Hemed: Mamlaka za kodi zisiogopeshe walipakodi

Unguja. Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amezitaka mamlaka za usimamizi wa kodi TRA na ZRA kuhakikisha mfumo wa kodi ni wa haki, uwazi, rahisi kueleweka na wenye kuzingatia mazingira halisi ya biashara na uwekezaji ili kuwahamasisha walipa kodi.

Ametoa kauli hiyo leo Juni 9, 2025 wakati akifungua kongamano la kodi na uwekezaji na kuongeza kuwa, lazima mifumo hiyo iwe wazi na kuwahamasisha walipa kodi badala ya kuwaogopesha.

“Tunahitaji kuhakikisha walipakodi wanahamasishwa na siyo kuogopeshwa, pia kuwajengea uwezo watendaji wa mamlaka hizi wenye ujuzi, ufanisi na weledi ili kuhakikisha wanatoa huduma bora bila ya kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima na walipakodi,” amesema Hemed.

Kwa upande wa wafanyabiashara na wawekezaji, amewataka kuendelea kutii na kutekeleza sera na sheria za kodi ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa ufuatiliaji wa malipo ya kodi stahiki inayopaswa kulipwa.

Amesema kodi ni mapato ya nchi ambayo mfanyabiashara amekasimiwa kuyakusanya kwa niaba ya Serikali hivyo, pale mfanyabiashara anapokuwa hakusanyi kodi kwa kukataa kutoa risiti, maana yake amevunja sheria za nchi.

“Hali kadhalika, mwananchi anapoacha kudai risiti, maana yake anasababisha mapato ya nchi kupotea na anakuwa ni sehemu ya upotevu wa mapato hayo, hivyo, naye anapaswa kuchukuliwa hatua stahiki, hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kwa nafasi yake kutoa na kudai risiti kila anapofanya malipo ili kufikia malengo ya nchi yetu kwa pamoja,” amesema.

Hemed ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara wote wa ndani na nje ya nchi kwamba, Serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa kodi usiokuwa na changamoto, bali unaowasaidia kukua na kuchangia ipasavyo maendeleo ya nchi.

Pia, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya miundombinu, sera, sheria na huduma stahiki ili kuhamasisha uwekezaji nchini.

Kongamano hili ni fursa nzuri ya kuendeleza mjadala wa pamoja, kusikiliza changamoto za pande zote na kuzitafutia ufumbuzi.

“Kwa upande wa Serikali, tutaendelea kufanyia marekebisho, maeneo ambayo yanaleta ukakasi katika ushirikiano wa umma na sekta binafsi, hivyo, nawasihi kutumia fursa hii kujadili namna bora ya kuanzisha na kuimarisha mashirikiano baina ya sekta binafsi na sekta ya umma katika kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema nia ni kuwaunganisha sekta hiyo kuangalia sera na sheria zilizopo ili kushamirisha wafanyabiashara na uwekezaji kisiwani.

“Kwa namna yoyote ile lazima tuangalie sera na sheria zetu zinaweza kwenda na mabadiliko ya kiulimwengu, kwa hiyo hili ni jambo muhimu katika uchumi wa nchi yetu,” amesema Dk Mkuya.

Amesema hatua hiyo pia ni muhimu katika kipindi hiki cha kuelekea katika bajeti kuu ya Serikali kwani kumekuwapo na mchango mkubwa wa sekta binafsi katika utekelezaji wa wake na kupitia kongamano hilo watapata mawazo ambayo watayajumuisha katika bajeti hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake, Najima Hussein Abdalla amesema kongamano hilo litatoa fursa kueleza changamoto na kutengeneza mazingira mazuri ya biashara.

Amesema ni muhimu yafanyike katika makundi maalumu, “kundi la utalii, wafanyabiashara na wajasiriamali, wajenzi kila mmoja anaweza kuelezea changamoto kwa wingi ili ziweze kufanyiwa kwa urahisi zaidi.”

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara Zanzibar, Ali Amour amesema kuna changamoto nyingi katika utekelezaji wa kodi kwani zinakuwa ni nyingi lakini zinapitia maeneo mengi.

“Kodi sio tatizo kwa sababu ni msingi wa maendeleo, kwa hiyo kodi nyingi zinazotoka kama VAT zinalipwa lakini kazi inakuja pale kuzipeleka sehemu husika kwa sababu inadai uende sehemu moja na nyingine, hivyo haziendani inakuwa gharama kwa hiyo zinatakiwa kufanyiwa marekebisho ili zifanyike kwa urahisi,” amesema.

Related Posts