Unguja. Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo kwa kipindi cha mwaka 2024/25 imetoa tani 2,700 za mbolea visiwani Zanzibar.
Hayo yamebainishwa leo Juni 9, 2025 na Waziri Shamata Shaame Khamis wakati akijibu hoja za wawakilishi katika mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi.
Amesema kati ya kiwango hicho, Unguja ni 1,620 na Pemba 1,080 za mbolea.
Shamata amesema Serikali imezingatia unafuu wa gharama za upatikanaji wa mbolea kwa kuitoa ruzuku ya asilimia 50 ya bei ya sokoni.
Kilo moja ya mbolea inapatikana kwa Sh1,000 ikilinganishwa na Sh2,000 inayotozwa katika soko.
“Haya ni manufaa makubwa kwa mkulima, kwa kuwa gharama iliyokuwa inanunua mfuko mmoja wa mbolea, mwaka huu inanunua mifuko miwili ya kilo 50 za mbolea,” amesema.
Alikuwa akijibu hoja ya Mwakilishi wa Mwanakwerekwe Ameir Abdalla Ameir aliyetaka kujua ni tani ngapi za mbolea wamepatiwa wakulima kwa mwaka huu na kwa kiasi gani kumekuwa na unafuu katika bei za ununuzi wa mbolea hizo.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdulatif Yussuf akizungumza katika mkutano wa Baraza la wawakilishi
Katika swali la nyongeza mwakilishi huyo ameuliza namna ambavyo Serikali inavyosaidia wajasiriamali wadogo wanaotumia kilimo hai na kiwango kinachozalishwa cha mbolea kwa ajili ya wakulima hao.
Akijibu swali hilo, amesema hakuna kiwango kinachozalishwa kwa mbolea za asili isipokuwa wakulima wenyewe wanazalisha mbolea katika mazingira yao.
Mwakilishi wa Uzini, Shaban Haji Waziri amesema kuna taarifa nyingi za mbolea inayoingizwa nchini kuharibu ama ardhi au mazao na kutaka kujua kiwango cha athari kipoje.
Hata hivyo, Waziri Shamata amekiri kuwapo kwa baadhi ya changamoto akisema iwapo mkulima akizingatia maelekezo ya wataalamu itapunguza tatizo hilo.
Amesema kwa upande wa wizara wanaendelea na tafiti za namna gani wanawawezesha wakulima kwa kuwapatia mbinu bora za kuyatumia tena mabonde yaliyoathiriwa na maji ya chumvi.
“Hii ni pamoja na kuja na mbegu zinazostahamili maji ya chumvi katika udongo pamoja na kuja na mapendekezo ya aina ya mazao na miti ya kupanda katika mabonde yenye athari ya maji ya chumvi,” amesema.
Amesema Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Zari) kwa kushirikiana na Taasisi ya NIBIO kutoka Norway wanafanya tafiti katika maeneo hayo na kwa sasa tayari wameshachukua sampuli za udongo kwa ajili ya uchunguzi.
Waziri Shamata alikuwa akijibu hoja ya mwakilishi wa Chambani, Bahati Khamis Kombo aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuwasaidia wananchi waliokumbwa na maji chumvi kwenye mabonde.