Mvutano huo hauishii kwenye majukwaa ya kampeni tu, bali umeenea kwenye fikra za wapiga kura, mitazamo ya wachambuzi wa siasa na hata ndani ya taasisi za utafiti.
Hata hivyo, mvutano huo unatokana na changamoto za kisiasa, kijamii au kiitikadi, huku sababu kubwa ikiwa ni tofauti ya uzoefu, uimara wa mitandao ya kisiasa, ushawishi wa waanzilishi na uwezo wa kifedha na kimuundo.
Kihistoria, Tanzania iliruhusu rasmi mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992 baada ya mabadiliko ya Katiba yaliyotokana na shinikizo la ndani na nje kuhusu demokrasia.
Hali hiyo ilizua wimbi la usajili wa vyama na kufikia Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, vyama kama NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), UMD na NRA vilishajiimarisha katika medani ya siasa.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa mwaka 2024, Tanzania ina jumla ya vyama 19 vilivyosajiliwa hadi Mei 2024, lakini si vyote vyenye ushawishi mkubwa au umaarufu wa kitaifa.
Vyama vilivyoanzishwa miaka ya 1990 vimekuwa na nafasi ya kuzoea muktadha wa siasa za Tanzania, kujijengea mitandao ya kitaifa, kushiriki chaguzi nyingi na kujifunza kutokana na mafanikio na changamoto mbalimbali.
Mathalan, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimekuwa kikitawala tangu mfumo wa chama kimoja, kilichorithi mtandao wa TANU na ASP.
Kimejijenga kitaasisi, kifedha na kimekuwa kikishinda kwa wastani wa asilimia 70 ya kura za urais tangu mwaka 1995. Katika uchaguzi wa mwaka 2020, CCM ilishinda kwa asilimia 84.4 ya kura za urais.
Kwa upande wa Chadema, kimekuwa chama kikuu cha upinzani tangu mwaka 2010. Katika uchaguzi wa 2015, mgombea wake wa urais, Hayati Edward Lowassa alipata asilimia 39.97 ya kura, kiwango kikubwa zaidi kuwahi kufikiwa na upinzani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.
CUF nacho kiliwahi kuwa chama chenye ushawishi mkubwa hasa Zanzibar, kikiongoza kwa karibu miaka 20 kama chama kikuu cha upinzani visiwani humo, kabla ya migogoro ya kiuongozi uliyokifanya kipoteze nguvu.
Kwa vyama vya NCCR-Mageuzi, UMD, NLD na UPDP viliwahi kuwa na sauti zenye nguvu katika miaka ya 1990 lakini baadaye ushawishi ulipungua kutokana na migogoro ya ndani, ukosefu wa fedha na kushindwa kuhimili ushindani wa kisiasa.
Vyama vipya kama ACT-Wazalendo iliyoanzishwa mwaka 2014, ADC, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Demokrasia Makini, AFP na CCK vinawakilisha kizazi kipya cha vyama vinavyojaribu kuleta mitazamo mipya ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Vyama vingi vipya havina matawi ya kutosha nchi nzima. Kwa mfano, katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2019, vyama kama Chaumma na ADC havikusimamisha wagombea katika zaidi ya nusu ya kata zote nchini, kwa mujibu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) mwaka 2020.
Mbali na hilo, ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2020, inaonyesha vyama vipya hukabiliwa na uhaba wa fedha za kampeni, hali inayovizuia kuwa na kishindo.
ACT-Wazalendo, licha ya kuwa na uongozi wenye mvuto wa kitaifa, kiliwahi kukiri kuwa, bajeti ya kampeni yake ya mwaka 2020 ilikuwa pungufu ya asilimia 20 ya ile ya CCM.
Sambamba na hilo, kwa kuwa vyama hivi havijawahi kuongoza Serikali kuu au hata majimbo mengi, wananchi wengi huvitazama kwa tahadhari.
Utafiti wa Taasisi ya Twaweza wa mwaka 2020, ulibaini asilimia 61 ya Watanzania huonyesha uaminifu mkubwa zaidi kwa vyama vilivyo na historia ya muda mrefu.
