Dar es Salaam. Tanzania imelenga kusajili miradi 1,500 ya uwekezaji mwaka 2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 60 ikilinganishwa na ile ya mwaka 2024.
Lengo hilo linawekwa wakati ambao tayari miradi 372 imesajiliwa kati ya Januari hadi Mei 2025 huku sekta ya viwanda ikiendelea kuwa kinara kwa kupokea mtaji mkubwa uliowekezwa katika usindikaji wa vyakula, viwanda vya bidhaa zinazotumika sana kama sabuni, vinywaji, chuma, karatasi za vifungashio na plastiki vikipata uwekezaji mkubwa.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Juni 9, 2025 na Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri wakati akizungumza na wanahabari juu ya mafanikio yaliyopatikana katika miezi mitano ya mwaka 2025.
Teri amesema ili kufikia lengo lililowekwa, wameweka kipaumbele katika kuhudumia wawekezaji waliopo kwa ukaribu na kutatua changamoto zao.
“Hii itafanikisha uwekezaji wao na kuwawezesha kufanya upanuzi wa uwekezaji wao hapa nchini na kuvutia uwekezaji zaidi na miradi ya ubia na Watanzania. Na hii inajidhihirisha kwa juhudi mbalimbali ambazo TIC inazifanya katika mikoa yote nchini na ushirikiano uliopo kati ya TIC na wakuu wa mikoa,” amesema.

Amesema juhudi zaidi zinaelekezwa katika kuhamasisha uwekezaji wa ndani na miradi ya ubia ili kuhakikisha wanakuza ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya uwekezaji.
Akizungumzia uwekezaji uliofanyika kwa miezi mitano, Teri amesema Januari hadi Mei 2025, TIC imesajili miradi 372 ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.04 ukilinganisha na miradi 335 iliyosajiliwa kipindi kama hicho mwaka jana.
Miradi hiyo ina thamani ya Dola 3,755.4 milioni za Marekani (Sh8.82 trilioni) ikiwa ni ongezeko ukilinganisha na Dola 2,847.6 milioni za Marekani (Sh7.7 trilioni) kipindi kama hicho kwa mwaka 2024. Miradi hiyo inatarajiwa kuzalisha ajira 41,117 itakapokamilika
Kati ya miradi iliyosajiliwa, 113 sawa na asilimia 30.37 inamilikiwa na Watanzania, miradi 186 sawa na asilimia 50 inamilikiwa na wawekezaji wa kigeni, 73 sawa na asilimia 19.63 ni ya ubia kati ya Watanzania na wageni.
Teri amesema sekta zilizoongoza kwa usajili wa miradi kwa Januari mpaka Mei 2025 ni viwanda vyenye, miradi 156 yenye thamani ya Dola 1,481.20 milioni za Marekani (Sh3.925 trilioni).
Sekta nyingine ni kilimo iliyosajili miradi 40 yenye thamani ya Dola 849.43 milioni za Marekani (Sh2.23 trilioni), Sekta ya usafirishaji ikiwa na miradi 56, yenye thamani ya Dola 337.83 milioni za Marekani (Sh888.49 bilioni).
Utalii ikiwa nafasi ya nne ni ujenzi wa majengo ya biashara yenye miradi 36 ya Dola 160.33 milioni za Marekani (Sh421.66 bilioni) huku utalii ukiwa na miradi 39, yenye thamani ya Dola 107.26 milioni za Marekani (Sh282.09 bilioni).
Katika kipindi hicho, mikoa iliyoongoza kwa usajili wa miradi inaongozwa na Dar es Salaam kwa miradi 134, Pwani (90), Arusha (29), Dodoma (14), Geita na Morogoro miradi 13 kila mkoa na kushika namba tano.
Teri amesema ili kuboresha uwekezaji wanaendelea na matumizi ya Sheria Mpya ya Uwekezaji (2022) ambayo inahusisha utoaji wa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kwa wawekezaji wa ndani na wa nje pamoja na kupunguza kiwango cha chini cha uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani.
Kiwango kimepunguzwa kutoka Dola 100,000 za Marekani (Sh263 milioni) hadi Dola 50,000 za Marekani (Sh131.5 milioni), jambo lililoongeza mwitikio wa Watanzania kuwekeza sambamba na uanzishwaji wa Ofisi ya Kanda ya Nyasa (Njombe).
“Ofisi hii inahudumia mikoa ya Njombe, Iringa, Ruvuma na Mtwara ili kusogeza huduma karibu na wawekezaji,” amesema.
Wakati lengo hili likiwekwa, wananchi wametaka usimamizi sahihi ili miradi yote ianze kutoa ajira.
“Kila siku tunaambiwa ongezeko, lakini ahueni huku mitaani haionekani, basi ni vyema miradi hii isimamiwe ili izalishe ajira na kupunguza watu mitaani wasiokuwa na kazi,” amesema Majura Msafiri mkazi wa Tabata, Dar es Salaam.