Sheria yaja kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa maadili

Dodoma. Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali za Haki Jinai lengo ni kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa maadili.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sajini ameyasema hayo leo Jumatatu Juni 9, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), Noah Saputu

Katika swali hilo, Noah amehoji ni lini Serikali italeta marekebisho ya sheria ya ndoa.

Akijibu swali hilo, Sajini amesema kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha Sheria ya Ndoa, Sura ya 29, ndoa imetafsiriwa kuwa makubaliano ya hiari kati ya mwanamke na mwanaume kuishi pamoja, na inaweza kuwa ya mume mmoja na mke mmoja au mume mmoja na wake zaidi ya mmoja.

Hivyo, amesema sheria haitambui ndoa ya aina nyingine yoyote isipokuwa kama ilivyotafsiriwa katika sheria tajwa. 

Amesema Serikali imeendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ambapo wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Haki Jinai ambapo kifungu cha 176 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu. kimependekezwa kufanyiwa marekebisho.

Amesema lengo ni kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa maadili.

Katika swali la nyongeza, Bulaya amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la ndoa za utotoni na unyanyasaji wa watoto hao ambao wanaolewa wakiwa wadogo.

Amehoji Serikali wana mkakati gani wa kukomesha ndoa za utotoni.

“Lakini pia kumekuwa na manyanyaso sana ya wanawake na kupigwa wakiwa kwenye ndoa je, mmefanya utafiti wa kutosha kuona matukio hayo yamekuwa makubwa kiasi gani,” amehoji Bulaya.

Akijibu swali hilo Sajini amekiri kuwepo kwa matukio hayo katika baadhi ya maeneo lakini yanadhibitiwa kwa sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Mtoto inayozuia mtoto kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji, unyanyasaji ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni.

“Kwa hiyo tuna imani sheria hiyo ikisimamiwa vyema ikiwa ni pamoja na wananchi kuielewa na kuchukua hatua za kutoa taarifa kwenye vyombo vya usimamizi wa sheria ili hatua stahiki zichukuliwe. Hatua hizo ni pamoja na kufikishwa mahakamani tutakuwa tumesaidia kukomesha jambo hilo,” amesema.

Sajini amesema muhimu kuliko yote ni wananchi wa Tanzania kuzingatia maadili, mila na desturi ambazo zinazuia mtoto kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji ili hatimaye kuwa na kizazi chenye malezi bora zaidi.

“Kuhusu manyanyaso ya wanawake kupigwa ni jambo ambalo limepigiwa kelele mara nyingi na sheria zetu za jinai haziruhusu sio mwanamke tu bali hata mtu yeyote kupigwa,”amesema.

Amesema hivyo inapotokea mwanamke kapigwa kwa sababu tu yuko katika ndoa sheria zinaruhusu kulalamika katika vyombo vya usimamizi wa sheria ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wanaume wanaokiuka.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Thea Ntara amehoji baada ya maoni ya Sheria ya Ndoa yaliyokusanywa na wakapewa muda kama mwaka mzima, ni lini muswada wa sheria hiyo utapelekwa bungeni.

Akijibu swali hilo, Sajini amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha marekebisho kuandaa Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Kijinai na suala hilo litazingatiwa ipasavyo.

Related Posts