Dar es Salaam. Katibu Mwenezi wa NCCR Mageuzi, Elisante Ngoma ametangaza kuhamia Chama cha ACT- Wazalendo huku akitaja sababu ni chama chake kupoteza dira katika kupambana na chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ngoma amekuwa miongoni mwa vigogo waliohamia kwenye chama hicho hivi karibuni, akitanguliwa na wakili Peter Madeleka, aliyejitosa ubunge Jimbo la Kivule pamoja na Katibu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda.
Akitangaza kuhamia ACT- Wazalendo leo Jumatatu Juni 9, 2025, Ngoma amesema amejiunga na chama hicho kwa sababu NCCR- Mageuzi imepoteza dira katika mapambano dhidi ya CCM.

Amesema wakati umefika wa kuachana na siasa za kuwalaghai Watanzania.
Pia, amesema anajiunga na chama hicho kuunga mkono juhudi za ACT-Wazalendo zinazotanguliza utu, uwajibikaji na maendeleo ya kweli ya kila Mtanzania. Anaamini naye atatoa mchango wake katika kufanikisha hilo.
“Nimevutiwa na jitihada za ACT- Wazalendo kuwalea vijana kiuongozi na kuwapa jukwaa kuonyesha uwezo wao. Nimechoshwa na siasa za kufifisha jitihada za vijana kukua kisiasa kwa kuwawekea vikwazo na kuzima sauti zao.
“Ninakuja ACT -Wazalendo kama kijana ambaye nipo tayari kupambana kwa nguvu zote kutekeleza malengo ya chama,” amesema Ngoma ambaye pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Vijana la Kituo cha Demokrasia (TCD).
Amesema amevutiwa na mipango ya ACT- Wazalendo kuelekea uchaguzi mkuu ujao kupitia kaulimbiu ya: “Tutashiriki tukipambana na tutapambana tukishiriki.”

Amesema uzoefu wa kisiasa umeonesha hivi sasa hakuna Tume Huru ya Uchaguzi. Hivyo, ACT- Wazalendo kushiriki uchaguzi ni jukwaa la mapambano.
“Ili kuonesha uzito wa hoja yangu, napenda kuchukua fursa hii kutangaza kuwa nitakisaidia chama changu kutekeleza malengo yake nyumbani Same Magharibi na maeneo mengine nchini,” amesema.
Ameongeza kuwa, Watanzania wanalia juu ya ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira, huduma mbovu za elimu na afya na kuporwa kwa rasilimali zao.
Ngoma amekishukuru chama chake cha zamani cha NCCR Mageuzi kwa heshima aliyopata ya kushika nafasi nyeti. Akiwa NCCR Mageuzi, amewahi kuwa Naibu Katibu wa Vijana Taifa, Katibu Mkuu wa Vijana Taifa na Katibu Mwenezi Taifa.