Daraja la Sh2.9 bilioni kurahisisha usafiri kati ya Momba, Tunduma

Songwe. Ujenzi wa daraja linalounganisha halmashauri za Momba na Tunduma mkoani Songwe umefikia asilimia 65.

Daraja hilo lenye urefu wa mita 54 linajengwa kwa thamani ya Sh2.9 bilioni na hadi sasa kiasi cha Sh1.5 bilioni kimeshalipwa kwa mkandarasi.

Meneja wa  Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), Wilaya ya Momba, Yusuph Shaban amesema ujenzi huo unatarajia kukamilika ndani ya miezi 24, ambapo hadi sasa limekamilika kwa asilimia 65 baada ya miezi 19 ya utekelezaji, na miezi mitano imebaki kukamilisha mradi na hadi kufikia sasa, mkandarasi amelipwa Sh1.5 bilioni.

“Daraja hilo linatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika ifikapo Oktoba 2025, na litakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Tarafa ya Msangano na Wilaya nzima ya Momba, kwa kuwa litaboresha mawasiliano na kurahisisha usafiri kati ya Momba na Tunduma,” amesema Shabani.

Akizungumza leo Juni 10,2025 alipokagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amesema daraja hilo litakapokamilika litawarahisishia mawasiliano wananchi wa halmashauri hizo mbili ambao wanajihusisha na kilimo cha mpunga, mahindi na ufuta.

Amesema kuwa kwa muda mrefu kusafiri kutoka Tunduma kupita eneo hilo ilikuwa ni anasa, lakini kukamilika kwa daraja hilo kutamaliza changamoto hiyo kwa wananchi wa Msangano na maeneo yote ya Momba.

Ujenzi wa daraja la Msangano – Chindi wilayani Momba mkoani Songwe ukiwa unaendelea.

“Niwapongeze sana Tarura kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa daraja hilo na miezi mitano iliyobaki wamsimamie mkandarasi amalize mapema ili msimu ujao wa mvua wapite juu bila adha yoyote.”

“Daraja hili likikamilika wananchi wataepukana na adha ya kuwa na mzunguko mrefu kufika Tunduma kupitia Mlowo na sasa watapita njia ya mkato kupitia daraja hilo” amesema Chongolo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Momba, Elius Mwandobo amesema daraja hilo ni kiunganishi kikubwa cha makao makuu ya Wilaya ya Momba yaliyopo Chitete na Halmashauri ya Tunduma, hivyo litakapokamilika litasaidia kukuza uchumi kwa wananchi wa wilaya hiyo katika masuala ya kilimo na usafirishaji

Related Posts