Aidha, Uchambuzi wa Mwelekeo wa Kisiasa Tanzania (REDET) uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mwaka 2021, ulioonyesha asilimia ya Watanzania waliokuwa tayari kupiga kura kwa kila chama.
Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 76 ya wananchi walikuwa tayari kuipigia kura CCM, huku asilimia 14 ni Chadema, ACT Wazalendo asilimia sita na vyama vingine ni asilimia nne.
Wanachosema wadau wa siasa
Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda anasema msingi wa mvuto na ushawishi wa chama cha siasa unaanzia kwa mwasisi wake.
Anaeleza kabla ya sera na falsafa nzuri, ushawishi wa chama cha siasa unaanzia kwa wasifu mzuri na kukubalika mbele ya jamii kwa mwasisi wa chama husika.
Anatolea mfano Chadema iliyoasisiwa na Mzee Edwin Mtei aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, nafasi ambayo ilimjengea ushawishi mbele ya umma.
“Chama lazima kiwe na watu na kianzishwe na watu wanaoweza kuwa na nguvu ya ushawishi. Chadema ilianzishwa na Mtei aliyekuwa Gavana na alikuwa na wasifu mkubwa kwenye jamii,” anaeleza.
Kwa mujibu wa Dk Mbunda, kihistoria vyama vingi vimeanzishwa na watu waliowahi kuwa na nafasi fulani serikalini, ndiyo maana imekuwa rahisi vyama vyao kujenga ushawishi pia.
Ameijenga hoja hiyo akimrejea marehemu Agustine Mrema aliyeasisi chama cha NCCR Mageuzi, akiwa tayari na ushawishi mbele ya jamii.
Dk Mbunda anasema hata ACT Wazalendo ilianzishwa na watu waliokuwa na ushawishi kina Profesa Kitila Mkumbo, Zitto Kabwe na kilichokipa nguvu zaidi ni ile ya kumeguka kwa CUF na kina Maalim Seif Sharif Hamad kuhamia.
“Utagundua kwamba vyama vyote vilivyokuwa na waasisi wenye ushawishi na vyenyewe vilipata ushawishi,” amesema.
Amesema vyama vingi vilivyoanzishwa baada ya mfumo wa siasa za vyama vingi, vilikosa waasisi wenye ushawishi ndio maana vinabaki kudorora ukilinganisha na vingine.
Mathalan, CCK anasema kingekuwa na ushawishi sasa iwapo kingelikuwa na waasisi waliojitokeza hadharani.
“Lakini zilisikika tu tetesi kwamba kina Samwel Sitta (marehemu) alikuwa sehemu ya kuanzishwa kwa chama hicho, bahati mbaya hakutoka hadharani,” anasema.
Anasisitiza ili chama kipate umaarufu, lazima wasifu wa waanzilishi uwe mkubwa na awe mwenye ushawishi mbele ya wengi.
Kwa upande wa mchambuzi wa masuala ya siasa, Kiama Mwaimu anasema vyama vingi vilivyoanzishwa miaka kadhaa baada ya mfumo wa siasa wa vyama vingi, havikujiandaa kushika hatamu.
Anasema ni ACT Wazalendo pekee ndicho kilichoamua kujitenganisha na vingine, chenyewe kinaonyesha kuwa na mikakati na kujijenga, ndiyo maana kinakuwa kwa kasi.
Hata hivyo, anahusisha hali ilivyonavyo vyama hivyo inachochewa na msingi wa kuasisiwa kwake, akidokeza yapo maslahi yaliyolengwa na sio kuwa na ushindani katika chaguzi.
“Haya mambo ya maslahi mengine ndiyo yanayosababisha vyama hivi vinaibuka nyakati za uchaguzi pekee, nyakati nyingine hutavisikia. Labda unapotokea mwaliko wa kushiriki mkutano ndiyo vitatokea,” anasema.
Mwaimu anaeleza kwa kuwa vyama hivyo vimejitambulisha kuwa vyama vya uchaguzi, hata mwenendo wake hauzingatiwi, ndio maana vimekosa wanachama zaidi ya viongozi wake.
