Mbeya. Majeruhi sita kati ya wanane waliopata ajali iliyoua 28, wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya kwa matibabu zaidi, huku miili ya marehemu ikiendelea kuchukuliwa na ndugu.
Ajali hiyo ilitokea juzi Juni 7, 2025 ikihusisha magari matatu katika mteremko wa Iwambi na kuua watu 27 papo hapo, mmoja akifariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali teule ya Ifisi iliyopo Mji mdogo wa Mbalizi.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali teule ya Ifisi, Dk Morice Martin amesema hadi sasa miili ya waliofariki inaendelea kuchukuliwa na ndugu na jamaa, huku majeruhi wakiendelea na matibabu.
Amesema kati ya majeruhi wanane waliolazwa hospitalini hapo, sita wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya na waliosalia hospitalini hapo afya zao zinazidi kuimarika.
“Sijawa na takwimu rasmi za miili iliyochukuliwa, lakini miili inazidi kutambuliwa na ndugu na wanaichukua, wale majeruhi baadhi yao wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa na wengine wamebaki hapa kwa matibabu, afya zao zinazidi kuimarika,” amesema Dk huyo.
Hata hivyo katika salamu za pole, Serikali iliahidi kugharamia matibabu kwa majeruhi na kutoa Sh500,000 kwa kila familia iliyopoteza ndugu katika ajali hiyo na gharama za majeneza.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera alipofika eneo la ajali na kuwatembelea majeruhi waliolazwa hospitalini Ifisi.
“Rais Samia Suluhu Hassan anatoa maelekezo kwa Tanroad (Wakala wa Barabara Tanzania) kuhakikisha wanaitengeneza hiyo barabara ya mchepuo ili magari makubwa yapite kule hapa pabaki kwa ajili ya magari madogo tu,” alisema Homera na kuongeza;
“Niwape pole waliopoteza wapendwa wao, niwaombe kuwa na subira katika kipindi hiki na Serikali iko pamoja na nyie, tutasimamia gharama za matibabu kwa majeruhi wote na kutoa mkono wa pole kwa wafiwa ambapo kila familia itapewa Sh500,000 na gharama za majeneza kwa miili yote 28,” alisema Homera.