Mwarobaini wa utoro shuleni | Mwananchi

Dodoma. Utoro unatajwa kuwa mojawapo ya sababu kuu za matokeo mabovu ya wanafunzi wanaomaliza shule za msingi na sekondari.

Taarifa mbalimbali kutoka serikalini zinaonyesha bado kuna tatizo kubwa la utoro shuleni, ambapo idadi kubwa ya wanafunzi wanashindwa kumaliza masomo huku darasa la nne likitajwa kuongoza kwa wanafunzi watoto wanaoacha masomo.

Taarifa ya Ofisi ya Rais-Tamisemi  kuhusu utoro zilizopo katika ripoti ya takwimu za elimu msingi (Best) zinaonyesha kuwa mwaka 2022 jumla ya wanafunzi 193,605 waliacha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo utoro.

Mwaka 2023 jumla ya wanafunzi walioacha masomo kwa shule za Serikali na taasisi binafsi walifikia 158,372 licha ya juhudi na mikakati inayofanyika kuondoa tatizo hilo.

Serikali kwa upande wake inaeleza kuwa bado kuna shida mahali na bila kukubaliana kwa pamoja, hali hii itakuwa ni mazoea ya kila siku ama kuwa mbaya zaidi ya sasa kwa siku zijazo.

Makongamano, semina, mikakati, maagizo na wakati mwingine shuruti bado hazijamaliza tatizo huku Kwa upande mwingine tatizo linazidi kuongezekana kutokana na mvutano wa pande mbili.

Hivi karibuni,   Tamisemi kupitia mradi wa Shule Bora kwa kushirikiana na Serikali ya Uingereza,  waliendesha mafunzo ya siku tatu kwa maofisa elimu wa mikoa kwa ajili ya kutafuta mbinu ya kumaliza tatizo hilo.

Bakari Jiri kutoka Ofisi ya Elimu Mkoa wa Pwani akiwasilisha mada kuhusu mkakati wa kukomesha utoro katika mkoa wa Pwani.

Wakiishi wa mikoa saba kati ya tisa inayotekeleza mradi huo ulio chini ya Shirika la Maendeleo la Uingereza (FCDO) , walishiriki sambamba na watendaji kutoka ofisi za mikoa na walimu.

Mratibu wa mradi huo huo kutoka Tamisemi, Winfrid Chilumba anasema pamoja na semina na mikakati inayowekwa, kuna mahali hapajakaa sawa.

“Kama hatutakubali kuyashirikisha makundi muhimu katika jamii wakiwemo wazee maarufu, viongozi wa dini,watu wa mila na wenye ushawishi bado safari haitakuwa na maana,” anasema.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, makundi hayo yanasikilizwa zaidi kuliko hata matamko na makemeo kutoka kwa baadhi ya viongozi, hivyo wakiamua kulivalia njuga jambo hilo wanaweza  kulitafutia mwaribaini wake.

Anaeleza kuwa mradi huo huo unalenga.

 kupunguza changamoto za utoro, mimba za utotoni na mdororo wa elimu ambao unaanzia shule za msingi.

Chilumba anasema matatizo ya ujifunzaji na ufundishaji siyo makubwa isipokuwa wengi hawaamini katika usaidizi wa watu wengine.

“Wazee wakisema hakuna kukata mti watu wanaogopa, na wakisema huo mto msichote maji watu wanaacha sasa lazima tuamini kuwa nguvu kubwa ipo huku,” anasema.

Ofisa huyo anasema mkakati mkubwa ni kubadili fikra za watu kwani si kila jambo au tatizo litatatuliwa kwa fedha.

Hata hivyo, anakiri utoro umeipungizia Serikali baadhi ya misaada kutoka kwa wahisani kwani wanaposaidia kwenye elimu wamekuwa na vigezo vyao ikiwemo kutaka kupunguza utoro.

Kabla ya mkakati shirikishi haujatolewa na Tamisemi, washiriki katika mafunzo hayo walikuja na mbinu waliyoitaja ingemaliza utoro shuleni.

Wengi walitaja kuwa tafiti zinabainisha kwamba wangeweza kuondoa tatizo ikiwa suala la chakula shuleni  litapewa msukumo.

Ofisa Elimu, Bakari Jiri kutoka Mkoa wa Pwani anasema kuna shida ya utoro lakini akabainisha mambo manne kuwa yanawavuta nyuma katika matokeo.

“Kwanza ni ukosefu wa chakula shuleni,morali ya ujifunzaji kuwa chini, mazingira duni ya kujifunzia na ari kwa walimu katika ufundishaji nayo haipo hivyo wanafunzi ni kama wanakata tamaa kwenda shule,”anasema.

Mwalimu huyo anataja sababu nyingine ni baadhi ya wazazi kutoipa  elimu kipaumbele, hivyo  kuchangia  utoro uliopitiliza.

Kwake anaona suala la chakula kama litapewa kipaumbele na kila mtoto akapata chakula shuleni, litaondoa utoro katika mkoa wa Pwani.

Anasema wazazi wengi wamekata tamaa na hawajishughulishi kufuatilia taarifa na maendeleo ya watoto wao shuleni.

“Wakishawaandikisha basi hata hawajui kama mtoto anasoma ama ameolewa na ameachana na mambo ya shuleni,” anaeleza.

Kwa upande wake, Kasisi Kandoro kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma aliwaambia washiriki wenzake kuwa utoro shuleni unachangiwa na vitu vingi lakini ushirikiano hafifu kutoka kwa wazazi nacho ni chanzo kingine.

Kandoro ambaye aliwasilisha andiko la mkakati wa ufumbuzi kwa washiriki wa Mkoa wa Mara, anasema jamii haioni tatizo hata wanapokutana na watoto mitaani ni kama hawastuki kwa sababu hawajashirikishwa.

Hata hivyo, alibainisha namna utoro unavyoficha vipaji vya wanafunzi akitolewa mfano wa mmoja wa watoto aliyekuwa mtoro lakini walipomrudisha alisoma muda mfupi akaongoza kwenye matokeo ya mitihani yake.

“Sisi Mara tumewashirikisha  viongozi wa Serikali, dini na wadau wengine ili kuwa na mkakati wa pamoja na kwa namna moja tumeanza kuona matunda,” anasema Kandoro.

Kama ilivyo kwa Mkoa wa Pwani, anataja suala la chakula shuleni kwamba lingeweza kuwa mwarobaini kwani wengi wanatoka katika mazingira yenye kipato duni.

Katika hatua nyingine taarifa zinaonyesha Wilaya ya Kilindi  katika Mkoa wa Tanga suala la chakula siyo shida tena kwani karibu asiliamia 96 ya shule zote wilayani humo wanafunzi wake  wanapata chakula.

Kwa upande wa Dodoma, Wilaya ya Bahi imekuwa ikifanya vizuri kwa miaka mitatu mfululizo tangu walipoanzisha mkakati wa kutoa chakula shuleni.

Related Posts