Majimbo ya uchaguzi Zanzibar yanahitaji uwazi, uadilifu

Uchaguzi ni miongoni mwa mambo muhimu yanayopaswa kufanyika kwa uwazi, uadilifu na bila kuacha mashaka yoyote. Pale ambapo mchakato huu unakosa misingi hiyo, ndipo nchi hujikuta ikikumbwa na matatizo ambayo yangeliweza kuepukika.

Moja ya masuala ambayo yamekuwa yakiibua mjadala mkubwa Zanzibar ni kuhusu upangaji wa majimbo ya uchaguzi.
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) mara nyingi imekuwa kimya, bila kutoa maelezo au kuruhusu hoja za wananchi kuhusu uamuzi wake.
Mfano wa wazi unaoonyesha ukosefu huu wa uwazi ni jinsi majimbo matano ya Mji Mkongwe na maeneo ya jirani yalivyofutwa na kufanywa kuwa jimbo moja.
Zamani kulikuwa na majimbo ya Malindi, Mkunazini, Mlandege na sehemu za Kikwajuni na Makadara.
Wapinzani kutoka ACT Wazalendo (zamani CUF) wanadai maeneo hayo ni ngome yao ya kisiasa, na hatua ya kuyaunganisha ilikuwa ya makusudi ili kupunguza uwakilishi wao.
ZEC haijatoa maelezo kuhusu mabadiliko hayo makubwa, ambapo majimbo matatu kamili na sehemu za mawili yaligeuzwa kuwa jimbo moja. Hili limeendelea kuibua maswali miongoni mwa wananchi.
Wakati huo huo, katika uchaguzi wa 2020, liliundwa jimbo jipya la Fuoni, licha ya kuwa na wapiga kura wasiozidi 1,600, idadi ambayo ni ndogo kuliko ile ya kawaida ya jimbo, ambayo ilitarajiwa kuwa watu wasiopungua 10,000.
Hali hiyo imeacha maswali mengi: je, kuna usawa na haki katika ugawaji wa majimbo?
Je, wananchi wanaweza kuwa na imani na mchakato wa uchaguzi ikiwa kuna tofauti kubwa kama hizi?
ZEC inapaswa kufafanua hadharani ni kwa msingi upi jimbo la Fuoni liliundwa kwa idadi ndogo ya wapiga kura, tofauti na miongozo iliyowekwa.
Kama kulikuwa na makosa au changamoto zisizozuilika, basi ingetakiwa kuona marekebisho kabla ya uchaguzi ujao.
Vivyo hivyo, ZEC inawajibika kueleza sababu za kuunganisha maeneo ya Mji Mkongwe hadi kuwa jimbo moja, hali iliyofutwa kwa namna isiyoeleweka.
Hili ni jambo linaloweza kuzusha mvutano na kuathiri amani ya uchaguzi. Zanzibar ina historia ndefu ya migogoro ya uchaguzi.
Ni wajibu wa ZEC kuhakikisha hali hiyo haitokei tena kwa kuweka uwazi, kusikiliza malalamiko ya wananchi na kufanya maamuzi kwa misingi ya haki.
Viongozi wa ZEC na watendaji wake wanapaswa kufahamu kuwa amani, usalama na matumaini ya Wazanzibari yako mikononi mwao.
Historia itawahukumu kwa wema au kwa makosa yao, kulingana na jinsi watakavyoendesha uchaguzi ujao.
Kadri tunavyokaribia uchaguzi mkuu, sauti za chuki kutoka kwa baadhi ya wanasiasa zimeanza kusikika. Ni lazima kauli kama hizi zikemeewe – bila kujali chama au nafasi ya anayezitoa.
Vile vile, ni muhimu uchaguzi uonekane kama tukio la kawaida katika maisha ya kila siku ya wananchi, si kipindi cha taharuki.
Katika chaguzi zilizopita, magari ya kijeshi yalitembea na bendera nyekundu kana kwamba nchi ipo vitani.
Askari walilaumiwa kwa kuwatia hofu wananchi, kuvamia mikusanyiko ya amani na kuwapiga watu kana kwamba ni mazoezi ya kijeshi.
Wakati wa uchaguzi, ndipo yanapoibuka makundi kama Janjaweed au Mazombi, ambao hudaiwa kuvamia nyumba za raia, kupiga, kupora mali na hata kufanya vitendo visivyofaa kwa jamii ya Visiwani.
Haya ni mambo ya hatari yanayopaswa kudhibitiwa haraka na Jeshi la Polisi, ambalo lina jukumu la msingi la kulinda usalama wa raia na mali zao.
Uchaguzi mkuu uko karibu. Hatuna muda wa kupoteza. Ni wakati wa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha uchaguzi wa 2025 unakuwa wa amani, huru, wa haki na unaoheshimu utu na usalama wa kila Mzanzibari.

Related Posts