Dk Dimwa: Wanawake ni nguzo ya ukombozi, jitokezeni kugombea

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, ametoa wito kwa wanawake nchini kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia katika mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama hadi Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa baadaye mwaka huu.

Dk Dimwa ametoa wito huo leo Juni 11, 2025 alipokuwa akizungumza na Kikundi cha Wanawake wa Kikristo na Maendeleo Zanzibar, kanda ya Magharibi ‘B’, katika hafla iliyofanyika Kiembesamaki, Unguja.

Amesema CCM inatambua mchango mkubwa wa wanawake katika ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa, akisisitiza kuwa maendeleo yaliyofikiwa ndani ya chama hicho yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na nguvu kazi ya wanawake wanaosimamia kikamilifu masuala mbalimbali ya kisiasa na kimaendeleo.

“Natoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwani wana uwezo wa kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo. Dhamira ya Chama Cha Mapinduzi ni kuhakikisha wanachama wote wanapata haki na fursa sawa katika kuimarisha demokrasia,” amesema Dk Dimwa.

Aidha, ameeleza kuwa kwa mujibu wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025, chama hicho kimeweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha wanawake kwa njia mbalimbali ikiwemo mafunzo ya uongozi, uwezeshaji kiuchumi na kuhamasisha ushiriki wao katika siasa.

Ametolea mfano wa wanawake waliowahi kushiriki harakati za kisiasa tangu enzi za chama cha Afro Shiraz Party (ASP) na Tanganyika African National Union (TANU), akiwataja waasisi hao kuwa ni pamoja na Bibi Titi Mohamed, Bi Johari Yussuf Akida na Bi Mwanaidi Dai, ambao mchango wao umeendelea kuwa dira ya kuigwa katika ujenzi wa Taifa.

Katika hotuba yake hiyo, pia alizungumzia umuhimu wa kupinga vitendo vya ubaguzi wa kidini na kikabila, huku akiahidi kuwa CCM itaendelea kusimamia haki na usawa kwa wanachama wake wote bila ubaguzi.

Ameongeza kuwa chama hicho kinaendelea kudhibiti vitendo vya rushwa ili kuhakikisha kila mwanachama anapata haki anayostahiki kwa mujibu wa taratibu na miongozo ya chama hicho.

Dk  Dimwa amesisitiza pia umuhimu wa kulinda amani na utulivu uliopo nchini kwa sasa, akieleza kuwa hali hiyo ni msingi wa kufanikisha uchaguzi mkuu ujao kufanyika kwa amani na utaratibu unaokubalika.

Aidha, amebainisha kuwa ana imani CCM itapata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa 2025 kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025, ambayo imetekelezwa kwa mafanikio na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Hussein  Mwinyi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Catherine Peter Nao amesema wataendelea kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi nchini, ili kuongeza uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya maamuzi.

Catherine ameeleza kuwa kikundi hicho kimejipanga kuelimisha na kutangaza maendeleo yaliyotekelezwa na Serikali zote mbili ya Muungano na ya Zanzibar  ili wananchi wafahamu kazi mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali iliyopo madarakani.

Related Posts