu ya kuwania ubunge jimbo la Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro, katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

Makada hao ambao ni Hassan Machaku, Elisha Mangwasi na Hanaf Mwetta wamechukua fomu kwa nyakati tofauti katika ofisi za chama hicho mkoa, zilizopo mtaa wa Kiusa, mjini Moshi, huku wakijipambanua kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanalichukua jimbo hilo ambalo limekuwa na historia ya upinzani.

Jimbo la Moshi Mjini ambalo kwa sasa  linashikiliwa na Priscus Tarimo (CCM), limekuwa na historia ya upinzani tangu uchaguzi wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi.

Akizungumza leo Jumapili 8, 2025 Katibu wa  ACT  Wazalendo jimbo la Moshi Mjini, Hassan Machaku amesema chama hicho kimejipanga vizuri kuhakikisha kinamsimamisha mgombea anayekubalika kwa lengo la kushinda kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Mpaka sasa wameshachukua fomu wanachama watatu ambao wanatia nia ya kugombea ubunge jimbo la Moshi Mjini, michakato inaendelea ili kumpata mgombea atakayepeperusha  bendera ya chama chetu kwenye uchaguzi hapo Oktoba,” amesema Machaku.

Machaku ambaye ni miongoni mwa waliochukua fomu ya kutia nia, amesema jimbo hilo lenye  kata 21, tayari kata 17 wamejitokeza wanachama kuomba ridhaa ya kugombea udiwani na chama chake kimejipanga kuhakikisha wanasimamisha wagombea wenye nguvu.

“Kata 17 tayari kuna watia nia na baadhi ya kata hizo wamechukua fomu zaidi ya wanachama wawili na mwaka huu tumejipanga vizuri kuhakikisha tunasimamisha wagombea katika kata zote 21 na ambao watakuwa na nguvu ya kuingia katika mapambano na vyama vingine na kupata ushindi” amesema Machaku.

Ameongeza kuwa; “kwa sasa kumekuwa na mwamko mkubwa kwa wanachama kujitokeza kuchukua fomu na chama tunataka tuchukue jimbo hili mwaka huu, ili tukaweze kushughulika na kero zinazowakabili wananchi ikiwemo miundombinu ya barabara kwenye kata hasa za pembezoni, kutetea masilahi ya watumishi ikiwemo walimu na madaktari, kuwainua vijana kiuchumi na kuimarisha michezo.”

Akizungumza na Mwananchi, Katibu wa mipango na uchaguzi wa Jimbo la Moshi Mjini, Ramadhan Khatib amesema mchakato wa uchukuaji fomu unaendelea katika jimbo hilo na watakamilisha shughuli hiyo Juni 30, mwaka huu.

“Uchukuaji fomu unaendelea katika Jimbo la Moshi Mjini na kikubwa tunajipanga kuingia kwenye mapambano ya uchaguzi na si kushiriki na tunataka kushinda jimbo hili” amesema Khatib

Related Posts