Maumivu ya maji, wananchi wakesha kuyasubiri Dar

Dar es Salaam. Upatikanaji huduma ya maji umeendelea kuwa wa kusuasua katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam hali inayosababisha wakazi wa maeneo hayo kukesha usiku wakisubiri maji.

Kutokana na kukosekana kwa maji katika baadhi ya maeneo wapo wanaolazimika kununua ndoo moja ya maji kwa gharama ya Sh300 hadi Sh1,000 hali inayowagharimu kiuchumi.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ya mwaka 2024 kaya za kipato cha chini Dar es Salaam zinatumia kati ya asilimia 15 hadi 25 ya kipato chao cha kila mwezi katika kupata maji safi.

Hali hiyo ni kinyume na miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inayopendekeza kaya kutumia si zaidi ya asilimia 3 ya kipato kwa huduma ya maji.

Hata hivyo, Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) imesema changamoto iliyosababisha uhaba huo wa maji ilishamalizwa ndani ya saa 14 baada ya kukamilika kwa matengenezo ya mabomba makubwa, kazi iliyofanyika kati ya Juni 8 na Juni 9, 2025.

Mwananchi imezungumza na baadhi wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameeleza kwa siku kadhaa kumekuwa na changamoto ya maji ingawa katika baadhi ya maeneo huduma hiyo imeanza kurejea.

Mkazi wa Tabata, Mirfat Juma amesema wakazi wa maeneo hayo wakati mwingine hulazimika kukesha usiku wakisubiri maji kama ambavyo ilitokea usiku wa  Juni 10, 2025 ambapo maji yalitoka baada ya kutopatika kwa wiki nzima.

“Kwa wiki nzima tumekuwa hatupati maji kabisa. Jana yametoka kuanzia saa sita usiku hadi saa nane. Hapo aliyewahi kushtuka anajaza vyombo vyake ndipo awaamshe na wengine kama msaada,” amesema Mirfat Juma.

Mirfat amesema hali hiyo inawapasa kupanga zamu ya kuchota maji kwa haraka kabla hayajakatika, huku wengine wakilazimika kubeba madumu mazito kwenye giza au kuamsha watoto ili kusaidiwa.

“Ni hatari sana, hasa kwa watoto na kina mama. Tunahangaika na ndoo mikononi, wengine wanateleza na kuanguka na sehemu ya kusubiri kuna kuwa na mbu na asubuhi wafnayakazi wanatakiwa kwenda kazini na wanafunzi shuleni,” amesema.

Eva Israel, mkazi wa Kinyerezi amesema kutotoka maji mara kwa mara wamejikuta wakivuna maji ya mvua zaidi.

“Tunaweza kukaa zaidi ya wiki mbili hakuna maji lakini ukashangaa kipindi cha mvua na wao wanaachia maji kwa hiyo wakazi wa huku wanajikuta wakichota maji ya mvua zaidi kuliko ya Dawasa kwa sababu wakati wanapoyahitaji hakuna wanapopata maji mengine yanatoa,” amesema Eva.

Living Sambua, mkazi wa Tabata Matumbi amesema kukosekana kwa maji katika eneo lao ni kawaida na inaweza kupita wiki hakuna maji na hata inapotokea bomba limepasuka hakuna anayejali kwa wahusika.

“Tunalalamika hakuna maji katika maeneo yetu halafu unakuta bomba limepasuka mtaani inaumiza, wahusika kama hawana muda na wakati mwingine wanapita wakiwa wanakwenda kusoma bili za maji,”amesema Sambua.

Kilio cha uhaba wa maji kilisikika pia katika maeneo mengine ya jiji hilo ikiwemo Kariakoo, Oysterbay, Kimara, Magomeni, Upanga, Mwenge na Mikocheni.

Mkazi wa Kimara King’ongo, Ashura Mohammed amesema eneo hilo limekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji.

“Hata yakitoka hiyo mara moja moja ni nyakati za usiku wa manane ambao watu wanakuwa wamelala hivyo kusababisha kushindwa kupata huduma hiyo,” amesema.

Ameeleza ili kupata huduma hiyo muhimu inawalazimu kununua maji hayo kwa wauzaji wanaotumia mikokoteni kusambaza majumbani jambo linaloongeza gharama za maisha.

“Dumu moja la maji ya bomba tunanunua kwa kati ya Sh500 hadi Sh700, kwa yale ya chumvi hugharimu Sh300 hadi Sh400, hii inatuumiza sana kutokana na kuongezeka kwa gharama za maisha”amesema.

