Dodoma. Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma imeendelea kusikiliza hoja za rufaa kupinga kifungo cha maisha jela walichohukumiwa Clinton Damas, maarufu Nyundo na wenzake, huku upande wa Jamhuri ukiomba kuzijibu Juni 12, 2025.
Warufani wanaiomba Mahakama kufuta kesi, hati ya mashitaka na hukumu iliyotolewa dhidi yao wakidai ilikuwa kinyume cha sheria.
Waliokata rufaa ni Nyundo aliyekuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Amin Lema, Nickson Jackson na aliyekuwa askari Magereza, Praygod Mushi waliotiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela Septemba 30, 2024 kwa kosa la kumbaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam.
Akiwasilisha hoja mahakamani hapo leo Jumanne Juni 10, 2025 mbele ya Jaji Amir Mruma, wakili wa warufani hao, Godfrey Wasonga amedai kulikuwa na dosari za kisheria katika kesi hiyo kuanzia hati ya mashitaka hadi hukumu.
Amedai ushahidi wa video uliotolewa mahakamani umeshindwa kuwatia warufani (washtakiwa) hatiani kwa sababu mashitaka waliyoshtakiwa nayo hayakuonekana kwenye video hizo ambayo ni kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume cha maumbile mwathiriwa wa tukio hilo.
Wasonga amedai makosa yanayoonekana kwenye video ni mwathirika wa tukio hilo aliyetambulishwa mahakamani kama XY kuonekana akimnyonya uume mshtakiwa wa pili, kosa ambalo linaangukia kwenye shambulio la aibu ambalo lina vifungu vyake vya sheria.
Kuhusu kurekodi video na kuzitumia mtandaoni, Wasonga amedai kosa hilo linaangukia kwenye Sheria ya Makosa ya Mtandao ambalo lina vifungu vyake vya sheria pia.
Amedai Mahakama ilionyeshwa vipande vinne vya video ambavyo ni 6, 7, 8 na 9 lakini kwenye hukumu vipande vya video vilivyowatia hukumuni ni namba 1, 2, 3 na 4 ambavyo havikuonyeshwa mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa wakili huyo, vipande vya video vilivyoonyeshwa viliwaonyesha washtakiwa wakijirekodi wakiwa wanacheza muziki, huku wakiwa na chupa za vinywaji lakini hazikuonyesha wakiwa wanatenda kosa la kubaka kwa kikundi wala kulawiti.
Wasonga amedai maelezo ya shahidi wa tatu ambaye ni mwathirika wa tukio hilo alifika kwenye nyumba baada ya kukubaliana na mtu aliyetajwa kwa jina la Kiboy, ambaye walikutana kimwili na wakati wameshamaliza ndipo watu watano waliingia na kuanza kumbaka na kumwingilia kinyume cha maumbile.
“Sasa hapa tunataka tujue mshtakiwa namba moja alikuwa ni huyu Kiboy ambaye hajatajwa mahali popote hata kuonyeshwa kwenye video, sana sana wanaoonekana ni hawa watuhumiwa wanne ambao wao walikuwa wanacheza na kunywa vinywaji kwenye video hizo,” amedai.
Kuhusu video kukutwa kwenye simu ya mrufani wa kwanza ambayo ni aina ya Google Pixel, Wasonga amedai hakuna ushahidi unaoonyesha simu hiyo ilikuwa inamilikiwa naye.
Amedai wataalamu wa simu na kompyuta kutoka Jeshi la Polisi hawakutoa ushahidi mahakamani kuwa baada ya kuchukua simu walizuia vitu kuingia ndani au kutoka nje ya simu hiyo, hivyo ilipoteza sifa ya kuendelea kuwa ushahidi mahakamani hapo.
Amedai mwenye mamlaka ya kuthibitisha kuwa simu inamilikiwa na nani ni kampuni ya mawasiliano ya simu ambayo ilitajwa mahakamani, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na risiti inayoonyesha jina la aliyenunua au boksi la simu.
“Lakini hakuna ushahidi ulioletwa mahakamani ulioonyesha hayo yote, hakuna mwenye mamlaka hata mmoja aliyekuja kutoa ushahidi kuwa simu hiyo ilikuwa ni ya mshtakiwa namba moja, kwa hiyo upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha kosa bila kuacha shaka,” amedai.
Wakili amedai ushahidi uliotolewa mahakamani ulikuwa umekatika, hivyo haupaswi kuaminika kwa sababu ni wa kutengenezwa na kupikwa, akiiomba Mahakama kutupilia mbali hukumu iliyotolewa dhidi ya warufani na iwaachie huru.
Kuhusu washtakiwa kutambuliwa kwenye video zilizosambaa mtandaoni, Wasonga amedai aliyetoa ushahidi huo alikuwa hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, ambaye kisheria hatakiwi kutoa ushahidi zaidi anatakiwa kupokea ushahidi.
Amedai katika hukumu, hakimu amesema aliwatambua washtakiwa kwa kutumia video, pia kulikuwa na chupa za vinywaji, pakiti tano za kondomu na nyingine zilizokuwa zimetumika.
“Hili nalo lilikuwa jipya kwa sababu mwathiriwa hakutaja popote masuala ya kondomu wala kuomba maji ya kunywa lakini hakimu ameyaandika kwenye hukumu iliyowatia hatiani warufani, aliyatoa wapi?” amehoji.
Wakili mwingine wa warufani, Robert Owino amedai hakuna ushahidi unaoonyesha warufani (washtakiwa) hao wanne walifanya kosa la kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume cha maumbile mwathiriwa kwa sababu unaonyesha mwathiriwa alikutana kimwili na mtu mwingine kabla ya watuhumiwa wengine kuingia.
“Sasa hapa inakuwa vigumu kujua kama hiyo michubuko aliyoipata ilitokana na yule waliyekubaliana naye au watu wengine kwa sababu haijathibitishwa na ushahidi wowote,” amedai.
Meshack Ngamando, wakili mwingine wa warufani amedai hata kama kesi ilikuwa na masilahi ya umma, lakini mahakama ilipaswa kuzingatia haki na uhuru wa washtakiwa badala ya kuangalia masilahi ya umma peke yake.
Upande wa Jamhuri umeiomba Mahakama kuwapa siku moja ili kuandaa majibu ya hoja za warufani ambayo watayawasilisha Alhamisi, Juni 12, 2025. Kutokana na ombi hilo, Jaji Mruma ameahirisha rufaa hiyo hadi siku hiyo saa 4:00 asubuhi.