Wakili waliotumwa na afande ahoji walipo watuhumiwa wawili

Dodoma. Wakili wa kesi ya rufaa iliyokatwa na  Nyundo na wenzake, kupinga adhabu ya kifungo cha maisha gerezani, Godfrey Wasonga ameihoji Mahakama walipo watuhumiwa wawili waliotajwa na shahidi wa tatu (mwathirika) kwenye kesi ya kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume na maumbile Binti Mkazi wa Yombo Dovya Dar es salaam kwani ushahidi wa binti huyo unaonyesha watuhumiwa walikuwa sita.

Wasonga amesema kwenye kesi ya msingi shahidi wa tatu ambaye ni mhanga (mwathirika) wa tukio hilo aliyetambulishwa mahakamani kwa jina la X alisema kuwa watuhumiwa kwenye kesi hiyo walikuwa sita, lakini ukamataji ulifanywa kwa watu wanne na wawili hawajapatikana mpaka sasa.

Wasonga ameyasema hayo leo Jumatatu Juni 9, 2025 wakati akiwasilisha hoja za kukata rufaa ikiwemo suala la ukamataji wa watuhumiwa kuwa halikuzingatia matakwa ya kisheria.

Amesema wakati wa kutoa ushahidi binti huyo aliiambia Mahakama kuwa alikubaliana na mtuhumiwa mmoja aliyemtaja kwa jina la Kiboy ambaye alimpeleka nyumbani kwake maeneo ya Mpamaa jijini Dodoma, lakini walipokuwa hapo walivamia watuhumiwa watano na kuanza kumbaka na kumwingilia kinyume na maumbile.

“Sasa tunataka kujua hawa watuhumiwa wengine wawili wako wapi? hasa huyu Kiboy ambaye ndiye aliyemtongoza huyu binti na wakakubaliana kwa sababu hajakamatwa mpaka sasa, hapa mbele yetu tuna watuhumiwa wanne tu ambao ni kati ya watu watano waliovamia kwenye nyumba ya Kiboy,” amesema Wasonga.

Amesema hakuna ushahidi uliotolewa mahakamani ulioonyesha washtakiwa kuhusika kwenye tukio hilo hivyo wakaanza kukamatwa bali kila mmoja alikamatwa kivyake.

Amesema mshtakiwa wa kwanza MT. 140105 Clinton Damas ambaye alikuwa ni askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) alikamatwa akiwa kwenye kituo chake cha kazi kilichopo Msata Wilayani Chalinze mkoani Pwani, huku mtuhumiwa wa pili Amin Lema  alikamatwa eneo la Sudan Temeke Dar es Salaam alipokuwa kwenye biashara yake ya kuuza chipsi.

Amesema mtuhumiwa wa tatu Nickson Jackson alikamatwa eneo la Sinza Dar es salaam na mtuhumiwa wa nne C. 1693 WDR ambaye ni askari Magereza Praygod Mushi alikamatwa kwenye kituo chake cha kazi kilichopo Gereza la Isanga jijini Dodoma.

Amesema ukamataji huu unaonyesha kuwa hapakuwa na genge la uhalifu lililoundwa na washtakiwa hao na hauelezi ni nani aliyewataarifu wakamataji kuwa watuhumiwa hao ndiyo waliohusika kwenye tukio hilo.

Aidha amesema hata kifaa kilichotumika kuonyesha video za watuhumiwa hakielezi kama ndicho kilichorekodi au nacho kilipokea video kutoka kwenye kifaa kingine.

“Kwa hiyo hapo tutataka ushahidi kutoka kwa watalaamu wa mtandao ili kuthibitisha hilo,” amesema Wasonga.

Upande wa rufaa wameleta sababu 33 za kukata rufaa ambapo wameziweka kwenye makundi tisa na mpaka leo Juni tisa wamezungumzia makundi manne tu.

Baada ya kusikiliza upande wa rufaa jaji anayesikiliza kesi hiyo, Amir Mruma ameiahirisha hadi kesho Juni 10, 2025 itakapoendelea kusikilizwa tena kwa upande wa wakata rufaa kuelezea hoja zao.

MT. 140105 Clinton Damas, Amin Lema, Nickson Jackson na C. 1693 WDR Praygod Mushi walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani Septemba 30, 2024 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka kwa kundi na kumwingilia kinyume na maumbile Binti Mkazi wa Yombo Dovya, Dar es salaam.

Rufaa yao ilianza kusikilizwa Juni 3, 2025 ikiwa imepita miezi minane tangu wahukumiwe adhabu hiyo.

Related Posts