Mkazi wa Magomeni, Abdulrahman Idd amesema:”Kwa siku nne mfululizo hatukupata huduma ya maji, sio Magomeni pekee naambiwa hali ipo katika maeneo mengine tulipata wakati mgumu.”

“Ingawa hivi sasa yanatoka, lakini si kwa mtiririko mzuri, yanaweza kutoka asubuhi mchana hayatoki. Tunaiomba mamlaka husika itusaidie utatuiz wa changamoto hii, maji yanatutesa sana hatuyapati kwa uhakika zaidi,” amesema.

Kilichosababisha hali hiyo

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Dawasa, Everlasting Lyaro amesema kulikuwa na changamoto iliyosababisha upatikanaji mdogo wa maji hasa kwa wakazi wa jiji hilo wanaotegemea maji kutoka mtambo wa Ruvu chini.

Amesema usiku wa Juni 8, 2025 kulikuwa na marekebisho ya mabomba makubwa hali iliyosababisha kupunguzwa kwa uzalishaji maji katika mtambo huo kwa asilimia 25.

“Kwa kawaida mtambo wa Ruvu Chini ambao ndiyo unahudumia eneo kubwa la Jiji la Dar es Salaam huwa unazalisha maji lita 270 milioni, lakini kwa saa 14 tangu saa sita usiku wa Juni 8 hadi saa nane mchana Juni 9 maji yalikuwa yanazalishwa kwa asilimia 75 pekee ili kuruhusu marekebisho ya mabomba makubwa.

“Marekebisho haya yalisababisha maji yaende kwa msukumo mdogo hivyo hata maji yalikuwa yanatoka kwa pressure ndogo ilikuwa haiwezekani kupanda juu hasa kwa wale wanaohifadhi kwenye matenki.

Hii iliathiri maeneo mengi kuanzia Bagamoyo, Bunju, Tegeta, Mwenge, Mikocheni, Magomeni hadi Ilala yani kwa kifupi ni mtambo unaotegemewa na asilimia 50 ya wakazi wa Dar,” amesema Everlasting.

Hata hivyo, mkuu huyo wa mawasiliano amesema uzalishaji umesharejea katika hali ya kawaida na sasa kiasi chote cha lita 270 milioni kinazalishwa na mtambo wa Ruvu Chini.

Kuhusu wakazi wa jiji hilo wanaohudumiwa na mtambo wa Ruvu Juu inayohusisha maeneo Kibaha, Mbezi, Kimara, Ubungo, Tabata, Mabibo na mengineyo amesema wanaendelea kupata maji kwa awamu.

“Mtambo huu unazalisha lita 196 milioni kwa siku, huu hauna changamoto yoyote isipokuwa kutokana na uhitaji mkubwa unaosababishwa na ongezeko la watu na mahitaji ya maji huduma hii inapatikana kwa awamu, sio mgao ni awamu hii ni kuhakikisha wote wanapata maji.

“Huu ukanda unahusisha viwanda, makazi na shughuli nyingi zinazohitaji maji na ikumbukwe kwamba kuna ongezeko kubwa la watu katika maeneo hayo hivyo tumeweka utaratibu wa maji yapatikane kwa awamu. Kwa sasa upatikanaji wa maji ni kati ya saa 8 hadi 12 ila matamanio yapatikane kati ya saa 12 hadi 16,” amesema na kuongeza:

“Katika hili tunasisitiza wananchi wawe na utaratibu wa kuhifadhi maji, pia jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika kuhakikisha tunapata vyanzo vitakavyowezesha kuongeza uzalishaji wa maji. Mradi wa bwawa la Kidunda, mradi wa kutoa maji bwawa la Mwalimu Nyerere na kuongeza uzalishaji wa visima vya Kisarawe 2 hii yote ikikamilika uzalishaji wa maji utakuwa wa kutosha,” amesema Everlasting.

Kufuatia hali hiyo wananchi wameshauri Serikali kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo, pamoja na kuweka mikakati ya kudumu ya kuhifadhi maji na kuongeza vyanzo vya uhakika.

“Hii ni huduma ya msingi kama elimu na afya. Hatuwezi kuendelea kuishi kama tunapambana na janga la kitaifa kila siku, tunataka maji ya uhakika hizi nyingine ni hadithi tu,” amesema Abdallah Mfaume, mkazi wa Kigamboni.

Related Posts