Moshi. Kijana Evance Geofrey (26) anayetuhumiwa kuwaua wazazi wake, Geofrey Motta (60) na Blandina Ngowi (53) eneo la Msufuni Msaranga, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, amepatikana akiwa hajitambui.
Taarifa zinadai kijana huyo aliokotwa barabarani na wasamaria wema na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kwa matibabu kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Inaelezwa kuwa, baada ya kufikishwa hospitalini hapo polisi walipata taarifa zake ndipo walipofika na kufanya taratibu za kipolisi.
Kijana huyo alipatikana Juni 5, 2025 akiwa hajitambui na sasa amelazwa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) akiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi.
Wanandoa hao waliokuwa wakazi wa Msufuni, waliuawa kikatili kwa kukatwa shingo na mwingine kunyongwa, usiku wa kuamkia Mei 29, 2025 na kisha miili yao kutelekezwa kwenye nyumba waliyokuwa wamepanga eneo la Msufuni, Manispaa ya Moshi.
Hata hivyo, miili ya wanandoa hao ilizikwa Juni 4, 2025 huko Kariwa chini, Kata ya Rau.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Abel Mtagwa akizungumzia mauaji hayo leo Juni 10, 2025, amethibitisha kupatikana kwa kijana huyo huku akisema yupo chini ya ulinzi na anaendelea na matibabu KCMC.
“Amepatikana akiwa hajitambui na alifikishwa Hospitali ya KCMC kwa matibabu Juni 5, 2025 tumemuweka chini ya ulinzi wa polisi akiendelea na matibabu,” amesema Kamanda Mtagwa.
Mwananchi lilipomtafuta mmoja wa ndugu wa mtuhumiwa huyo, Haika Geofrey alithibitisha ndugu yake kupatikana na kwa sasa amelazwa Hospitali ya KCMC.
Kuhusu mazingira gani ambayo ndugu yao alipatikana, amesema hajui chochote, bali alipata taarifa ya kulazwa KCMC.
“Sijui chochote, niliambiwa kalazwa hospitali ya KCMC akiwa hajitambui, sina taarifa zaidi ya hiyo,” amesema ndugu huyo.