Mbeya. Katika kuhakikisha Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya inaondokana na adha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, Serikali imetoa zaidi ya Sh16.5 bilioni kutekeleza miradi ya kimkakati itakaobhudumia wananchi 53,000.
Miradi hiyo itahusisha Kata saba zenye vijiji 25, sambamba na kuanza utekelezaji wa usanifu wa mradi wa maji kutoka mwambao mwa Ziwa Nyasa na uchimbaji wa visima virefu vitano.
Hatua hiyo imetajwa ni mikakati ya Serikali ya awamu ya sita katika kufikisha huduma kwa wananchi wa mijini na vijijini ikiwa ni kufikia malengo ya kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025.
Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Hance Patrick amesema hayo leo Jumanne Juni 10, 2025, ikiwa ni siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi hiyo.
Amesema miongoni mwa miradi inayotekelezwa ni wa Kata ya Ngana ambao utahudumia vijiji 25 na kugharimu Sh8 bilioni.
Mradi mwingine wa Sinyanga awamu ya kwanza ambao umekamilika na kugharimu Sh900 milioni kupitia fedha za Uviko-19, sambamba na mradi wa Kijiji cha Lema wenye thamani ya Sh415 milioni , ambao wananchi wameanza kunufaika.
Mhandisi Patrick, amesema ili kuhakikisha Wilaya ya Kyela inaandika historia ya changamoto ya maji tayari Serikali imetoa Sh672 milioni kwa ajili ya mradi wa ziwa nyasa ambao upo kwenye hatua ya usanifu.
Katika hatua nyingine amesema wanatekeleza miradi ya uchimbaji visima virefu 30 katika majimbo yote ya Mkoa wa Mbeya, huku kwa Wilaya ya Kyela imenufaika na visima vitano vyenye thamani ya Sh300 milioni ambavyo vimefikia asilimia 70.
“Lakini pia Serikali imeendelea kuwekeza katika miradi mingine hususani wa Mbambo wenye thamani ya Sh4.7 bilioni, na Ipinda wenye thamani ya Sh697 milioni,” amesema.
Awali, Mbunge wa Kyela Ally Mlaghila (Kinanasi), amesema wana kila sababu ya kuishukuru Serikali ya awamu kwa kile alichoeleza ni kuwapendelea kwa kutenga fedha nyingi kutatua kero ya maji.
“Tumeshuhudia hapa Kyela kuna visima vitano kikiwepo cha Mpuguti ambacho kimekamilika na huduma ya maji inaendelea kwa wananchi na maeneo mengine yaliyotajwa.
“Pamoja na miradi hiyo iliyotekelezwa, lakini tumesikia Meneja Ruwasa amesema kuna usanifu wa maji kutoka ziwa nyasa kuleta katika Wilaya nzima ya Kyela na Mkoa wa Mbeya na kwamba huo ni mpango wa Serikali kutengeneza gridi ya Taifa ya Maji,” amesema Dk Homera.
Amebainisha kuwa gridi hiyo ya Taifa itahusisha pia upande wa ziwa Tanganyika ambalo litasambaza maji mikoa ya Magharibi, lakini pia kwa upande wa ziwa nyasa Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya na mikoa ya jirani itanufaika.
Homera amesema utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima vitano wilayani humo hauna fidia zozote kwa wananchi watakaoguswa, lengo la Serikali ni kufikisha huduma kwenye maeneo yenye adha.
“Tunaomba tu wananchi onyesheni ushirikiano kwa sababu huduma hiyo haibagui wanaotaka fidia na wasiotaka lengo ni kuona wananchi wanapata maji safi na salama,” amesema.
Mkazi wa mikoroshini, Anna Sanga amesema ujio wa miradi ya visima unakwenda kuwa suluhisho la changamoto ya adha ya maji katika baadhi ya maeneo.