Rorya. Kuishi na mwanamke kwa takriban miaka minne bila kufunga ndoa kunadaiwa kuwa chanzo cha mtafaruku mkubwa wa kifamilia wilayani Rorya, mkoani Mara, hali iliyosababisha mwanamke mmoja na mtoto wake wa mwaka mmoja kujeruhiwa vibaya kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali.
Night Mchama (27) na mwanawe kwa sasa wamelazwa katika Hospitali ya Kanisa la Mennonite (KMT) Shirati wakipatiwa matibabu baada ya tukio hilo la kushangaza na kusikitisha ambalo linadaiwa kufanywa na mzazi mwenzake, Jacob Ngoro.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni uamuzi wa Night kukataa kuendelea kuishi na mwanamume huyo baada ya kushindwa kulipiwa mahari, licha ya kuishi naye kama mume na mke kwa kipindi cha takriban miaka minne.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dk Halfan Haule amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa vyombo vya usalama vinaendelea kumtafuta mtuhumiwa ambaye alikimbia baada ya kufanya tukio hilo.
“Tukio lipo, mwanamke bado yupo hospitalini ila mtoto ametibiwa na kuruhusiwa. Tunaendelea kumtafuta mtuhumiwa kwani alikimbilia kusikojulikana baada ya kuwajeruhi mama na mtoto,” amesema Dk Haule.
Akizungumza akiwa hospitalini jana Juni 10, 2025, Night alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Juni 3, 2025, asubuhi baada ya kuvamiwa na mume wake aliyemtaka warejee kuishi pamoja ikiwa ni baada ya Night kurudi nyumbani kwao.
“Nilimkatalia nikamwambia kuwa lazima alipe mahari kama ambavyo baba ameelekeza. Ndipo akasema kuwa kumbe mimi na baba letu ni moja, akachomoa panga na kuanza kunikata na kunichoma sehemu mbalimbali za mwili wangu,” alisema.
Night alieleza kuwa alianza kuchomwa bega la kulia mara tano, kisha akageuka na kuchomwa mgongoni, mapajani na tumboni, huku mtuhumiwa huyo akishindilia panga kabla ya kukimbia baada ya kusikia sauti za watu.
Alisema kuwa wakati wa tukio hilo alikuwa nje kidogo ya mji wa wazazi wake akiokota kuni akiwa amembeba mtoto wao mgongoni. Kwa mujibu wa Night, mtoto pia alijeruhiwa kwa kukatwa panga mapajani, tumboni na begani.
Night aliongeza kuwa alitoroshwa kutoka nyumbani kwao na kuanza kuishi na mwanamume huyo kama mume na mke baada ya kumaliza kidato cha nne, ambapo majibu yalipotoka alipata ufaulu wa daraja la tatu na alitakiwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano. Walianza maisha ya ndoa nchini Kenya kwa mwaka mmoja kabla ya kurejea kijijini hapo.
Hata hivyo, Mei 24, 2025, wazazi wake walimfuata na kumtaka arejee nyumbani hadi atakapolipiwa mahari. Hilo lilifuatia kifo cha baba mkwe wake ambapo kwa mujibu wa mila zao, hakuruhusiwa kushiriki msiba huo hadi awe mke halali.
“Hakukubaliana na wazazi wangu na hata siku hiyo alitaka kufanya fujo, lakini mimi ilibidi niondoke. Kumbe baada ya kuondoka na yeye akawa na mipango yake, ndipo siku ya tukio alipofika nyumbani kwetu asubuhi na kuniambia tutoroke. Nilipokataa ndipo yakatokea haya,” alisema.
Baba wa Night, France Nyerere alisimulia kuwa alikuta binti yake amelala chini akiwa anavuja damu nyingi sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Nilikuwa bado nimelala niliposikia kelele za kuomba msaada. Nilipotoka nje nilimkuta binti yangu akiwa analia huku mwili wote umetapakaa damu. Nisijue cha kufanya ndipo akanionyesha panga lililokuwa tumboni kwake na kuniomba nilitoe,” alisema.
Alisema alifanikiwa kulitoa panga hilo na baadaye watu waliendelea kufika eneo la tukio na kuwasiliana na polisi ambao walikuja na kuwapeleka majeruhi hospitali.
Daktari wa zamu katika Kitengo cha Dharura cha Hospitali ya KMT Shirati, Chrispin Msabi alisema walimpokea Night akiwa katika hali mbaya na aliwahishwa chumba cha upasuaji ambapo walibaini kuwa alikuwa amechanwa utumbo mwembamba na mshipa mkubwa wa damu.
“Tulilazimika kuukata utumbo mara mbili ili kuuunganisha tena kabla ya kumpeleka ICU kwa uangalizi wa karibu. Kwa sasa ametoka katika hali ya hatari ingawa bado hali yake sio nzuri na itachukua muda kupona,” alisema Dk Msabi.
Aliongeza kuwa mgonjwa hataruhusiwa kula vyakula vigumu kwa miezi sita, hivyo asipopata lishe laini na kamili anaweza kuathirika kwa utapiamlo au hata kupoteza maisha.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyahera, Joseph Sausi alithibitisha tukio hilo na kusema walitoa taarifa kituo cha polisi Shirati ambao waliwapeleka majeruhi hospitali. Alisema uongozi wa kijiji unaendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kumtafuta mtuhumiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Mark Njera alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa alikimbilia nchini Kenya baada ya kufanya tukio hilo.