Raia kupewa mafunzo ya ulinzi wa amani

Dar es Salaam. Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), kimezindua kozi ya mafunzo ya ulinzi wa amani kwa raia ikiwa ni kwa mara ya kwanza kufanya.

Lengo la kozi hiyo ni kuwaandaa na kuwawezesha raia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi wanapokuwa kwenye jukumu la ulinzi wa amani.

Kozi hiyo itaendeshwa katika ukumbi wa Chuo hicho cha Mafunzo kilichopo Kunduchi Dar es Salaam kuanzia Juni 9 hadi 13, 2025. 

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania, Brigedia Jenerali George Itang’are leo Juni 9, 2025 wakati akifungua kozi hiyo ya kwanza.

Kozi hiyo ya walinda amani wa kiraia ya Umoja wa Mataifa inafadhiliwa na Serikali ya Japan na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). 

“Kozi hii inalenga kutoa mafunzo kwa ajili ya moja kati ya vipengele vitatu vya ulinzi wa amani. Ulinzi wa amani unahusisha vipengele vitatu ambavyo ni cha raia, jeshi na polisi. Kipengele cha raia ndicho kikubwa zaidi kinachounganisha vipengele vyote vitatu.

“Katika kozi hii inalenga kutoa mafunzo kwa wale wote watakaounda kundi hili ambalo litakua ni nje ya polisi na jeshi katika ulinzi wa amani,” amesema Brigedia Jenerali Itang’are. 

Washiriki wa kozi hiyo ya mafunzo ni wale wenye sifa ya kuhudumu katika ulinzi wa amani kutoka taasisi mbalimbali za kiraia.

Amefafanua kwamba wana jukumu la kusimamia misheni za ulinzi wa amani, shughuli za kawaida za ulinzi wa amani.

“Tunatimiza maelekezo ya Afande Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Mkunda kwamba tuunganishe components (vipengele) zote tatu,” amesema.

Amesema kozi hiyo inaanza wa washiriki kutoka baadhi ya taasisi za kiserikali huku akibainisha kwamba wanazingatia matumizi ya teknolojia.

“Sasa hivi hata Umoja wa Mataifa una kitu kinaitwa ‘Smart Camp’ yaani kila kitu ndani ni cha kiteknolojia. Sasa na sisi tunawaandaa katika mazingira hayo ya kisasa,” amefafanua. 

Kwa upande wake, Mratibu wa programu za utawala bora kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Godfrey Mulisa amesema kwa kushirikiana na Serikali ya Japan na jeshi watawajengea  uwezo raia wa kawaida katika masuala ya kulinda amani.

Amebanisha nchi nyingi zinafanya mafunzo hayo ambayo ni rasmi, ni mfumo ndani ya umoja wa mataifa na ni fursa kwa raia wa Tanzania ambao wengi wao ni waajiriwa wa taasisi za Serikali.

“Tunategemea watakaopata mafunzo haya wanaweza kutumika kusaidia kutunza amani ndani na nje ya Tanzania kama raia na si kama tulivyozoea wanajeshi peke yake.”

Naye, mwakilishi wa ubalozi wa Japan, Nomura Hiroyuki amesema Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika mambo mbalimbali likiwamo hilo la masuala ya ulinzi wa amani.

Related Posts