Majimbo haya Singida usibeti, kila mtu bingwa

Singida. Ni kama watu wanaoisubiri ile siku ya kuja Masihi! ndivyo ilivyo kwa makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wenye nia ya kugombea ubunge katika majimbo ya Mkoa wa Singida huku kila mmoja akiota kwamba kuna mtu ‘amekanyaga waya’ ili siku zisitembee.

Hiyo inajidhihirisha kwa namna joto lilivyopanda huku makada wakianza kujipitisha kwenye mikusanyiko na ahadi lukuki kwa wananchi lakini minada na magulio vimekuwa sehemu ya kampeni za chini kwa chini ukiacha misiba, na mikusanyiko ya sherehe za kimila na za kwaida.

Majimbo matatu kati ya manane yaliyopo mkoani Singida hayatabiriki, kwa sababu inaelezwa huenda yeyote anaweza kupenya kutokana na nguvu za ushawishi kutoka kwa wagombea wanaoyanyemelea kwa sasa.

Wakati hayo yakionyesha wazi kuwa yanaweza kunyakuliwa, Jimbo la Ilongero (Singida Kaskazini) kuna fukuto kubwa huku likitajwa kwamba kutakuwa na mchuano mkali ikiwa makada wawili maarufu nchini atarusha kete zao licha ya kutoweka wazi.

Majina ya Haidali Gulamali na Lazaro Nyalandu yanatajwa sana na wakazi wa jimbo hilo huku ikielezwa kwamba mchuano ni mkali kutokana na rekodi zao na uwezo wa kiushawishi.

Nyalandu aliwahi kuliongoza Jimbo hilo kwa vipindi viwili na nusu kwa sababu hakumaliza kipindi cha tatu baada ya kujiuzuru.

Gulamali ambaye amewahi kushika nyadhifa kadhaa ikiwemo uhasibu wa Chama Mkoa wa Dodoma, aligombea na Mbunge wa sasa, Abeid Ighondo na aliongoza kura za maoni lakini aliingia matatani akituhumiwa kwa rushwa.

“Kama Nyalandu na Gulamali wataingia kwenye tatu bora, vita itakuwa kali na sijui itakuwaje, lakini wakitaka wamuondoe mmoja kati yao ndipo mbunge anaweza kupata kura japo chache,” anasema Ayubu Ngaa mmoja wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa Singida.

Baada ya mabadiliko madogo ya Katiba ya CCM, Mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa anahusika upogaji kura katika ngazi zote za kupitisha watia nia wa nafasi ya ubunge.

Mjumbe huyo anasema ubashiri wa kupata mbunge kati ya Gulamali na Nyalandu ni mgumu kwa kuwa wote wana mbinu zisizokaririwa, hivyo wajumbe wanaweza kuingia na misimamo yao.

Mtiti mwingine utakuwa Jimbo la Itigi ambalo zamani lilitwa Manyoni Magharibi kabla ya mgawanyo wa majimbo mapya na menginw kubadilishwa majina uliofanywa na Tume ya Uchaguzi hivi karibuni. Jimbo hilo linaongozwa na Yahya Masare.

Majina ya watu wanne yanatajwa kuliwania, lakini yalinatajwa sana ni majina mawili ambayo ni Yohana Msita ambaye ni MNEC wa CCM Mkoa Singida na mfanyabiashara maarufu, Msafiri Nghambi, wanamfanya Masare asilale.

Kwenye kinyang’anyilo hicho, Nghambi anapewa nafasi kubwa kutokana na mazingira ya maisha yake na biashara zake, yanamfanya ajulikane maeneo mengi huku akielezwa ni mtu anayejishusha kwa watu wa hali ya chini licha ya ukwasi alionao.

Jimbo la Manyoni Mashariki ambalo pia limebadilishwa jina sasa linaitwa Manyoni, hilo linaonekana kuwa jepesi zaidi kutokana na aina ya wagombea walioonyesha nia ingawa lolote linaweza kutokea kwa kuwa muda bado.

Lakini inaelezwa, Mbunge wa Jimbo hilo, Dk Stephen Chaya ni kama anapita kwenye njia isiyo na miiba ingawa yeye anasema hawezi kumdharau mtu.

“Wanaotupa ridhaa ni wajumbe, siwezi kuwasemea wanataka nini, lakini mengi tumeyatekeleza mimi na madiwani wangu na kwa kweli naamini watanipa ridhaa tukamilishe tuliyoanzisha,” amesema Dk Chaya.

Vita ya ndani ya Ukumbi wa Bunge kati ya Miraj Mtaturu na Nusrat Hanje inahamia katika Jimbo la Ikungi na tayari wawili hao walishaingia katika tambo mbele ya wajumbe.

Nusrat ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum kutoka kundi la wabunge 19 walioingia kwenye utata na chama chao (Chadema), anatajwa kutaka kuhamia CCM.

Na hata katika mkutano wa Bunge la bajeti unaendelea jijini Dodoma, mbunge huyo amekuwa akitembelewa na wageni wakiwamo viongozi wa CCM wilaya ambao hutambulishwa bungeni.

Hata hivyo, Mtaturu alipotakiwa kueleza amejipangaje kwenye ushindani huo, anasema; sina shida na huyo dada yangu, wajumbe wanajua yeye ni mpitaji tu na siyo mtu wa pale isipokuwa anataka kujionyesha.”

Mbunge wa Viti Maalum, Jesca Kishoa ni sawa na Simba mwenda pole anayeliwinda Jimbo la Iramba Mashariki ambalo lipo kwenye himaya ya Isack Mtinga.

Moja ya wabunge ambao wamejionyesha hadharani kwamba anakihama chama chake ni Kishoa ambaye picha kadhaa zimekuwa zikimuonyesha akiwa na mavazi ya kijani na nyeusi ambazo ni sare za CCM na mikutano yake hugawa vitenge vya chama hicho Tawala.

Hata hivyo, Mtinga (Katibu wa zamani wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa) bado anaonekana kuwa na nguvu licha ya upande mmoja kuwa na minong’ono kwamba amekuwa na uongozi wa ukanda.

Jimbo la Singida mjini halitabiriki, wengi wanasema lina joto lakini wanamtaja Mbunge wa sasa, Mussa Sima kuwa amekuwa na mipango isiyotabirika wakati wa kampeni.

Sima tangu alipochukua Jimbo hilo baada Mohamed Dewj (MO) alipoamua kwa hiyari yake kuliachia mwaka 2015, hajapata kashikashi kubwa.

Wengine ambao wenye asilimia kubwa za kurejea katika nafasi zao na wametangaza kugombea ni Dk Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi) na Elibariki Kingu wa Singida Magharibi.

Awali, Dk Mwigulu alitajwa kukutana na mwanahabari, Mathias Canali lakini mwanahabari huyo alipoulizwa na Mwananchi juu ya hilo, alisema bado anawaza kuwatumikia wananchi kwa nafasi nyingine si ya ubunge.

Wana CCM mkoani Singida wanataja msimamo mkali wa Kamati ya siasa ya Mkoa chini ya Mwenyekiti wake, Martha Mlata huenda ukachagiza kupata wagombea wenye sifa njema mbele ya wapiga kura.

Singida imekuwa na historia ya kuongozwa na wabunge kutoka vyama vya upinzani, katika vipindi viwili mfululizo, Jimbo la Singida Mashariki (Ikungi) alikuwa akishinda Tundu Lisu (Chadema) huku katika maeneo mengine wamekuwa wakishinda madiwani wa chama hicho hali inayohitaji kuwa na wagombea wanaokubarika zaidi.

Related Posts