Afariki dunia kwenye nyumba ya kulala wageni

Njombe.  Erasto Raphaely (50), mkazi wa Kijiji cha Igelehedza kilichopo Kata ya Ilembula, Wilaya ya Wanging’ombe, amefariki dunia katika mazingira yanayotajwa kuwa ya kutatanisha akiwa ndani ya nyumba ya kulala wageni pamoja na mwanamke anayedaiwa kuwa mke wa mtu.

Tukio hilo limetokea saa mbili usiku wa Jumapili ya Juni 8, 2025, ambapo marehemu aliripotiwa kuzidiwa ghafla akiwa chumbani na baadaye kufariki dunia akiwa njiani kupelekwa katika Kituo cha Afya cha Ilembula.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi wa awali umeonesha kuwa kifo hicho hakihusiani na tukio la jinai, bali kilitokana na kuzidiwa na msisimko wa tendo la ndoa.

Amesema tukio hilo limetokea saa mbili usiku wa Jumapili ya  Juni 8, 2025, huko wilayani Wanging’ombe, mkoani Njombe.

Akizungumza leo Juni 10, 2025, Kamanda Banga amesema kuwa marehemu, ambaye alikuwa na mwanamke mmoja (jina limehifadhiwa kwa sababu za kimaadili), alikuwa katika chumba kimojawapo kwenye nyumba ya kulala wageni (bila kuitaja jina) walipokuwa wakiendelea na tendo la ndoa, ndipo alipozidiwa ghafla.

Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda, marehemu aliwahishwa katika Kituo cha Afya cha Ilembula kwa lengo la kupata huduma ya haraka, lakini alifikia kituoni akiwa tayari ameshafariki dunia.

“Huyo marehemu alifikishwa katika kituo cha afya Ilembula baada ya kufikishwa hapo alitambulika kuwa amefariki dunia,” amesema Banga.

Kamanda Banga, amesema kuwa kutokana na mazingira ya kifo hicho, Jeshi la Polisi halitachukua hatua ya kumkamata mwanamke aliyekuwa na marehemu kwa kuwa limetajwa kuwa la kawaida, na uchunguzi wa daktari umebaini kuwa kifo kimetokana na kuzidi kwa msisimko wa tendo la ndoa.

Ameongeza kuwa hakuna dalili zozote za jinai zilizogundulika.

Aidha, Kamanda Banga ametumia fursa hiyo kuwasihi wanandoa mkoani humo kuwa waaminifu katika ndoa zao na kuepuka mahusiano ya nje ya ndoa, akisisitiza kuwa baadhi ya matukio kama haya huacha fedheha kwa familia tu, bali pia kuchangia kuathiri maadili katika jamii.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ilembula, Hezron Myale, amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa rasmi ya familia iliyosomwa wakati wa mazishi yaliyofanyika leo, Juni 10, 2025, marehemu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo kwa muda mrefu, na hilo linaelezwa kuwa chanzo kikuu cha kifo chake.

“Suala la nyumba ya wageni sisi hatuna taarifa tumesikia tu maneno ya hapa na pale kila mtu anapokuwa anaongea, lakini mimi kwenye taarifa ya historia ya marehemu kaburini tumeambiwa alikuwa na shida ya moyo,” amesema Myale.

Akizungumzia tukio hilo mkazi wa mkoani Njombe, Pashal Shauri amesema changamoto kubwa kwa sasa kwa wanandoa ni kukosa uaminifu, maelewano na uvumilivu hali ambayo inasababisha kusalitiana na kuleta migogoro katika familia.

“Tatizo kubwa ni ndani ya ndoa kwa sababu hakuna maelewano baina ya wanandoa na madhara yake ni kukamatwa ugoni na kuaibishwa na wakati mwingine watu kufanyiana visasi” amesema Shauri.