Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya mazungumzo na wawekezaji mbalimbali wenye uwezo wa kushirikiana na Serikali kuanzisha Shirika la Ndege la Zanzibar.
Mipango hiyo imeelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdulatif Yussuf katika mkutano wa 19 wa baraza la wawakilishi leo Juni 9, 2025 alipojibu hoja za wawakilishi hao Chukwani Zanzibar.
“Kwa sasa Serikali inafanya mazungumzo na Shirika la Ndege la Misri ili kuweza kufanikisha suala hilo, makubaliano ya awali juu ya uanzishaji wa shirika hilo yameshafanyika,” amesema.
Alikuwa akijibu hoja ya mwakilishi wa Mtambwe Dk Mohamed Ali Suleiman aliyehoji Serikali haioni ni muda muafaka sasa kuja na mkakati wa kuanzisha shirika lake la ndege.
Pia, amesema kwa muda mrefu, wananchi wa Pemba wamekuwa wakiomba Serikali kupitia wawakilishi wao kuwafikisha ombi la kupatiwa huduma ya ndege kupitia Shirika la Ndege la Air Tanzania na lini zitaanza safari hizo.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdulatif Yussuf akizungumza katika mkutano wa Baraza la wawakilishi
Katika swali la nyongeza la mwakilishi wa Ziwani, Suleiman Makame amesema jambo hilo la kupeleka ndege hiyo limekuwa la muda mrefu na kama Serikali imeshindwa ni vyema ikasema wazi kuliko kuendelea kuwaaminisha wananchi kuwa ndege itakwenda huko.
Hata hivyo, Naibu Waziri amesema katika kuimarisha usafiri kisiwani Pemba, Shirika la ndege la Air Tanzania linatarajia kuanza safari zake Julai mwaka huu.
Nadir amesema shirika limeshachukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuanzisha safari za ndege katika Uwanja wa Ndege wa Pemba.
“Ndege aina ya Q 300 yenye uwezo wa kuchukua abiria 50 ilishafanyiwa majaribio, safari za ndege kutoka shirika hilo zinatarajiwa kuanza rasmi Julai, 2025,” amesema Nadir.
Amesema wastani wa abiria kati ya 90,000 hadi 100,000 hutumia uwanja wa ndege wa Pemba kwa mwaka. Kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni abiria 97,375 na mwaka 2024/25 ni abiria 94,907 wametumia Uwanja wa Ndege wa Pemba.