Biashara zayumba Pakistan, mzozo na India watajwa sababu

Wachumi wamesema mapigano kati ya India na Pakistan yaliyodumu kwa siku nne kabla ya kusitishwa kwa faida ya pande zote mbili, yamesababisha uchumi wa Pakistan kuzidi kudorora.

Wakinukuriwa katika mtandao wa Dawn, wachumi hao wamesema suala hilo linatokana na Pakistan kuwa muagizaji mkubwa wa bidhaa kutoka India, kwamba mzozo kati ya mataifa hayo ulisababisha India kuzuia moja kwa moja baadhi ya makubaliano na nchi hiyo

‘’Pakistan iliagiza bidhaa kutoka India za thamani ya Dola 500 milioni kwa miezi tisa ya kwanza ya mwaka wa fedha uliopita. Mfano Januari hadi Aprili mwaka huu iliagiza sukari, kemikali, vifaa vya magari na petroli kutoka India, vyote vikiwa na thamani ya Dola milioni 448 milioni.’’

‘’Mwaka 2024, Pakistan iliagiza bidhaa zenye thamani ya Dola 1.2 bilioni kutoka India ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka Dola 530.91 milioni za mwaka 2023, ila kwa sasa suala hilo halipo,’’ alieleza mmoja wa wachumi hao kwa sharti la kutotajwa jina.

Wataalam hao walisema kutokana na kusuasua kwa uagizaji wa bidhaa, Pakistan ipo katika matatizo makubwa ya kiuchumi na biashara.

Kutokana na mgogoro huo soko la hisa la Pakistan nalo limeyumba kutokana na kuporomoka kwa uwekezaji huku Shirika la Fedha Duniani (IMF) nalo likieleza hatua ilizochukua kwa Pakistan kama masharti ya kuipatia nchi hiyo mkopo.

Related Posts