“Ukifuatilia kwa undani ni vyama vilivyokuja kujaza nafasi kwa sababu huoni vikiwa na mikutano inayojaza wafuasi wengi,” anasema.
Hata hivyo, anasisitiza kwa hali ilivyonavyo, inasababisha vikose ruzuku na hatimaye kuangukia kwenye ukata kiasi cha kushindwa kujiendesha.
Mtaalamu wa Historia katika Siasa, Philemon Mtoi anasema sio kila chama kilichoanzishwa miaka kadhaa baada ya mfumo wa vyama vingi, kinalenga kushinda uchaguzi.
Kwa mtazamo wake, anaeleza baadhi ya vyama hivyo vimeibuka kama sehemu ya propaganda ya chama tawala na mara nyingi vinaifanya kazi yake kuwabeba watawala.
Hata hivyo, anasema si dhambi kwa watawala kuwa na propaganda za namna hiyo, kwa sababu kila chama kina uhuru wa kutumia mbinu yoyote kuhakikisha kinashika dola, isipokuwa kuvunja sheria za nchi.
Katika mazingira hayo, anasema usitarajie vyama hivyo vipya viwe na nguvu au ushawishi unaoshindana na vile vikongwe, kwa kuwa sababu za kuanzishwa kwake si kushindana bali kusaidia.
“Sio kitu cha kushangaza ni kitu kilichokuwepo katika dunia ya sasa. Baadhi ya vyama hivi vipya ni matokeo ya propaganda za vyama vikongwe, vimeanzishwa kimkakati,” anaeleza.
Kwa mujibu wa Mtoi, vyama vilivyoanzishwa wakati mfumo wa siasa za vyama vingi unaanza vilionekana dhahiri kuwa na nia ya dhati ya kushika dola na hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusifia sera ya kimojawapo.
“Unaona kabisa chama hakifanyi mikutano, kinasubiri uchaguzi hadi uchaguzi, unafikiri kitakuwa na nguvu sawa na kile kinachosimama siku zote kufanya siasa,” anasema.
Mtoi anasema katika historia NCCR Mageuzi, CUF na Chadema ni vyama vilivyoanzishwa vikionyesha wazi malengo yake, licha ya baadhi kupoteza mvuto kwa sasa.
Anasema vile vipya baadhi vimebaki kuwa vishiriki vya uchaguzi na havikuwahi kuwaza kuwa na ushindani katika siasa za nchi.
“Kuna vyama hata vinapotaka kufanya mikutano yake inabidi vipate usaidizi wa kifedha kutoka kwa watawala, sasa huyu atakuwaje na ushindani,” anasema.
Anasema ndiyo sababu kwa sasa inakuwa vigumu kukuta chama cha siasa kati ya vipya ukiacha ACT Wazalendo, vinasimama kuzungumzia masuala ya wananchi.
“Kuna vyama ambavyo wananchi wanaviangalia kama mustakabali wa Taifa na kuna vingine vinavyoonekana kwa ajili ya kubeba watu fulani. Wale wanaokuja kimsimu hawafanyi hata vikao hadi pale watakavyosaidiwa, haviwezi kuwa na ushindani na vyama vya zamani,” anasema.
Anasisitiza ili kupima nguvu vilivyonavyo vyama vya zamani na vipya, ni vema kuangalia sera zao, harakati na shughuli za kisiasa zinazofanywa na vyama husika.
Anaeleza vyama vya zamani vilianzishwa kwa sababu ya kushindana kwenye uchaguzi, ingawa havikuwahi kupata nafasi hiyo, lakini dhamira yao iko wazi.
Kwa upande wa vipya, anasema baadhi vimeonyesha mtazamo wa wazi kuwa havitarajii kushinda nafasi yoyote, zaidi ya kubaki hai ili vijitokeze nyakati za uchaguzi.
“Ni vigumu kushindanisha, hapa kuna anayetaka dola ingawa hakufanikiwa kuishika, halafu kuna yule anayetaka mkate wa kila siku ili aendelee kuishi,” anasema.