Wawakilishi walia Sheria ya Udhalilishaji kutumika kama kichaka cha kukomoana

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imekiri sheria ya kuwanyima dhamana watuhumiwa wa udhalilishaji ina upungufu huku wananchi wakiitumia kama kichaka cha kukomoana.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma amesema wakati mwingine watu wanakuwa na ugomvi wa kawaida mtaani, lakini wanatumia mwanya huo kuwabambikiza kesi na wengi wameshaumizwa kutokana na sheria hiyo.

Hamza ametoa kauli hiyo leo Juni 10, 2025 wakati akijibu hoja katika mkutano wa 19 wa Baraza la wawakilishi Chukwani, Zanzibar.

Alikuwa akijibu swali la nyongeza la mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir.

Ameir amehoji ni lini mwarobaini wa kukomesha tabia hiyo ya kubambikiziana kesi na kuwaumiza wengi utapatikana, kwa kuwa inapofika mahakamakani wengi hukutwa hawana hatia.

Kuhusu sheria inayowanyima dhamana watuhumiwa wa udhalilishaji kutumiwa kama kichaka cha kukomoana, Hamza

katika majibu yake amesema kuna changamoto kwa wananchi ya kubambikiana kesi kwa lengo la kukomoana.

Amesema watu wakitofautiana mitaani hujenga tabia ya kubambikiziana kesi, baadaye inabainika mshtakiwa hakuwa na kosa mahakamani, lakini tayari anakuwa ameshaumizwa ikizingatiwa kesi hizo zinatumia muda mrefu kumalizika.

“Ni kweli kuna changamoto katika sheria hii, watu wanatumia mwanya wa kutokuwa na dhamana kubambikiziana kesi kwa sababu wanajua mpaka kesi ije kumalizika tayari anakuwa ameshakaa ndani kwa kipindi kirefu maana kesi zenyewe hazisikilizwi haraka.

 “Na ukiangalia kesi nyingi za namna hii wengi ni vijana kwa kweli wanapoteza mwelekeo wao wa maisha, na inabainika wengine wanakuwa tu wamegombana mtaani, lakini wanasingizia kudhalilishwa,” amesema Hamza.

 Ili kupata mwarobaini wa tatizo hilo, Hamza amesema ipo haja kama wakiona inafaa baraza litunge sheria nyingine kwani sheria zote zinapitia kwenye baraza hilo na hiyo ilipitia humohumo.

 “Kwa sababu hakuna njia nyingine kama tunavyojua polisi na Mahakama wanatumia sheria hizo mbazo zinapitia hapa barazani, kwa kuwa sheria bado ipo lazima itaendelea kuumiza wengi, kwa hiyo cha kufanya baraza linaweza kubadilisha sheria hii kupitia kamati au mwakilishi akaja na hoja binafsi tukajadiliana kisha kubadilisha sheria hii,” amesema Hamza.

Hamza amesema kuanzia mwaka 2023 hadi Machi mwaka huu jumla ya kesi 651 zimefikishwa mahakamani, mwaka 2023 kesi 331, mwaka 2024 kesi 242 na kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu ni kesi 78. Kesi nyingi zinahusu wizi, udhalilishaji na ubakaji.

 Katika takwimu hizo, Hamza alikuwa akijibu swali la mwakilishi nafasi za wanawake, Shadya Mohamed Suleiman aliyetaka kujua hasa ni kesi zipi zinakuwa nyingi kwa mujibu wa taarifa za vyombo husika takwimu za kesi ambazo zimefikishwa katika Mahakama kisiwani humo.

 Awali, katika swali la msingi mwakilishi Ameir alitaka kujua kwa kiasi gani sheria mbalimbali zinazopitishwa katika baraza hilo zinazingatia kipengele muhimu cha haki za binadamu.

 Hata hivyo, akijibu swali hilo, Hamza amesema Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 10 (j), inaweka msingi muhimu wa kisheria kwa vyombo vyote vya Serikali na watumishi wake kuongozwa na kuzingatia mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binadamu pamoja na misingi ya utawala bora.

Kwa mujibu wa kifungu hiki, Katiba inatambuliwa kama sheria mama, hivyo, sheria zote zinazotungwa na mamlaka husika zinapaswa kuakisi na kulinda haki za binadamu kama zilivyoainishwa katika katiba na mikataba ya kimataifa ambayo Zanzibar ni sehemu yake. 

Katika kuhakikisha masharti hayo yanazingatiwa, amesema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekuwa ikishirikishwa katika hatua za mchakato wa utungaji wa sheria, hususani katika kutoa maoni na mapendekezo yanayolenga kuhakikisha sheria hizo hazivunji haki za binadamu bali zinaziimarisha. 

“Ushirikishwaji huu ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya Zanzibar ya kulinda, kuheshimu na kutekeleza haki za binadamu kwa mujibu wa matakwa ya katiba na viwango vya kimataifa,” amesema.

Related Posts