Katibu Mkuu Chama cha Wafugaji adaiwa kuchangisha fedha isivyo halali, ajibu

Simiyu: Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), kimeingia lawamani baada ya kudaiwa kuwachangisha fedha wakulima kutoka kila kanda kwa ajili ya maandalizi ya Kongamano la Wafugaji Tanzania.

Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Thomas Nkola maarufu,  Mkulima amepinga uamuzi huo akidai kuwa kongamano hilo linaandaliwa na Wizara ya Kilimo na Uvuvi na siyo wakulima.

 Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika Juni 14 hadi 15 katika Viwanja vya Nyakabidi, wilayani Bariadi, huku kilele chake kikitarajiwa kuwa Juni 16, 2025 na kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan kama mgeni rasmi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Juni 9, 2025 mjini Maswa, Mkulima amesema michango hiyo si halali kwa kuwa CCWT ni miongoni mwa waalikwa kwenye kongamano hilo kupitia mwaliko wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, na si waandaaji wakuu wa shughuli hiyo.

Amesema kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Mathayo Mgusa ameandika barua kwa vyama mbalimbali vya wafugaji ikiwemo Umoja wa Wafugaji Mkoa wa Kagera kuchangia Sh15 milioni kwa ajili ya kongamano hilo.

Hata hivyo Mathayo Mgusa, amesema baadhi ya watu wanaichanganya shughuli hiyo na uzinduzi wa kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa, ambao unaratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na pia utafanyika Juni 16, 2025, katika viwanja hivyohivyo vya Nyakabidi.

“Kuna barua yenye Kumb. Na. CCWT/HQ/2025/02 ya Juni 3, 2025, iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa CCWT ikiwataka wafugaji wa mkoa wa Kagera kuchangia Sh15 milioni kwa ajili ya kongamano hilo. Hii si sahihi, kwani chama kinatumia mwaliko wa wizara kama kigezo cha kuchangisha fedha,” amesema huku akionyesha nakala ya barua hiyo kwa waandishi wa habari.

“Awali kongamano hili lilitarajiwa kufanyika jijini Dodoma na lilishapata mfadhili aliyeahidi kutoa Sh52 milioni, kabla ya kuhamishiwa Simiyu bila maelezo ya kina,”amesema.

Ametoa wito kwa viongozi wa chama hicho kuzingatia uwazi na kuwaheshimu wafugaji wanaowakilisha, akisisitiza kuwa chama kisitumike kama kichaka cha kuchangisha fedha isivyo halali.

“Matendo kama haya ndiyo yanayopunguza imani ya wafugaji kwa chama na hata kwa serikali. Tuwaambie ukweli, tusitumie jina la Rais au mwaliko wa wizara kujinufaisha,” amesema.

Akizungumzia tuhuma hizo, Katibu Mkuu wa CCWT, Mathayo Mgusa amekiri kuwa chama hicho kimekuwa kikiomba michango kwa ajili ya kufanikisha kongamano hilo, lakini akasisitiza kuwa lengo ni kushirikisha wadau ili kufanikisha tukio hilo kubwa la kitaifa.

“Hili ni kongamano letu sisi wafugaji. Tumeona ni vyema kushirikisha wadau kwa kuwa gharama ni kubwa, hatuwezi kufanikisha pekee yetu. Hiyo barua uliyoitaja ni miongoni mwa juhudi zetu za uhamasishaji wa ushiriki wa kifedha,” amesema.

Mgusa amesema baadhi ya watu wanaichanganya shughuli hiyo na uzinduzi wa kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa, ambao unaratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na pia utafanyika Juni 16, 2025, katika viwanja hivyohivyo vya Nyakabidi.

“Kutakuwa na matukio mawili tofauti katika tarehe moja. Uzinduzi wa kitaifa wa chanjo na utambuzi wa mifugo unasimamiwa na wizara, huku kongamano likiwa ni la wafugaji. Hakuna mfugaji yeyote anayetozwa fedha kwa ajili ya tukio la wizara,” amesisitiza.

Amesema kuwa chama hicho kimekuwa kikitumia nguvu nyingi kuwakutanisha wafugaji wa maeneo mbalimbali ili kuwasemea na kusaidia kutatua changamoto zao.

Kongamano hilo linatarajiwa kukutanisha zaidi ya wafugaji 20,000 kutoka kanda mbalimbali za Tanzania, na litahusisha mijadala kuhusu maendeleo, changamoto na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.

Related Posts