Dar es Salaam. Rasilimali za nchi zimetajwa kuwa vyanzo sahihi na vya kudumu vya upatikanaji wa fedha za kushughulikia Bima ya Afya kwa Wote, huku Serikali ikishauriwa kutumia wataalamu na kujifunza kutoka katika nchi zilizofanikiwa.
Vyanzo vilivyotajwa ni madini, gesi na rasilimali zingine za asili.
Ushauri huo umetolewa na wataalamu wa bima nchini, wakati wananchi wengi wakiwa na matarajio chanya kusikia kuhusu huduma hiyo katika Bajeti Kuu 2025/2026, inayotarajiwa kusomwa bungeni Alhamisi wiki hii.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Juni 9, 2025 Mkufunzi wa Chuo cha Afrika cha Bima na Hifadhi ya Jamii (ACISP), Anselim Anselim amesema suala la bima kwa wote ni la fedha inayoanza kwanza na afya ni unufaikaji wa fedha itakayowekezwa.
Hivyo wakati nchi inafanya maandalizi ilipaswa kujikita zaidi kuangalia kwanza ni namna gani fedha za kushughulikia bima kwa wote zitapatikana.
“Hivi juzi ilitajwa kodi ya kwenye simu tatizo kuna kodi nyingi mno eneo hilo ambazo zinaathiri uchumi, lakini vipo vyanzo vingine vingi kwa mfano tunasema kwenye sekta ya madini na gesi ambayo imeanza kuchimbwa, asilimia fulani ya mapato iende kushughulikia bima ya afya kwa wote,” amesema.
Anselim amesema vipo vyanzo vingine kwa mfano hati fungani ya jamii iwepo kwa ajili ya kushughulikia bima kwa wote kwa kuwa miaka ya mwanzo Serikali isitegemee itakuwa na wanachama wengi, lakini matumizi yatakuwa juu.
Pia amesema lazima zitengwe fedha za kutosha kushughulikia kundi la asilimia 24 kutoka kaya zisizo na uwezo huku akisema kuwa changamoto kubwa kwa sasa ni magonjwa yasiyoambukiza, hivyo michango pekee haiwezi kutosha.
“Ukianza huduma na fedha isiyojitosheleza utasumbuana na watoa huduma… mtu anaenda anaulizwa wewe ni wa bima kwa wote subiri kwanza, anawekwa kwenye folani itawarudisha nyuma wengine kujiunga na maana yake itakuwa haikui.
“Bima ni mchezo wa namba kwa maana hiyo fedha ni muhimu ili wanachama wawe wengi mfumo uweze kufanya kazi,” amesema.
Ametolea mfano wa nchi ya Rwanda yenye watu milioni 14 akisema kuwa ni miongoni mwa nchi zilizofanikiwa.
Hata hivyo, Watanzania kwa mujibu wa sensa iliyofanyika 2022 imefikisha idadi ya watu milioni 61.
“Pamoja na kwamba inatajwa kufanikiwa, wana changamoto kubwa kwa sasa ya kushindwa mahitaji ya mfuko na skimu, hii ni kwa sababu maandalizi hayakufanywa vizuri, nini kitakuwa chanzo cha kuwekeza fedha kwenye mfuko na matumizi wanayoyatarajia,” amesema.
Anselim amesisitiza kuwa pamoja na kwamba chanzo kikubwa ni uchangiaji katika mfuko, lakini unapoingia kwenye bima kwa wote, lazima uangalie vyanzo vingine vya kuongezea fedha.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Tanzania (Aphfta), Dk Samwel Ogillo amesema bajeti ya afya ina mwelekeo mzuri, kwa kuwa inaonyesha mpango mzima wa utekelezaji kuelekea bima ya afya kwa wote.
Hata hivyo, amedai bado kuna wasiwasi kutokana na uchumi wa nchi kuwa chini na hata rasilimali za nchi hazitoshi kuendesha kikamilifu.
“Tunaamini angalau itakapokuja bajeti kuu, itakuwa na maono ya kuhakikisha kuwapo kwa fedha fulani itakayoelekezwa moja kwa moja kutekeleza mpango huu,” amesema huku akisisitiza kuwa anatarajia kuona bajeti kuu inaonyesha utekelezaji wa mpango huo.
Wakichangia matarajio yao katika bajeti kuu, wadau wa elimu wamesema sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa ngazi ya msingi kwani miundombinu ya shule nyingi ni mibovu.
Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko amesema ni wakati sasa Serikali kuangalia upya kiwango cha fedha zinazotolewa kwa ajili ya kugharamia elimu bure ikiwemo ruzuku na fedha za fidia ya ada, kwani kilichopo hakiendani na gharama za maisha za sasa.
“Kiwango kilichopo kilifanyiwa makadirio siku nyingi, tufanye mapitio, tuweke viwango vipya,” amesema Nkoronko.
Viwango vilivyowekwa na Serikali kama ruzuku ni Sh10,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh25,000 kwa sekondari huku wadau wakipendekeza fedha hiyo kuongezwa hadi kuwa Sh25,000 kwa shule za msingi na Sh58,000 kwa sekondari
Maneno yake yaliungwa mkono na mwalimu mstaafu Kassana Maganga ambaye alitaka shule za vijijini kutupiwa macho kwani si wanafunzi pekee wanaopata taabu bali hadi walimu.
“Shule nyingi za vijijini walimu wanakosa ari ya kujituma kwa sababu mazingira yao ya kazi hayawahamasishi nyumba hakuna, kama zipo ni mbovu, au wanapanga mbali na sehemu zao za kazi kwa sababu maeneo ya karibu makazi hayaridhishi,” amesema.
Amesema jambo hilo wakati mwingine huwafanya walimu kutumia muda mwingi barabarani kabla ya kufika katika vituo vyao vya kazi na mara nyingine wanafika wakiwa wamechoka.
Mdau wa elimu, Dk Luka Mkonongwa amesema ni vyema kuwe na maboresho katika kila upande ikiwemo vifaa vya kufundishia, miundombinu ya kujifunzia na sehemu za kuishi walimu.
Pia ametaka kufanyika kwa uwekezaji katika ujenzi wa madarasa ili kupunguza mrundikano wa wanafunzi na kuwafanya kukaa kwa idadi ya 45 na wakizidi wawe 50, kama sera ya elimu inavyotaka.
“Darasa moja linabeba wanafunzi hadi 200 idadi ikiwa hivi, tusiwalaumu walimu kuwa hawafundishi vizuri kumbe tumewarundikia wanafunzi, kufanya hivi kunapunguza kutoa maarifa stahiki na matokeo yake wanafanya kazi bora liende, walimu waongezwe ili wagawane mzigo wa kufundisha,” amesema.
Mkonongwa amesema uboreshaji wa miundombinu ya vyuo vikuu nalo ni jambo ambalo linapaswa kuangaliwa kwani, ni moja ya sehemu ambayo inapaswa kuvutia hadi wanafunzi wa nje.