Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Vitambulishi vya Taifa (Nida) ikiwa miongoni mwa waliowasilisha gawio la Sh38.8 bilioni serikalini, minong’ono imeibuka huku wengi wakihoji fedha hizo zimetoka wapi.
Hiyo ni kutokana na kile kilichodaiwa na wengi kuwa Nida hutoa vitambulisho kwa wananchi bure na wanaopaswa kulipia Sh20,000 ni waliopoteza, fedha ambazo hata zikikusanywa haziwezi kufikisha kiwango hicho cha gawio.
Nida imeungana na mashirika mengine yaliyo chini ya Msajili wa Hazina kutoa gawio lake lakini yenyewe ikitoa asilimia 15 ya mapato ghafi kwa sababu haijiendeshi kibiashara.
Kwa ujumla leo Jumanne, Juni 10, 2025 Serikali imepokea gawio la Sh1.28 trilioni na kuwasilisha mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Wakati Nida ilipotajwa kuwa miongoni mwa watakaotoa fedha hizo, kelele za minong’ono zilienea ukumbi mzima wa Ikulu jijini Dar es Salaam na hasa kiwango cha fedha kilipotajwa.
Akielezea namna gawio hilo lilivyopatikana, Mkurugenzi Mkuu wa Nida, James Kaji amesema utumiaji wa taarifa unaofanywa na taasisi nyingine umekuwa chanzo cha kipato kwao.
Amesema maono ya mifumo kusoma ndiyo jambo lililofanya wao kupata namna ya kujiingizia kipato kutokana na kutoa taarifa za wananchi kwa taasisi mbalimbali zinapohitajika.
“Taasisi zote zinapotafuta utambuzi ikiwemo kampuni za simu, benki unapotaka kufungua akaunti wanataka kuchukua taarifa kutoka kwetu lazima walipie. Unapoomba taarifa kwetu akiweka kidole gumba cha mteja taarifa za muhusika kusoma hulipiwa Sh500,” amesema Kaji.
Kufuatia hilo wamekuwa na uhakika wa kukusanya zaidi ya Sh2 bilioni kila mwezi ambayo ni makusanyo kwa Serikali.
Amesema jambo hilo limerahisisha huduma na hata mtu akitaka kufungua akaunti hahitaji kutafuta barua za watendaji na wanapotaka kusajili simu malipo ambayo hutumia fingerprint ikiwemo Tamisemi.
“Ni maelekezo ya mifumo kusomana ndiyo yaliyofanya hadi tukapata gawio hili tu,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania ( TPDC), Mussa Makame amesema kuongezeka kwa gawio walilotoa kutoka Sh10 bilioni hadi Sh11.5 bilioni mwaka huu kunatokana na kusomana kwa mifumo.
“Haya ni mafanikio yaliyotokana na maono ya Serikali na viongozi wake sambamba na watumishi na uongozi wa TPDC na kampuni zetu tanzu katika kuhakikisha tunatimiza majukumu yetu ya kila siku, ili tuwe na matokeo chanya,” amesema.
Kwa upande wake, Kamishna wa Mamlaka ya Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo amesema mchango wao kama taasisi isiyokuwa ya kibiashara umetokana na uwekezaji uliofanyika.
TFS mwaka 2024 walichangia Sh21 bilioni ambayo iliongezeka hadi kufikia Sh29.8 bilioni.
“Jambo hili halijatokea hivihivi, Serikali imewekeza katika misitu na sisi tumepewa dhamana kuisimamia na kuiendeleza ikiwemo rasilimali watu ambao wameajiriwa,” amesema.
Amesema kwa sasa wanakusanya fedha kutoka vyanzo endelevu ikiwemo mashamba ya miti, utalii ambalo linatekelezwa kwa sehemu kubwa na mazao ya nyuki.
“Uwekezaji katika mifumo ya Tehama nayo imesaidia sana kukusanya mapato ya Serikali na matumizi yake, imetusaidia sana kutoa huduma kwa haraka na uhakika,”
Hilo limeenda sambamba na kufanya uwekezaji wa mkakati na kuendeleza mazao ambayo hayakuwa ya kitamaduni katika sekta ya misitu ikiwemo utalii, maeneo hayo yamewekezwa sasa na kutanua wigo wa huduma za kitalii.